KAMPUNI ya Huawei ya China ina mpango wa kuzisaidia shule za sekondari 150
nchini Tanzania ili ziwe zikipata mafunzo kwa njia ya mtandao wa mawasiliano (E-Education)
kama njia ya kukabiliana na uhaba wa walimu na vitabu vya masomo.
Hayo yameelezwa jana (Jumapili, Oktoba 20, 2013) na Rais wa Kampuni hiyo, Bw. William
Xu alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye makao makuu yao jijini
Shenzhen, China.
Alisema walipokea maombi ya Serikali ili kuona jinsi
mkongo wa mawasiliano ya Taifa (NCITBB) utakavyoweza kuinua kiwango cha elimu
ya watoto wa Kitanzania kwa kiasi kikubwa. Kampuni ya Huawei ndiyo iliyojejenga
mkongo huo.
Alisema kwa kuanzia mradi huo utazihusu shule 50 ambapo
shule mbili kutoka kila mkoa zitaunganishwa kwenye mtandao saa zote (ziko
online) zikiwa na madarasa ya kujifunzia teknolojia mpya (multimedia
classrooms), maabara ya kompyuta (computer lab), projekta, mafunzo ya kwenye mtandao
yanayofundishwa kwa njia ya video, (Online video teaching) na (online
applications).
“Shule nyingine 100 zimekwishaainishwa lakini zenyewe zitakuwa
zikipata mafunzo offline (hazitakuwa mtandaoni moja kwa moja), bali katika
awanu ya pili zinaweza kuunganishwa na kuwa online kutegemea na upatikanaji wa
intaneti na kasi yake,” alisema.
Alisema shule hizi zitakuwa zikipokea mawasiliano kutoka
kituo chao kikuu ambacho kimejengwa Dakawa, Morogoro.
Vilevile Bw. Xu alimkabidhi Waziri Mkuu hati ya makabidhiano
ya msaada wa dola za marekani 155,000 kwa ajili ya ujenzi wa ujenzi wa madarasa
mawili na vifaa vya komputa kwa shule ya msingi Kibaoni ambayo alisoma Waziri
Mkuu iliyoko wilayani Mlele, Katavi.
Akitangaza matumizi ya msaada huo, mtaalamu kutoka
kampuni ya Huawei, Bw. Moses Hella alisema msaada huo utatumika kujenga madarasa
mawili moja likiwa computer lab na jingine ni darasa la kujifunzia teknolojia
mpya (multimedia classroom), kompyuta 50, laptop tano kwa ajili ya walimu, Huawei
tablets 100 na audio system.
Kwa upande wake, Waziri Mku aliishukuru kampuni hiyo kwa kukubali
kutumia teknolojia yake katika kuendeleza elimu nchini kwa kuanzisha mfumo wa E-Education kwenye shule 50 kwa wakati
mmoja.
Aliishukuru pia kampuni hiyo kwa
kukisaidia Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela cha Arusha na
kuongeza kuwa angependa kuona chuo hicho
kinakuwa cha mfano katika maeneo ya utafiti na teknolojia ya mawasiliano barani
Afrika.
Kuhusu msaada kwa shule ya msingi
Kibaoni, Waziri Mkuu aliwashukuru kwa kumuunga mkono katika kampeni yake ya
kuhakikisha amefanya kitu kuisaidia shule hiyo ambayo alisoma kati ya mwaka
1957 na 1960.
“Ninawashukuru sana kwa msaada huu.
Niliahidi kwamba kabla sijaondoka madarakani nataka nifanye jambo la ukumbusho
kwa manufaa ya jamii ya eneo lile. Kwa kweli nawashukuru sana kwa kutupatia
msaada huu naamini kuwa shule hii sasa ni ya kisasa na wanafunzi wake watakuwa na
elimu ya teknohama na siyo wa BBC (born before computers) kama mimi.
Alisema ataikabidhi hati hiyo kwa
viongozi wa Halmashauri yake ili watunze kwenye rekodi zao.
Shule ya msingi Kibaoni aliyosoma imechakaa,
eneo ilipo ni dogo sana na haifai kwa ukarabati. Ili kukamilisha azma yake, Waziri Mkuu aliomba Halmashauri ya Wilaya ya
Mlele itafute eneo jipya ili ujenzi wa shule hiyo ukikamilika, wanafunzi
walioko katika shule hiyo wahamie kwenye shule mpya. Hadi sasa madarasa 12
yamekwishajengwa na kuezekwa.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya sita ya ziara yake
ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya China leo asubuhi amewasili
Chengdu ambako atakuwa na mikutano mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, OKTOBA 21, 2013
No comments:
Post a Comment