Monday, January 13, 2014

Papa akemea vikali uavyaji mimba

 
Hii ni kauli ya kwanza kali ya Papa Francis kuhusu swala la uavyaji
Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis, amelaani vikali kitendo cha kuavya mimba akikitaja kuwa, dalili ya ‘kuogofya’ ya utamaduni wa kupotosha ambao hauthamini maisha ya binadamu.
Aliongeza kwamba, inatishia hata kutafakari kuhusu uavyaji mimba za mapema.
Tangu kuchaguliwa kwake mwezi Machi, Papa Francis, hajazungumzia kitendo cha kuavya mimba kwa ukali kama walivyofanya watangulizi wake.
Aliyatoa matamshi yake hayo katika hotuba yake ya kwanza mwaka huu kwa wajumbe katika Vatican.
‘Inatisha hata kutafakari kuwa kuna watoto waathiriwa wa kitendo cha uavyaji mimba ambao hawatawahi kuona hata siku moja,’’ alisema papa kama sehemu ya hotuba yake ambayo ilikuwa inagusia haki za watoto kote duniani.
‘‘Lakini cha kusikitisha ni kwamba kinachokuwa kimetupwa sio chakula kibaya ambacho kitakuja kuoza , ni binadamu wanaokuwa wametupwa kwa njia isiyokubalika.’’
Mwandishi wa BBC mjini Roma, Alan Johnston, anasema kwamba kumekuwa na wasiwasi katika kanisa katoliki kuwa Papa Francisa hajakuwa akikemea vikali kitendo cha kuavya mimba.
Aidha wadadisi wanasema kwamba msimamo wa Papa kuonelea bora msamaha kuliko kulaani, uliwatia wasiwasi baadhi ya viongozi wa kanisa hilo ambao wana msimamo mkali zaidi kuhusu uavyaji mimba , lakini bila shaka watakaribisha matamshi yake haya.
Miezi kadhaa iliyopita, Papa Francis alikiri kwamba hakuzungumzia pakubwa kuhusu swala la uavyaji mimba pamoja na kutumia mpango wa uzazi.
Lakini alijitetea akisema kuwa alihisi sio vizuri kuyazungumzia mambo hayo yanayozua mjadala mkali wakati wote.

No comments:

Post a Comment