Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya Pamoja na Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria Youcef Yousif pamoja na ujumbe wake, pamoja na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania Profesa Sospter Muhongo Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mhe Steven Masele na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhe E. maswi ugemi huo ulipomtembelea Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria Mhe. Youcef Yousif aliyemtembelea Ikulu Dar es salaam.
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Januari 7, 2014, amekutana na
kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria Mheshimiwa
Youcef Yousfi ambaye yuko katika ziara ya siku sita nchini.
Katika ziara hii, Mheshimiwa Yousfi na
ujumbe wake unaojumuisha viongozi wa mashirika ya umma, wanatarajia kutembelea
kituo cha umeme cha Gridi ya Taifa cha Ubungo mjini Dar es Salaam, ujenzi wa
bomba la gesi katika eneo la Vikindu na Mkuranga mkoani Pwani, machimbo ya
Mererani na Minjingu mkoani Manyara.
Rais Kikwete ameeleza kufurahishwa kwake
na ziara hiyo, akisisitiza kwamba Tanzania na Algeria zimekuwa marafiki na
washirikia wa karibu wa siku nyingi katika masuala ya siasa na uchumi, kufuatia
misingi imara iliyowekwa na waasisi wa nchi hizo - Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Mheshimiwa Ahmed Ben Bella,
Rais amebainisha kwamba ushirikiano wa
nchi hizi mbili ni muhimu sana sio tu katika kuendeleza uhusiano wao wa
muda mrefu, bali pia katika uwekezaji na utafutaji na uchimbaji wa
mafuta na gesi pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu.
Alisema Rais: "Tunahitaji washirika wazoefu, waaminifu na wenye ujuzi katika
sekta ya mafuta na gesi kama Algeria katika kuendeleza sekta hiyo ambayo ni
mpya kwetu”.
Alitolea mfano wa uzoefu wa miaka mingi
wa Algeria katika uchimbaji na usafirishaji wa gesi asilia katika mradi wa
bomba la gesi la Maghreb–Europe, unaounganisha machimbo ya gesi ya
Hassi R'Mel nchini Algeria, na kusafirisha gesi asilia hadi nchi za Morocco,
Hispania na Ureno
"Tanzania itanufaika sana na juzi na uzoefu wa
Algeria katika sekta ya gesi hasa katika wakati huu ambapo Shirika la Taifa la Maendeleo
ya Petroli (TPDC) limepewa jukumu la kujiendesha kibiashara hivyo linahitaji
washirika mahiri", alisema Rais
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR
ES SALAAM
No comments:
Post a Comment