WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekutana na Balozi
wa Brazili nchini Tanzania, Bw. Fransisco Luz na kujadiliana mambo kadhaa
kuhusu maendeleo na mahusiano baina ya nchi hizo mbili.
Akizungumza na Balozi Luz ofisini Magogoni
jijini Dar es Salaam leo mchana (Jumatano, Aprili 29, 2015), Waziri Mkuu alimshukuru
Balozi huyo kwa ushirikiano ambao ameutoa kwa Serikali ya Tanzania katika
kipindi cha miaka sita ambacho amekuwa akiiwakilisha nchi yake hapa nchini.
Balozi Luz ambaye amepangiwa kwenda Jordan kwenye
kituo kipya, alisema anaondoka nchini akiamini kwamba mtu atakayekuja kumpokea
ataendelea mambo aliyoyaanzisha ikiwemo mradi wa kufadhili utafiti na
uendelezaji wa zao la pamba kwenye kituo cha utafiti wa kilimo cha Ukiriguru, Mwanza.
Balozi Luz ambaye alifika kumuaga Waziri Mkuu,
alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu kwamba ubalozi huo umefanikiwa
kupeleka Watanzania wawili kusomea kozi za Uzamili (Masters’ Programme) kwenye vyuo
vikuu vya Brazil.
“Wanafunzi hawa wawili waliondoka Februari mwaka
huu, ni kati ya wanafunzi saba waliofuzu lakini wengine watano walikosa
ufadhili kutoka kwenye taasisi zao. Mmoja anasomea Geo-Physics na mwingine Oil
Engineering,” alisema Balozi Luz.
Balozi Luz ambaye anatarajia kuondoka nchini
mapema mwezi ujao, amepangiwa kituo kingine ambapo ataenda kuiwakilisha nchi
yake nchini Jordan.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
No comments:
Post a Comment