WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa
dini nchini waitumie mikutano yao ya mahubiri kutoa elimu juu ya athari za dawa
za kulevya kwa waumini wao na Watanzania wote kwa ujumla.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumapili, Mei 3,
2015), wakati akizungumza na viongozi na waumini wa Kanisa la Moravian Tanzania
kwenye ibada ya uzinduzi wa Jimbo la Mashariki la kanisa hilo uliofanyika makao
makuu ya jimbo hilo, Mbagala Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
“Niwaombe sasa viongozi wa dini tuungane na
Serikali kutoa elimu juu ya athari za biashara ya dawa za kulevya na matumizi
yake katika jamii. Ninawasihi viongozi wa dini tuanzie makanisani na misikitini,
na kwenye mikutano yote tunayoifanya; tusimalize mikutano yetu bila kutoa elimu
kuhusu athari za dawa za kulevya kwa waumini wetu na umma kwa ujumla,” alisema
Waziri Mkuu.
“Viongozi wa dini mna jukumu kubwa la kuwalea zaidi
vijana ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wao ndiyo
kundi kubwa zaidi miongoni mwa waumini wenu. Ninaamini tukishirikiana kutoa elimu
hii pamoja, tutaweza kuwaokoa vijana wetu ambao ndiyo waathirika zaidi,”
alisema.
Alisema jimbo hilo jipya linalojumuisha mikoa
mitano ya Dar es Salaam, Morogoro, Lindi, Mtwara na Pwani lina jumla ya wakazi 9,817,207
kwa mujibu wa Sensa ya Makazi na Watu ya mwaka 2012. Pia lina ukubwa wa
kilometa za mraba 190,646 sawa na asilimia 20.1 ya eneo lote la Tanzania.
“Kati ya wakazi hao, asilimia 56.8 ni watu
wenye umri wa kufanya kazi yaani kuanzia miaka 15-64, wengi wao wakiwa ni
vijana. Pia kuna asilimia 38.1 ambao ni watoto wenye umri chini ya miaka 15 na
waliobakia ni wazee wenye miaka 65 na zaidi sawa na asilimia 5.1,” alisema.
Aliutaka uongozi wa kanisa utumie fursa
zilizopo kwenye mikoa hiyo za kilimo, madini na gesi asilia kwa kuwahamisha
waumini wake na kuwabadilisha kifikra ili wazitumie fursa hizo kujiletea
maendeleo na kujikomboa kiuchumi.
Akizungumzia kuhusu mauaji ya watu wenye
ulemavu wa ngozi, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini washirikiane
na Serikali kukemea kwa nguvu zote vitendo hivyo vya kikatili. “Tangu mwaka
2006 kumetokea mauaji ya watu 46 na kati ya hayo, matukio 43 yalikuwa kwenye ukanda
ya ziwa na mikoa ya magharibi. Niwaombe tena taasisi zote za dini zitusaidie
kuondoa au kubadili imani hizi za kishirikina miongoni mwa jamii. Ninaamini
tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja dhidi ya fedheha hii tutashinda,”
alisisitiza.
Mapema, akitoa mahubiri katika ibada hiyo ya uzinduzi,
Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Dk. Isack Nikodemo aliwataka
waumini wa Kikristo Tanzania waombe sana kwa ajili ya amani ya Taifa hili hasa
katika kipindi hiki ambacho Taifa linajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
“Kanisa la Tanzania kaeni magotini kwa Yesu, liitieni
jina la Bwana kwa sababu amani inahitajika sana. Taifa la Tanzania liko safarini,
linahitaji amani wakati huu kuliko wakati mwingine, hata kama mawimbi yatainuka
kama mlima, mwiteni yeye naye atatuliza dhoruba zote,” alisema huku akinukuu
neno kutoka kitabu cha Marko sura ya nne aya ya 35-41.
Alisema hata katika maisha ya kila siku, watu
wanakumbana na safari za aina mbalimbali iwe ni kazini, kwenye ndoa au kwenye familia.
Alionya kuwa ipo hatari ya kusafiri bila Yesu katika maisha ya mwanadamu.
Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu pia alitoa vyeti
na nishani kwa Askofu mstaafu Lusekelo Mwakafwila na wachungaji wengine wanane
pamoja na wazee wawili ikiwa ni ishara ya kanisa hilo kutambua mchango wao wa
kueneza injili katika jimbo la Mashariki tangu likiwa chini ya Jimbo la Kusini.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment