WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imeanzisha Kurugenzi ya Wauguzi na Wakunga
katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kurahisisha utatuzi wa changamoto
zinazowakabili kwenye utoaji wa huduma kwa umma.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Mei 5, 2015), wakati akizungumza wauguzi na
wakunga pamoja na wakazi wa mkoa wa Mara kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku
ya Wakunga Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mkendo, mjini Musoma.
“Nina
taarifa kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha (2015/2016), Kurugenzi hiyo itakuwa na
bajeti yake yenyewe itakayotumika kuboresha huduma za wauguzi na wakunga
nchini. Haya yote yanafanyika kwa kuwa Serikali inatambua na kuthamini shughuli
za wauguzi na wakunga hapa nchini,” alisema.
Alisema
mafanikio yaliyofikiwa ya kupunguza vifo vya watoto na vifo vya wanawake
yamechangiwa na kazi nzuri zinazofanywa na wakunga licha ya kuwa kada hiyo
inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi.
Alisema
ili kukidhi mahitaji ya wakunga nchini, Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi
wanaojiunga na fani ya uuguzi na ukunga. Akitolea mfano, Waziri Mkuu alisema:
“Mwaka 2009 tulikuwa na wanafunzi wa uuguzi na ukunga 617 wa ngazi ya Cheti na
925 wa ngazi ya Diploma. Kufikia mwaka 2014 idadi hiyo iliongezeka kufikia
wanafunzi 2,566 wa Cheti sawa na ongezeko la asilimia 315 na wanafunzi 2,294 wa
Diploma sawa na ongezeko la asilimia 141 katika kipindi cha miaka mitano.”
Akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na hadhara hiyo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi Jamii,
Dk. Stephen Kebwe alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika
ambazo zimeweza kupunguza vifo vya watoto na kuvuka Malengo ya Milenia.
Alitumia
fursa hiyo kuwahimiza wanaume wa mkoa huo na wanaume wote nchini kukubali
kutumia njia za uzazi wa mpango ili wawasadie wenza wao kuwa na afya imara. Pia
aliwataka waachane na dhana potofu za mitaani bali wafuate tiba na huduma
sahihi uzazi wa mpango kwenye vituo vya afya.
“Inashangaza
kuona baadhi ya wanaume wanawaacha wake zao eti kwa sababu hawazai, lakini
wakiwaacha baada ya muda unasikia yule mama amepata ujauzito, hapo kosa ni la
nani?” aliuliza.
“Pia
ninawasihi akinababa waachane na dhana potofu kuhusu njia ya kufunga kizazi.
Ninawahimiza washiriki njia hii ya kufunga kizazi wanaposhauriwa kufanya hivyo
kwa sababu kufunga ule mrija hakumuondolei mwanaume hadhi ya kufanya tendo la ndoa,
bado inawezekana hata baada ya kufunga mrija,” alisisitiza.
Mapema, akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkazi wa
taasisi ya Mama Ye, Bw. Craig Ferla aliitaka Serikali na wadau waliangalie
suala la vifo vya akinamama na watoto kwa jicho la tofauti na kulipigia kelele
zaidi ili uwekezaji kwenye fani ya ukunga na uuguzi uweze kuongezwa.
Bw.
Ferla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Utepe Mweupe wa Muungano wa Uzazi
Salama Tanzania, alisema Serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakipigia kelele
idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani lakini hakuna mtu anayesema
chochote kuhusu vifo vya wanawake na watoto wachanga.
“Watu
wanapiga kelele kuwa Taifa limepoteza watu 972 kati ya Januari na Aprili mwaka
huu, lakini hatujui kwamba katika kipindi hicho hicho Taifa limepoteza wanawake
na watoto 15,000 kutokana na matatizo ya uzazi na hii ni mara 15 zaidi lakini
hakuna anayepiga kelele,” alifafanua.
Alisema
wanawake 8,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na uzazi wakati watoto
40,000 hupoteza maisha wakiwa katika mwezi wao wa kwanza duniani. “Vifo vya
ebola tangu ianze vimefikia 10,000 lakini dunia nzima imeitikia lakini hivi vya
akinamama hakuna anayesema chochote.”
“Kuna
tatizo jingine ambalo linakwenda kimyakimya nalo ni la vifo vya watoto
wanaozaliwa wafu. Hawa wanafikia 47,000 kwa mwaka ambao ni karibu watoto 15,000
kwa miezi minne lakini nalo pia hakuna anayelisemea licha ya kuwa ni janga
kubwa kitaifa,” aliongeza.
“Ninaiomba
Serikali na wadau wawekeze zaidi katika kada ya wakunga ili tuweze kuokoa
maisha ya akinamama na watoto,” alisema Mkurugenzi huyo ambaye kwa muda wote
alitumia Kiswahili fasaha na kuufanya mkutano mzima umshangilie kwa nguvu.
IMETOLEWA
NA
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
2
MTAA WA MAGOGONI.
No comments:
Post a Comment