WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amepokea hundi ya
mfano (dummy cheque) yenye thamani ya sh. bilioni 1.5 kutoka benki ya NMB zikiwa
ni mchango wa taasisi hiyo kwenye kampeni ya uchangiaji madawati kitaifa.
Akizungumza na Waziri Mkuu ofisini kwake Magogoni
jijini Dar es Salaam jana jioni (Jumatano, Aprili 29, 2015), kabla ya kukabidhi
hundi hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bw. Tom Borghols alisema
wameamua kutoa mchango ili kusaidia kupunguza tatizo la uhaba wa madawati
linalozikabili shule za msingi na za sekondari hapa nchini.
“Tunaelewa kwamba shule nyingi hapa nchini
zinakabiliwa na uhaba wa madawati … tunaamini kuwa elimu bora inachangiwa pia
na mazingira mazuri ya kusomea ikiwa ni pamoja na kukaa kwenye madawati
wanapoandika. Kama sehemu ya mchango wetu kwa jamii (CSR), tumeamua kutenga sh.
bilioni 1.5 ili zisaidie kupungua tatizo hilo,” alisema.
Akipokea mchango huo, Waziri Mkuu aliushukuru
uongozi wa benki hiyo ulioambatana na Bw. Borghols kwa kuamua kusaidia juhudi
za Serikali kutatua tatizo hilo. Alisema mchango huo ni mkubwa na anaamini
kwamba utawachochea wadau wengine kuchangia juhudi za Serikali kutatua tatizo
la madawati nchini.
“Nimecheki na watu wangu kwa kweli mahitaji ni makubwa
lakini naamini mchango wenu utasaidia kupunguza tatizo la madawati kwa kiasi
fulani. Tunawashukuru kwa uamuzi wenu wa kuchangia suala hili la kitaifa,”
alisema.
Hadi sasa Serikali inahitaji kununua madawati
1,016,476 kwa ajili ya shule za msingi na za sekondari. Kati ya hayo, madawati
892,772 yanahitajika kwa ajili ya shule za msingi na madawati 123,704
yanahitajika kwa ajili ya shule za sekondari.
Madawati hayo yote yataigharimu Serikali kiasi
cha sh. bilioni 91.4/- kwa gharama ya sh. 90,000/- kwa kila dawati.
Hata hivyo, Serikali iliamua kutenga fedha za
chenji ya RADA ili zitumike kununua madawati na vitabu. Fedha hizo, zilisaidia
kununua madawati 168,163 kwa bei ya sh. 90,000/- kwa dawati moja.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment