NA AUDAX MUTIGANZI, BUKOBA +255 784 935 586
Uwekezaji katika nchi
hii ni sera iliyotiliwa mkazo na rais wa jamhuri ya muungani wa Tanzania wa
awamu ya tatu, Benjamini William Mkapa, sera hii imechangia kuchochea kasi ya
maendeleo kwa kuleta mabadiliko katika nyanja za kijamii na kiuchumi.
Ninachotaka kusema sera
ya uwekezaji imechangia kuboresha na kuimarisha huduma katika Nyanja mbalimbali
ndani ya jamii, imeongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani,
imekuza sekta ya utalii, imeboresha
masuala ya kilimo mambo ambayo yanachangia ukuaji wa pato la taifa.
Ni lazima tukubali kwamba sera hii imechangia kwa kiasi
kikubwa kupunguza ukosefu wa ajira hasa kwa wanaohitimu masomo yao katika ngazi
mbalimbali hapa nchini walikokuwa wakitegemea sana ajira zinazotolewa na
serikali ambazo ni chache ukilinganisha
na idadi ya wanafunzi wanaohitimu masomo yao katika vyuo vya elimu ya juu na elimu ya kati.
Kwa maana hiyo hatuna
budi kumpongeza rais mstaafu wa awamu ya tatu, kwa kutilia mkazo
suala la uwekezaji, katika kutilia mkazo suala la uwekezaji aliweka mazingira mazuri ambayo hadi sasa yanaendelea kuwavutia wale
wanaojitokeza kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali.
Ndugu zangu Watanzania
ni lazima tukubali kwamba mchango wa Rais Mstaafu Mkapa katika kuendeleza
nchi hii ni mkubwa, sera ya uwekezaji imechangia kwa kiasi
kikubwa matumizi ya rasilimali zilizo adimu zinazopatikana hapa nchini ambazo ni pamoja na malighafi zinazotumiwa na
viwanda vya wawekezaji vilivyoko hapa nchini vinavyozalisha bidhaa mbalimbali.
Ni kweli sera hii ni nzuri imechangia kuchochea kasi ya
maendeleo, katika utafiti wangu nilichokigundua ni kwamba wawekezaji walio wengi wanaojitokeza kuwekeza hapa
nchini ni wale wanaotoka nje ya nchi.
Kwa uelewa nilikuwa nao ni wawekezaji wachache toka nje ya
nchi ambao wanaweza kuwa na machungu ya nchi hii katika kuhakikisha inapiga hatua kubwa kimaendeleo.
Ninachokielewa kila
mwekezaji anayejitiokeza kuwekeza hapa nchini lengo lake kubwa ni kuchuma mali
na kuondoka bila kutangulizambele maslahi ya nchi, hakuna mwekezaji ambaye
anaweza kuwa na machungu ya nchi hii bila kutanguliza maslahi yake binafsi kwa
kuwa anawekeza kwa lengo la kupanua myaji wake ndio maana wawekezaji
wanajitokeza wanakuja kibiashara zaidi.
Je, sisi Watanzania wenye uwezo tulioko ndani na nje ya nchi
tuko wapi? Ni lazima tujiulize swali hilo kwa kuwa ni la ufahamu,
kinachonishangaza na kuniuma ni pale ninapowaona baadhi ya Watanzania wenye
mitaji mikubwa wakosa moyo wa uzalendo
hasa pale wanapofikia katika mataifa mengine.
Kuna usemi ‘usemao samaki mmoja akioza sio kwamba wote
wameoza’ usemi huu nitakubaliana nao sio
kwamba watanzania wote waishio nje ya nchi wenye mitaji mikubwa wanaokosa moyo
wa uzalendo, kuna baadhi ya Watanzania
wanaokumbuka walikotoka kwa kutenga
mitaji walionayo kwa kuwekeza hapa nchini.
Miongoni mwa Watanzania waliotenga sehemu ya mitaji waliyo
na hatimaye kuwekeza nchini ni pamoja na Paskazia Barongo Mtanzania aishiye
nchini Sweeden ambaye amejitokeza na kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuanzisha
chuo cha ualimu kinachojulikana kwa jina la ERA kilichoko katika mtaa wa Kagemu
ulioko katika kata ya Kitendagulo, mkoani Kagera.
Chuo hicho kinatoa mafunzo ya ualimu daraja la tatu ngazi ya
cheti, Bi Balongo anasema kwamba chuo
hicho kimeanza rasmi kutoa mafunzo ya ualimu kuanzia mwaka jana mwezi wa nane,
anaeleza kwamba alifikiria mpango wa
kuanzisha chuo hicho mwaka 2008 baada ya
kupona katika ajali mbaya sana ya gari aliyoipata akiwa nchini Sweeden.
Anaeleza kwamba baada ya kupona katika ajali hiyo alijisikia
kwamba ana deni kubwa kwa watanzania hususani wazaliwa wa mkoa wa Kagera hasa
waliomuombea hadi akafikia hatua ya kupona, anasema kuwa katika ajali alivunjika
vunjika sehemu mbalimbali za viungo vya mwili wake.
Bi. Barongo anasema katika kuwaenzi Watanzania walimuombea
hadi akapona baada ya ajali hiyo alilazimika kuwekeza katika sekta ya elimu na
sekta ya afya, anasema amelazimika kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuwa
inamchango mkubwa katika ustawi ndani ya jamii.
Anasema kuwa anachokiamini ni kwamba kama waliompatia matibabu hadi
akapona wasingekuwa na elimu
wasingefanya chochote kulingana na hali mbaya aliyokuwa nayo baada ya kupata
ajali hiyo, anaendelea kusema kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha pamoja na
kukabiliwa na changamoto nyingi.
Anabainisha kwamba hakulazimika kuwekeza katika sekta ya
elimu kwa lengo la kufanya biashara bali amewekeza katika sekta hiyo kwa lengo
la kutoa huduma, katika kutoa huduma anasema kwamba chuo chake kinampokea
mwanafunzi yoyote aliyemaliza kidato cha nne bila kujali ufaulu wake.
Bi. Balongo anasema wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne
wenye ufaulu mzuri wanajiunga moja kwa
moja na mafunzo ya cheti cha ualimu
ngazi ya daraja la tatu na wale wanaojiunga na chuo hicho wenye ufaulu
usioridhisha wanapatiwa elimu maalumu ya kuwawezesha kurudia mitihani yao
inayowapa sifa ya kufanya mitihani ya cheti cha ualimu.
Anaendelea kusema kuwa chuo chake kinatoa elimu ya kiwango
cha juu ambayo inaenda sambamba na vyuo vya ualimu vinavyomilikiwa na serikali,
anasema kuwa ataendelea kukiboresha chuo hicho , anasema kuanzia mwaka kesho
chuo hicho kitaanza kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya kilimo.
Bi. Barongo anasema
chuo kimelazimika kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya kilimo kwa lengo
la kuwawezesha vijana waweze kujiari wenyewe na ili waachane na dhana ya kutegemea ajira
chache zinazotolewa na serikali.
Amesema mafunzo
yatakayotolewa kwa vijana yatawawezesha kujifunza mbinu bora za kilimo,
anabainisha kuwa kilimo kinalipa vizuri ukilinganisha na shughuli nyingine za
uzalishaji mali zinazohitaji mitaji mikubwa.
“ Nina mpango mkubwa wenye lengo la kuboresha maisha ya
vijana, mimi sikuwekeza kwa leng la kupata faida nimewekeza katika sekta ya
elimu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na ndio maana najitolea katika
mambo mengi, mimi ni tofauti na wawekezaji wengine wanaotafuta faida” anasema.
Bi.Barongo anasena chuo chake cha ERA kina eneo kubwa ambalo
litawawezesha wanafunzi watakaojitokeza kusoma masuala ya kilimo kujifunza kwa
vitendo badala ya kupata mafunzo ya masuala ya kilimo kwa njia ya vitabu.
Anasema chuo kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 129 na
matarajio ya chuo hicho ni kupokea
wanafunzi 500 kwa wakati mmoja pindi miundo mbinu itakapokamilika, akielezea
miundo mbinu ya chuo anasema kwa sasa chuo hicho kina jumla ya mabweni mawili
ya wasichana na moja la wavulana.
Akielezea miundo mbinu mingine katika chuo hicho anasema
kina madarasa matatu , chumba cha walimu, maktaba dogo, chumba cha komputa,
ofisi ya walimu, ofisi ya mkurugenzi na ofisi ya makamu mkuu wa shule na jiko
la kisasa, anaongeza kuwa chuo hicho kwa sasa kinatoa ajira kwa watu 26.
Katika kueleza changamoto mbalimbali zinazokikabili utendaji
wa kazi wa chuo hicho Bi.Barongo anasema utaratibu wa serikali kubadili mifumo
yake mara kwa mara kwamba inaathiri kiwango cha elimu.
Akitoa ufafanuzi wa changamoto hiyo anaeleza kwamba chuo hicho kwa mara ya kwanza
kilisajiliwa na wizara ya elimu, anasema kwa sasa vyuo vyote binafsi vinatakiwa
kusajiliwa NACTE, anaendelea kusema kuwa
ubadilishwaji wa mfumo wa usajili wa vyuo kwamba unavigharimu na unawavunja
moyo wawekezaji katika sekta ya elimu.
Ameishauri serikali
kuboresha zaidi manzingira ya uwekezaji
katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha inazishawishi taasisi za kifedha kutoa
mikopo kwa wawezekazi katika sekta ya elimu yenye riba na masharti nafuu,
tofauti riba inayotozwa kwa wawekezaji katika sekta nyingine zinazojihusisha na
masuala ya biashara ya moja kwa moja.
Pia ameishauri serikali kuondoa ukilitimba katika zoezi la
usajili wa mashule na vyuo vya elimu kwa
kuwapa madiwani wa manispaa, majiji na halmashauri za wilaya madaraka makubwa
ya kutoa vibali vya uanzishwaji wa mashule na vyuo.
Bi.Barongo anasema kwa kiasi Fulani mgogoro katika manispaa
ya Bukoba ambao ulipelekea kutofanyika kwa vikao vya baraza la madiwani kwamba ulimuathiri sana kwa kuwa
ulimchelewesha upatikanaji wa kibali cha kuanzisha chuo hicho hali
iliyomgharimu sana kwa kuwa alikuwa analazimika kuja nchini mara kwa mara
kufuatilia usajili.
Anamalizia kwa kuwapongeza wale wote waliomtia moyo hadi
akatimiza adhima yake ya ya kuanzisha chuo cha ualimu, pia amewahimiza
Watanzania kukumbuka walikotoka kwa
kutenga mitaji waliyonayo na kuwekeza hapa nchini kwa kuwa Watanzania ndio
wenye uchungu na nchi yao.
No comments:
Post a Comment