*Azindua kisima cha maji, awapigia debe kwenye umeme
*Amtaka RC Dar azuie michango ya darasa la kwanza
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka
wakazi wa Dunda ‘A’ na Dunda ‘B’ wajiunge kwenye Vyama vya Kuweka na Kukopa
(SACCOS) na wavisajili kwenye Halmashauri yao ili waweze kukubalika kupatiwa
mikopo.
Alikuwa akizungumza na wakazi wa eneo
hilo jana jioni (Jumanne, Januari 28,
2014), lililopo Mtaa wa Kigogo Fresh Kata ya Pugu wilaya ya Ilala nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwenye hafla fupi ya uzunduzi wa kisima cha
maji kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo.
Waziri Mkuu aliwataka wasajili vyama
vyao ili waweze kutambulika kwa urahisi na waweze kuwa na watu wenye dhamana ya
kurejesha mikopo mara watakapoanza shughuli za ujasiriamali.
“Tatizo letu ni ukosefu wa anuani
za makazi ili wakopaji watambulike na waweze kurejesha mikopo. Tunasisitiza
SACCOS kwa sababu tunajua kutakuwa na watu wenye dhamana ya kusimamia
urejeshwaji wa mikopo hii,” alisema wakati akijibu swali la Bw. Abdallah
Mwaking’inda na wakazi wa Dunda.
Vilevile, alitumia fursa hiyo
kumwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadick afuatilie shule
ambazo zinatoza michango kwa watoto waliopaswa kuandikishwa darasa la kwanza
lakini wakashindwa kuazna shule kwa sababu ya michango hiyo.
“Uandikishwaji wa watoto wanaoanza
darasa la kwanza ni wa lazima kwa kila mtoto, tulifanya hivyo ili tuhakikishe watoto
wote wapate elimu. Sasa kama mzazi ana watoto wawili au watatu akishindwa
kuwalipia manake watoto hao wamebaki nyumbani,” alisema.
“RC litazame vizuri suala hili kwa
sababu kama zoezi la uandikishaji ni hili, ina maana kuna wazazi watashindwa
kuwapeleka watoto shule,” alisema.
Mapema, kwenye risala yao, wakazi hao wa Dunda ‘B’ walimshukuru
Waziri Mkuu kwa kuwaunganisha na mfadhili kutoka taasisi ya REHEMA ambayo
imewajengea kisima hicho chenye urefu wa mita 90, tenki la lita 10,000 na mnara
wa mita 20 wa kuwekea tenki hilo kwa gharama ya sh. milioni 20.
Walimuomba pia Waziri Mkuu
awasaidie kupata umeme wa three phase
ili uweze kutosheleza mahitaji ya eneo zima la Dunda ikiwa ni pamoja na
kuendesha kisima chao.
Akijibu haoja hiyo, Mhandisi
Theodori Bayona kutoka TANESCO makao makuu alisema watarudisha huduma ya three
phase iliyokuwepo zamani lakini ikaondolewa kwa sababu ya wizi wa mara kwa
mara. Aliwaomba wakazi hao wawe walinzi wa nyaya pindi watakapowekewa na kwamba
watatakiwa kulipia service line ya kawaida ili umeme upelekwe hadi kisimani
moja kwa moja.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck
Sadick aliwahidi kuwachangia tenki moja la lita 10,000 ili waweze kuwa na ujazo
mkubwa wa maji kwenye matenki yao na kuepusha kazi ya kupampu maji mara kwa
mara.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, wenye
magari yanayobeba maji, wanauza ndoo moja kwa sh. 400/- katika eneo hilo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.