WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wote watumie
fursa ya uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura kwa kujiandikisha ili
waweze kushiriki uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25,
mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kujiandikisha kwenye Ofisi ya
Mtendaji Kata iliyopo kijiji cha Kibaoni, wilayani Mpanda, mkoani Katavi
jana jioni (Ijumaa, Mei 25, 2015), Waziri Mkuu alisema hii ndiyo fursa
pekee ya kuwawezesha kushiriki uchaguzi mkuu ujao.
“Ninawasihi Watanzania wote tusiache kutumia fursa hii…
kila mtu ahakikishe kuwa anajiandikisha. Ni fursa pekee itakayohakikisha
kila mwananchi anashiriki uchaguzi wa kumpata Rais, Mbunge na Diwani,”
alisema.
Waziri Mkuu alisema amefarijika kwa kazi aliyoiona
ikifanyika kwani hadi sasa Halmashauri za Nsimbo na Mlele zimefanikiwa
kuandikisha watu kwa zaidi ya asilimia 100.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya uandikishaji katika
Halmashauri ya Mlele, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Godwin Benne
alisema walilenga kuandikisha watu 19,482 lakini hadi kufikia jana
walifanikiwa kuandikisha watu 20,292 sawa na asilimia 105. Uandikishaji
katika wilaya ya Mlele ulianza tarehe 18 Mei, mwaka huu.
“Mlele tuna vituo 84 katika tarafa tatu za Inyonga, Mpimbwe na Mamba. Inyonga tuna vituo 28, Mpimbwe viko 23 na Mamba viko 33.
"
Akifafanua zaidi, Bw. Benne alisema katika kata ya Kibaoni
ambayo ina vituo sita, jana peke yake walifanikiwa kuandikisha watu
1,007 kikiwemo kituo cha Kibaoni ambacho Waziri Mkuu Pinda
alijiandikisha. Alivitaja vituo vingine kuwa ni Milumba, Sungusungu,
Ilalangulu, Manga na Shule ya Msingi Kakuni ambako Mama Tunu Pinda
alijiandikisha jana hiyo hiyo.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo,
Bw. Neneka Rashid, uandikidhaji ulianza Mei 18, 2015 kwenye kata 12 na
kwamba hadi kufikia jana, kata nne zilikwishaandikisha watu 12,001 sawa
na asilimia 108.9 licha ya kuwa matarajio yao yalikuwa ni kuandikisha
watu 11,014. Alizitaja kata hizo kuwa ni Nsimbo, Kapalala, Magamba na
Uruwira.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment