KESI
ya mauaji ya Aaron Nongo mwenye ulemavu wa ngozi (albino) imeanza kusikilizwa
tena leo hii kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza baada ya kusimama kwa miezi
takriban mitano.
Shauri
hilo namba 213 la mwaka 2014 liko mbele ya Jaji Robert Makaramba, ambaye ndiyo
kwanza ameanza kulisikiliza baada ya jaji wa awali, Ashery Sumari, kupewa
uhamisho.
Washtakiwa
katika kesi hiyo walikuwa watano, lakini leo hii mahakama imearifiwa kwamba
mmoja – Paulo Budeba Genji maarufu kama Lumalija – alifariki dunia Novemba 22,
2014 katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, wakati akiwa mahabusu.
Taarifa
hiyo ilitolewa na kiongozi wa mawakili wa upande wa mashtaka, Emil Kiria,
ambaye aliiomba mahakama, akirejea Kifungu cha 284 (a) cha Sheria ya Mwenendo
wa Makosa ya Jinai, kwamba inapotokea hali kama hiyo mashtaka dhidi ya mtu huyo
yanafikia kikomo, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama.
Washtakiwa
waliobakia kwenye kesi hiyo ni Chacha Jeremia, Mathew Jeremia Mlimi, Paschal
Lugoye Mashiku na Alex Joseph maarufu kama Bugwema Silola Jangalu.
Kesi
hiyo ambayo inaendelea tena kesho katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, iko
katika hatua ya ushahidi ambapo shahidi wa sita wa upande wa mashtaka atatoa
ushahidi wake.
Leo
hii mashahidi wawili wametoa ushahidi wao na kufanya idadi ya mashahidi
waliokwishatoa ushahidi wao kufikia watano mpaka sasa.
Marehemu
Nongo aliuawa Juni 26, 2009 majira ya saa tatu usiku akiwa nyumbani kwake
Ibanda Relini, jijini Mwanza ambapo wauaji hao walimkata usoni na kisha kumkata
miguu yake yote miwili na kutoweka nayo pamoja na meno mawili ya mbele.
No comments:
Post a Comment