Mwenyekiti wa taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt Shukuru Kawambwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya WAMA Nakayama Dkt Ramadhani Dau na Mkuu wa Shule hiyo wakipokea moja ya Tabuleti 61 alizozitoa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Wama Nakayama iliyoko kijijini Nyamisati, Rufiji, Mkoa wa Pwani leo Januari 27, 2014 toka kwa Mwenyekiti wa taasisi ya kusaidia elimu ya Opportunity Education Foundation wa Marekani Bw. Joe Ricketts akikabidhi moja ya Tabuleti 61 alizozitoa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili katika Shule hiyo.
Serikali
kusambaza tabuleti za kufundishia sekondari
Yaanza kazi hiyo kwa
kushirikiana na taasisi ya Marekani ya Opportunity Education Trust
Serikali inakusudia kutoa maelfu kwa
maelfu ya tabuleti za kufundishia masomo mbali mbali kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari
nchini kama njia ya ubunifu zaidi, ya kisayansi na ya uhakika ya kukabiliana na
changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(ICT).
Ili kufanikisha mpango huo, Serikali
inakusudia kuingia ushirikiano (partnership)
na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Opportunity Education Trust ya Marekani
ambayo leo, Jumatatu, Januari 27, 2014, inazindua mpango wa majaribio wa utoaji
wa tabuleti hizo kwa wanafunzi na walimu wao wa shule za sekondari nchini.
Mpango wa Serikali wa kusambaza tabuleti
kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari ulitangazwa usiku wa jana,
Jumapili, Januari 26, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokutana na kuzungumza na Bwana Joe
Ricketts, mwenye taasisi ya Opportunity Education Trust na mmoja wa matajiri wa
Marekani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika
Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemweleza kwa undani Bwana Ricketts hatua
ambazo zimechukuliwa na Serikali yake kupania na kuboresha elimu tokea mwaka
2006, hatua ambazo zimechangia kupanua kwa kasi na kwa kiwango kikubwa wigo wa utoaji
elimu nchini na changamoto ambazo zimezuka kutokana na upanuzi huo mkubwa.
Rais Kikwete amesema baadhi ya
changamoto hizi ni ukosefu wa walimu, na hasa walimu wa masomo ya sayansi, na
ukosefu wa vitabu vya kufundishia changamoto mbili kubwa ambazo zinatatuliwa na
matumizi ya tabuleti.
“Mbali na upanuzi mkubwa wa
nafasi za wanafunzi kupata elimu ya ngazi mbali mbali, pia tumepanua sana
ufundishaji wa walimu. Mwaka 2005, vyuo vyetu vyote vilikuwa vinatoa walimu 500
sasa tunatoa walimu 12,000 kwa mwaka. Hivyo, tunaamini kuwa katika mwaka mmoja
ama miwili ijayo, tutakuwa tumemaliza tatizo la walimu wa masomo ya sanaa,”
Rais Kikwete alimwambia Ricketts na kuongeza:
“Lakini bado tunakabiliwa na
upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi, kama zilivyo nchi nyingine. Tuna upungufu
wa walimu 26,000 na kwa mwaka vyuo vyetu vyote vinahitimisha walimu 2,100 tu.
Hii ina maana kuwa itabidi kusubiri miaka 13 kuweza kumaliza tatizo hili kwa
mahitaji ya sasa. Hili haliwezekani na hii ndiyo maana halisi ya kutumia
sayansi na teknolojia ya namna hii kufundishia wanafunzi wetu.”
Rais Kikwete alisema kuwa matumizi ya
teknolojia kufundishia nchini ni jambo linalowezekana kwa urahisi kwa sababu mtandao
wa mawasiliano wa National Fibre Network
ambao karibu umefikia kila wilaya sasa.
Rais Kikwete alimshukuru Bwana Ricketts
na taasisi yake kwa kukubali kuchangia
maendeleo ya sekta ya elimu nchini kwa kusambaza teknolojia ya kisasa kama moja
ya njia za ubunifu zaidi za kufundishia hasa masomo ya sayansi.
Chini ya mpango huo wa majaribio wa
kusambaza teknolojia hiyo ya kisasa, taasisi ya Opportunity Education Trust inatoa tabuleti 1100 kwa ajili ya
walimu na wanafunzi wa sekondari katika shule 33.
Bwana Ricketts ambaye ni mwenyeji wa Omaha,
Nebraska alimwambia Rais Kikwete: “Hapa tunafanya majaribio na Tanzania ni
nchi ya kwanza duniani miongoni mwa nchi ambazo tunaunga mkono mipango ya
maendeleo kunufaika na mpango huo wa majaribio. Ni azma yetu kuwa baada ya kuwa
tumefanya tathmini ya mafanikio na changamoto za hatua hii ya majaribio,
tutaupanua mpango huu kushirikisha shule nyingi zaidi kwa kushirikiana na
Serikali kwenye mpango wake mkubwa wa kusambaza teknolojia hii katika shule
zote za sekondari hapa Tanzania.”
Bwana Ricketts na wataalam wake pamoja
na maofisa wa Serikali wameanza kutekeleza mpango huo leo, Jumatatu, Januari
27, 2014, kwa kutoa tabuleti kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wama
Nakayama iliyoko Mkoa wa Pwani.
Baada ya leo, shughuli hiyo itahamia
Zanzibar na Pemba, kabla ya Bwana Ricketts na wataalam wake kutoa tabuleti kwa
shule zilizoko mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kagera na
Morogoro.
Shule zinazonufaika katika mpango huo
ni za Serikali na binafsi na kwa kuanzia masomo ambayo yanapatikana katika
tabuleti hizo ni hesabu, jiografia, historia na kiingereza.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment