Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka
ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kusini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa
CCM yuko katika ziara ya kiaina jimboni kwake. Akidai kwamba hataki
kuwasumbua wananchi kwa matayarisho ya ujio wake, anaingia katika kijiji
kimoja baada ya kingine na kukutana na wananchi kwa matembezi ndani ya
kijiji ili ajithibitishie kwa macho kero na changamoto hizo na
kuzitafutia ufumbuzi.
Jumapili tarehe 19 oktoba ametembelea
kijiji cha Bihanga kata ya Burungura na kushuhudia shule ya msingi yenye
madarasa manne yaliyoezekwa kwa nyasi. Wanafunzi walimueleza adha kubwa
wanayoipata wakati wa mvua. Utoro katika shule hiyo ni mkubwa kwa
sababu ya mazingira mabaya. Akakaa na viongozi wa kijiji na wananchi na
kuamua kuweka nguvu pamoja kujenga madarasa 4 kabla ya mwisho wa mwaka.
Amesema atarejea kwenye uzinduzi wa madarasa hayo mwezi Januari.
Katika
kijiji cha Kiga kata ya Rulanda Profesa Tibaijuka alipokelewa na
Mwenyekiti wa Kijiji Ndugu Masud Ibrahim. Aliandamana na wanawake vijana
na watoto ambao katika mda mfupi walijitokeza kwa wingi kumlaki mara
baada ya kusikia ujio wake, kuteka maji katika chemchem pekee ya
Nyakashengya inayotegemewa na kijiji hicho. Profesa aliteka dumu la maji
kwa bibi kizee mmoja mama Mwajabu ambaye hajiwezi tena.
Kwa mila na
desturi mwanamke huwezi kwenda mtoni ukarejea nyumbani bila maji
kuwasaidia wasiojiweza! Hiyo ni kupoteza wakati? Profesa Anna
alishuhudia uharibifu mkubwa wa chanzo hicho na ufugaji holela wa mifugo
inayotoka vijiji jirani ikiwa mali ya wafugaji wakubwa.
Aidha
Mwenyekiti na wanawake walimuonyesha kwa uchungu mashamba yao ya mihogo
yaliyoharibiwa kabisa na makundi ya ng'ombe hao. Kijiji hicho zamani
kilikuwa kinazalisha mihogo kwa biashara lakini sasa hawana hata ya kula
wao wenyewe kwa sababu ya uharibifu wa mifugo.
Profesa Tibaijuka
aliahidi kuleta mainjinia kuboresha chanzo cha maji na kutenga sehemu ya
kuteka maji, kunywesha mifugo na kufua nguo. Kwa kuwa tayari kijiji
kina mpango wa matumizi bora ya ardhi alitoa Shs laki tano kwa vijana
kuunda kikosi cha ulinzi wa mashamba. Wanawake walidai wanaogopa kwenda
kulima kwa sababu wanafukuzwa na kupigwa na wachungaji hao.
Waziri
Tibaijuka aliagiza kuwa mifugo yote itakayokutwa katika mashamba
ikamatwe na kupelekwa kwa Mkuu wa Wilaya kwa sababu wananchi walidai
hawana imani na polisi.
Akipita ndani ya kijiji alitembelea
yatima 2 waliomaliza darasa la saba na kujitolea kuwalipia karo
wakifaulu kwenda sekondari. Aidha alitoa mchango wa kujenga darasa moja
la sekondari ya Rulanda, kuezeka madarasa mawili shule ya msingi ya
kijiji jirani cha Nyabule ambayo imekwama mda mrefu.
Alitoa mchango wa
laki mbili na nusu kwa vikundi 4 vya wanawake ili waboreshe mtaji wao.
Katika mkutano wa hadhara uliotawaliwa na ngoma hoihoi na vifijo
kumpokea mbunge wao, Profesa Anna aliwaasa vijana kuwa na nidhamu na
kutodanganywa na wapiga porojo na kejeli bila matendo yoyote.
Alisema
vijana watambue kuwa tofauti za itikadi hazitakiwi kuleta uhasama na
vurugu. Akawaeleza kuwa watambue kuwa nguvu na jeuri ya ngumi inatokana
na utofauti wa vidole! Je kama vyote vingelikuwa saizi moja ngumi
ingekuwa na nguvu gani? Kwa mantiki hiyo kila mmoja wetu ana mchango
mkubwa katika kuleta maendeleo awe mke awe mume, awe CCM au Chadema au
CUF.
Cha msingi ni kauli na hoja zake. Aliwaambia vijana wapime akili ya
mtu kwa kauli na kazi zake. Mtu asiye na heshima hawezi kuleta
maendeleo yoyote. Na Kiongozi anayesubiri utawala kwanza ndiyo
ashughulikie matatizo ya wananchi ana faida gani?
Alisema vijana
wasiyumbishwe wachambue mambo na waone nani wa kuwaongoza. CCM ina
mengi ya kurekebisha lakini pia imefanya mengi. Umati ulimshangaa kwa
busara na uelewa wake wa mambo na kumsikiliza kwa makini. Kero ya
wanyama waharibifu wa mazao nyani tumbili na viboko alisema atazitafutia
ufumbuzi haraka iwezekanavyo. Sherehe ilimalizika kwa chakula cha
pamoja.
Awali Katika kata ya Gwanseli Profesa Tibaijuka
alisali misa ya jumapili katika Kanisa la Kilutheri KKKT la ilemera
ambapo Alitembelea shule ya ufundi yenye uwezo wa kuwafundisha wanafunzi
22 kwa mwaka vijana 10 wanajifunza useremala na wasichana 12 ushonaji
na elimu ya nyumbani. Wote ni yatima na wanafadhiliwa na Swedeni.
Profesa Tibaijuka alichanga lhaki mbili na nusu kuwasaidia. Aidha
alitembelea dispensari ya Ilemera na kushuhudia wagonjwa kupungua baada
ya mlipuko wa malaria wilayani muleba kuthibitiwa.
No comments:
Post a Comment