Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Maisha
Bora kwa Watanzania hajawezi kuja kwa
watu kushinda wanacheza mchezo wa pool badala ya kujihangaisha kwa kufanya kazi
na shughuli nyingine za kujiingizia mapato.
Aidha, Rais Kikwete
ameahidi kuwa Serikali yake itakomesha haraka iwezekanavyo kero ya wananchi wa
sehemu za Mkoa wa Njombe kulazimika kupanda mitini ili kupata mawasiliano ya
simu za mkononi.
Rais Kikwete
amayesema hayo leo, Ijumaa, Oktoba 18, 2013, wakati alipohutubia mkutano wa
hadhara katika Kijiji cha Wanginyi, Kata ya Lupembe, Wilaya ya Njombe katika
Mkoa Mpya wa Njombe kwenye siku yake ya kwanza katika ziara yake ya siku saba
kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa huo.
Akizungumza na wakazi
wa Kijiji hicho na vijiji vya jirani, Rais Kikwete amezungumzia dhana nzima ya
Maisha Bora kwa Watanzania akisisitiza kuwa maendeleo na Maisha Bora kwa Kila
Mtanzania hajawezi kupatikana kwa watu kushinda wanacheza mchezo wa pool mchana
kucha.
“Ndugu zangu,
nimepata kusema huko nyuma na nataka kurudia tena kuwa Maisha Bora kwa Kila
Mtanzania yanawezekana kwa watu kujituma na kuchapa kazi na siyo kwa watu
kushinda kwenye meza za pool wakipiga kale kampira huko wakiilaumu Serikali na
kuulizana ‘Maisha Bora yako wapi?’”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Inawezekana kweli Maisha Bora yakaja kwa mtu anayeshinda anagonga
mpira wa pool kwenye meza? Ni kwa kufanya kazi kwa bidii na shughuli nyingine
za kutuingizia kipato ndipo maisha yetu yatakapokuwa bora.”
Kuhusu hali ya
mawasiliano ya simu Mkoani Njombe, Rais Kikwete, baada ya kuwa ameambiwa kuwa
katika baadhi ya sehemu za Mkoa huo, watu wanalazimika kupanda juu ya miti ili
kupata mawasiliano, alisema kuwa Serikali yake itakomesha haraka kero hiyo.
“Ni ajabu na aibu kabisa
kwamba watu wanalazimika kupanda miti ili kupata mawasiliano….Hii ni hatari …
kwa sababu mtu anaweza kuanguka na kuvunja viungo…mtu anaweza kuvunja kiuno,”
alisema Rais Kikwete huko watu wakiangua kicheko.
“Tutahakikisha kuwa
watu hawavunjiki viungo kwa sababu ya kupiga ama kupokea simu za ndugu zao,”
Rais Kikwete amewahakikishia wana-Njombe.
Katika kufafanua azma
hiyo ya Serikali kumaliza kero hiyo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Serikali italimaliza
tatizo la mawasiliano katika Mkoa wa Njombe kwa awamu mbili.
Alisema kuwa katika
awamu ya kwanza, kiasi cha sh milioni 260 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha
mawasiliano katika vijiji 25 vya Jimbo la Uchaguzi la Njombe Kaskazini na kuwa
kazi hiyo itakuwa imekamilika ifikapo Machi, mwakani, 2014. “Tunataka watu
waache kupanda miti kwa kutafuta mawasiliano ya simu tu.”
Amesema kuwa katika
awamu ya pili, kiasi cha sh bilioni 1.552 zitatumika kutoka Mfuko wa
Mawasiliano Vijijini kwa ajili ya kuboresha mawasiliano ya simu katika Mkoa
mzima wa Njombe.
Amesema kuwa kazi ya
kuboresha mawasiliano katika awamu hiyo ya pili, itakamilika ifikapo Agosti,
mwakani, 2014.
Kuhusu matumizi ya
simu zenyewe, Mheshimiwa Mbarawa amewataka Watanzania kuzitumia simu hizo za
mkononi vizuri kwa mawasiliano ya maana na yasiyokuwa na ovyo ikiwa ni pamoja
na kutukana watu. “Tuzitumie simu zetu vizuri kwa mawasiliano mazuri na ya
maana na siyo kutumia simu kujenga na kusambaza fitina na majungu ama kushiriki
matusi dhidi ya watu wengine.”
Baadaye jioni, Rais
Kikwete alikuwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika sherehe za Uzinduzi Rasmi
wa Mkoa wa Njombe kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.
No comments:
Post a Comment