“Inapofikia wasimamizi wa Kanuni za Chama wanapigwa vita ya
wazi kwa uamuzi wao wa kukisimamia Chama, tafsir yake ni moja tu watu
wanaowapiga vita hawakitakii mema chama chetu.”
“..Chama Cha Siasa
chochote duniani hubomoka kutokana na
migongano iliyokithiri ya muda mrefu. Uzoefu wa vyama vikubwa vilivyoporomoka
umeonyesha hivyo! Chama lazima kidhibiti
uchu wa madaraka wa baadhi ya viongozi wake na ndani ya serikali yake...” –
Dr Eginald P. Mihanjo
“..Chama cha siasa ni
itikadi. Chama cha siasa ni siasa kwa maana halisi ya neno lenyewe siasa –“siasa”.
Ni mahali ambapo watu wenye madhumuni mamoja yaliyoainishwa waziwazi hukutana
na kuwa kitu kimoja. Chama cha siasa sio
mkusanyiko wa “majini dume yenye tamaa”, - majini ambayo yametanguliza mbele
tamaa kufa na kupona-tamaa ya kutengeneza pesa au kupata vyeo kwa gharama yoyote! – Dr Bashir Ally
UTANGULIZI:
Hili ni tamko la vijana makini wa jumuiya ya umoja wa vijana
wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuunga mkono juhudi na utendaji wa sekretarieti
ya halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi ikiongozwa na Katibu Mkuu Komredi
Abdulrahaman Kinana.
Maneno ya utangulizi yamebeba dhima ya tamko hili, kufuatia
taarifa zilizoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari vikiwanukuu baadhi ya
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi,wakiwatuhumu Viongozi wa
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahaman Kinana
na Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndugu
Nape Moses Nnauye.
Sisi Vijana tunatambua kuwa tuhuma hizo na maneno hayo ya
hovyo yametolewa kwa nia ovu yenye kulenga kuwakatisha tamaa Viongozi hao wa
Chama. Tunafahamu kuwa upo mkakati wa kiuhaini ulioandaliwa na kuratibiwa na “mtandao”
ndani ya Chama ambao umejipanga kuendesha uhaini huo.
Sisi vijana wa UVCCM tunatambua na kuthamini juhudi za
Katibu Mkuu na Sekretarieti yake katika kukijenga na kukiimarisha Chama kwa kuisimamia
barabara misingi na shabaha ya kuundwa kwake, katika umri wetu hatukuwahi kuona
Chama kikiwa karibu na wananchi kwa kufuatilia, kusikiliza na kushiriki katika
utatuzi wa kero, shida na changamoto zao kama ilivyo katika kipindi hiki chini
ya Comrade Kinana na timu yake. Juhudi hizi ni za kuungwa mkono na kamwe si za
kubezwa na mwanaCCM muadilifu, muaminifu na mwenye mapenzi ya kweli kwa Chama.
Juhudi za kukiimarisha Chama kutoka ngazi za chini, kwa
mabalozi ni mkakati bora kuwahi kutekelezwa na Chama, kukirudisha Chama kwa
wanachama ni kutimiza lengo la kuundwa kwa Chama hiki, Chama hiki ni cha
wanyonge, masikini wa Taifa hili, HAIWEZEKANI matajiri watake kukihodhi na
waratibu mikakati ya kukihujumu kwa pesa zao hali sisi vijana tukitazama,
tunasema tutakilinda Chama chetu na tutawalinda viongozi wetu waadilifu.
Ni hawa ambao wanabezwa leo ndio wameweza kurudisha Imani ya
wananchi kwa Chama, Imani na matumaini ambayo tayari yalishaanza kupotea na
Chama kuonekana si tena cha wanyonge, wakulima na wafanyakazi wa nchi hii.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio waliozunguka kwenda
kukutana na wakulima wa Pamba kule mikoa ya Kanda ya ziwa na kumpeleka balozi
wa China na kumshawishi kujenga viwanda ili kuboresha manufaa kwa wakulima.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio waliokwenda Kusini
kukutana na wakulima wa Korosho na kushirikiana nao pamoja na bodi kutatua
tatizo la Korosho.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio walioibua hoja na kero
za wafugaji, walimu na wananchi kwa ujumla, na kuwataka viongozi wa Serikali
kuhakikisha wanawajibika kwa wananchi walipa kodi wa Taifa hili.
Kupinga mafanikio ya Ziara hizo ni kupinga utetezi wa
wanyonge.
Mtu anayebeza ziara hizo na kuwaita Viongozi waliozifanya
waropokaji na wahuni wahuni ni mtu mjinga, mtu wa hovyo,hana maadili,
asiyekipenda Chama, mhaini na mzandiki anayepaswa kuchukuliwa hatua kali za
kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine.
TAMKO hili limezingatia wosia wa Baba wa Taifa, muasisi wa
Chama Cha Mapinduzi Mwl Julius Kambarage Nyerere katika kitabu Chake TUJISAHIHISHE.
Imetolewa na Paul Makonda.
Katibu wa Hamasa na Chipukizi.
No comments:
Post a Comment