Katika mkutano wa Kumi wa Bunge la Kumi
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Spika wa Bunge ndugu Anna Makinda
alitangaza mabadiliko kadhaa ya muundo wa Bunge katika Kamati mbalimbali za
Bunge. Moja ya maamuzi ya Spika yalikuwa ni kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Mashirika ya Umma ambayo inajulikana kifupi kama POAC. Maamuzi haya
yameleta sintofahamu kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala ya Bunge
na Uwajibikaji katika nchi yetu. Ni muhimu tufahamu uundwaji wa POAC
ulitokana na misingi gani na kwamba Uamuzi wa Spika unarudisha nyuma
maendeleo makubwa ya kujenga Bunge imara na lenye meno. Maamuzi ya Spika ni
kinyume cha kanuni za Bunge, sheria ya Ukaguzi na Katiba ya nchi. Maamuzi ya
Spika yanavuruga Bunge,ni ya hovyo na yanapaswa kupingwa na kila mdau wa
Uwajibikaji nchini.
Baada ya Tanzania kuingia kwenye zoezi la
Ubinafsishaji, mashirika mengi ya Umma yaliuzwa na mengine kufa kabisa.
Wakati huo kulikuwa na chombo kinaitwa SCOPO (Standing Committee on
Parastatal Organisations) kwa madhumuni ya kusimamia uendeshaji wa Mashirika
ya Umma. Bunge lilikuwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na kamati
hiyo ilifutwa mwaka 1997 kufuatia hatua za ubanifsishaji na ukweli kwamba
Mashirika ya Umma hayatakuwapo na hivyo hapakuwa na haja ya kuwapo kwa kamati
hiyo. Mwenyekiti wa mwisho wa Kamati hiyo alikuwa ni Mzee William Shellukindo
wakati huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Mwaka 2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali alifanya mkutano wa Uwajibikaji na kueleza Taifa kuwa
kimsingi Mashirika ya Umma bado yapo na mahesabu yao, kwa kuwa hayaangaliwi,
ni mabaya sana nafedha za umma zinapotea. Pia alieleza kuwa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ibara ya 143(5) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kutoa taarifa za Ukaguzi za Mashirika ya Umma (Public
Authorities and Other Bodies). Hivyo aliomba Bunge liunde Kamati ya Bunge ya
Mashirika ya Umma ili liweze kupokea, kujadili na kutoa maelekezo kuhusu
mahesabu ya Mashirika ya Umma na kusimamia ufanisi wa Mashirika ya Umma. Vile
vile alishauri Kamati hiyo isimamie sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika
ya Umma. Spika wa Bunge wa wakati huo, kupitia Kamati aliyoiunda chini ya Job
Ndugai (wajumbe wengine walikuwa dkt Willibrod Slaa, Beatrice Shelukindo,
Hamad Rashid Mohammed na Nimrod Mkono) wakaunda Kamati ya Bunge ya Mashirika
ya Umma kwa mujibu wa Kanuni za Bunge za Mwaka 2007. Kamati ya POAC iliundwa
rasmi mwaka 2008 mwezi Februari. Nilipewa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa
kwanza wa Kamati hii. Sababu za kuanzishwa kwa kamati ya POAC bado zipo na
kimsingi sababu hizo ni za maana sana sasa kuliko ilivyokuwa kabla.
Majukumu ya POAC yaliainishwa na sehemu
ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007, kanuni ya
115 (13)(a-e). Majukumu hayo ni pamoja na kushughulikia mahesabu
yaliyokaguliwa ya Mashirika ya Umma, kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya
ya fedha za Umma, kutathmini ufanisi wa Mashirika ya Umma na kufuatilia
utekelezwaji wa sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya Umma. Kuanzia mwaka
2008 Mdhibiti na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa
taarifa za mahesabu ya mashirika kama Katiba ya nchi inavyomtaka na sheria ya
ukaguzi ya mwaka 2008. Sheria hii imeitaja kamati ya POAC kama moja ya kamati
zenye majukumu ya kuwasilisha Bungeni taarifa ya mwaka ya mahesabu ya
Mashirika ya Umma.
Katika kipindi cha miaka mitano POAC
imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa umahiri na kwa kweli kwa uwazi sana
kuliko kamati nyingine zote za Bunge. Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge
iliyowasilishwa katika mkutano wa saba wa Bunge, mwezi Aprili mwaka 2012
ulipelekea kutolewa kwa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo
ilisababisha mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri. Hatua hii ilikuwa ni
hatua muhimu sana katika kuweka mizizi ya utamaduni wa uwajibikaji nchini
kwetu. Wakati Kamati inajiandaa na Taarifa yake ya Mwaka 2012 kwenye Mkutano
wa Kumi na Moja, Spika ameivunja. Ikumbukwe maagizo ya mwisho ya Kamati ya
POAC yalikuwa ni kuzuia mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa mikopo kwa Serikali
bila ya kuwapo kwa mikataba. Hivi sasa Serikali imekopa zaidi ya shilingi 1.2
trilioni kutoka mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya miradi mbalimbali,
mikopo hiyo ya fedha za wafanyakazi haina mikataba yeyote na POAC iliona
hatari ya fedha za wafanyakazi kupotea na kuleta madhara makubwa kwa wastaafu
nchini.
Katika maelezo yake Spika amesema nchi
nyingine duniani hazina kamati kama ya POAC. Nadhani waliomshauri Spika
waliamua kumdanganya na yeye akadanganyika. Nchi zote za Afrika Mashariki
zina Kamati ya kusimamia Mashirika ya Umma. Kenya inaitwa Public Investments
Committee, Uganda inaitwa State Corporations Committee na hata nchi nyingine
kama India ambazo zinafuata utamaduni wa kibunge kama wetu wanayo na wanaita
Public undertakings Committee. Nchini Afrika Kusini sio tu kuna Kamati ya
Mashirika ya Umma bali pia kuna Wizara inayosimamia Mashirika ya Umma
(Ministry of Public Entreprises). Kimsingi Kamati ya POAC ilipaswa kuongezewa
nguvu zaidi ili kufikia uwezekaji wa Serikali kwenye makampuni binafsi badala
ya kuifuta. Uwezekaji wa Serikali kwenye makampuni kama BP, AirTel, Kilombero
Sugar, SonGas nk hauna uangalizi wowote.
Uamuzi wa Spika wa Bunge kuifuta Kamati
ya POAC ni uamuzi unaorudisha nyuma juhudi za nchi kujenga asasi za
uwajibikaji, ni kinyume cha sheria ya ukaguzi wa umma inayotaja Kamati tatu
za Bunge za kusimamia fedha za Umma na ni kinyume cha Katiba ya nchi. Spika
wa Bunge anasema kazi za Kamati ya POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania
ina jumla ya Mashirika ya Umma 258 yenye thamani ya shilingi trilioni 10.2
mpaka mwezi Juni mwaka 2012, hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi
kushughulikia Mashirika yote ya Umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje
kusimamia Wizara za Serikali, Mikoa na wakala za Serikali na wakati huo huo
Mashirika ya Umma 258? Kwa vyovyote vile Taifa linarudi miaka ya kabla ya 2008
ambapo Mashirika ya Umma yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za Umma. Hivi
karibuni Kamati ya POAC iligundua mtindo wa Wizara za Serikali kupeleka fedha
Serikali kwenye Mashirika na kutumia kifisadi ili kukwepa ukaguzi kwenye
Wizara (Wizara ya Utalii ilipeleka zaidi ya shilingi 600 milioni Bodi ya
Utalii mwaka 2010/2011). Ikumbukwe pia wizi wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji
holela wa baadhi ya mali za Serikali kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati
ambazo Bunge halina kamati inayosimamia Mashirika ya Umma.
Kwa vyovyote vile Spika wa Bunge
amedhihirisha namna ambavyo anafanya maamuzi bila kuzingatia maslahi ya nchi
wala kuzingatia historia ya uwajibikaji katika nchi. Namna mijadala ya Bunge
inavyoendeshwa, namna anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge
kibogoyo na namna anavyofanya maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za
kuokoa misingi ya uwajibikaji wa nchi. Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe
kwa kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue
kwamba Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza
la wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi
yetu itaumia.
By Zitto Kabwe.
No comments:
Post a Comment