Ndugu Gratian Mukoba, Rais wa Shirikisho la Vyama
vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Ndugu Nicholaus Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Mheshimiwa Gaudentia Mugosi Kabaka, Waziri wa Kazi
na Ajira;
Mheshimiwa Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza;
Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara;
Ndugu
Alexio Musindo, Mkurugenzi Ofisi ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa nchi za
Tanzania, Kenya, Rwanda na Burundi;
Ndugu Almasi
Maige, Rais wa Chama cha Waajiri;
Dr. Aggrey Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama
cha Waajiri Tanzania (ATE);
Waheshimiwa Mabalozi;
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa;
Viongozi Waandamizi wa Serikali;
Ndugu Wananchi na Wafanyakazi Wenzagu;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Nakushukuru sana Rais wa TUCTA Ndugu Gratian Mukoba
na viongozi wenzako wa vyama vya wafanyakazi
kwa kunialika kuja kushiriki nanyi katika sherehe za mwaka 2015 za Mei Mosi
hapa Mwanza. Aidha, natoa pongezi nyingi
kwa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi na Ujenzi Tanzania (TAMICO) ambao ndio
wenyeji wetu mwaka huu kwa maandalizi mazuri ya Sherehe hizi. Hakika yamefana
sana.
Sote ni mashahidi wa jinsi maandamano na maonesho
ya kazi za wafanyakazi wa Tanzania yalivyopendeza. Nimesoma mengi ya mabango ya
waandamanaji, napenda kuwahakikishia kuwa ujumbe umefika.
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza ndugu zetu
wa Mkoa wa Mwanza wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Ndugu Magesa Mulongo kwa
kukubali kuwa wenyeji wa maadhimisho ya sherehe hizi. Mmetupokea vizuri na kutukirimu kwa heshima
kubwa. Tunajisikia tuko nyumbani.
Ndugu Rais wa TUCTA;
Kwa mara nyingine tena nakupongeza kwa kuchaguliwa kwako
kuwa Rais wa TUCTA. Sisi katika Serikali
tumeupokea kwa furaha uchaguzi wako. Narudia kukuhakikishia ushirikiano wangu
na wa wenzangu wote katika Serikali ninayoiongoza, katika utekelezaji wa majukumu
yako. Ni matumaini yetu kuwa
tutashirikiana kwa ukamilifu katika kuendeleza maslahi na ustawi wa wafanyakazi
wa Tanzania na nchi yetu.
Ndugu
wafanyakazi;
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapa pole kwa
msiba mkubwa mlioupata wa
kuondokewa na Bwana Erasto John Kihwele
aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU). Hakika
mmepoteza kiongozi mahiri katika kujenga hoja na kupigania haki za wafanyakazi
wa reli. Namkumbuka sana kwa jinsi alivyosimama
kidete kutetea wafanyakazi wa TAZARA katika kikao chetu cha pamoja mwaka jana.
Utetezi wake ulizaa matunda kwa kuanzishwa kwa Baraza la Wafanyakazi TAZARA.
Kwa kweli sote tumepata pigo. Nawaomba
muendeleze yale mazuri aliyoyasimamia. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu
mahali pema peponi”. Ameen.
Pongezi kwa Wafanyakazi Bora
Ndugu Wafanyakazi;
Kama
ilivyo ada leo tena tunawapongeza wafanyakazi wenzetu waliotekeleza vizuri
majukumu yao katika maeneo yao ya kazi.
Tunawapongeza kwa kazi yao njema iliyowawezesha kuibuka washindi kati ya
wafanyakazi wengi walio bora. Nawapongeza
na kuwasihi waendelee na ari na moyo huo wa kuchapa kazi kwa bidii, nidhamu na
maarifa. Ni matumaini yangu kuwa mafanikio
yao yatakuwa kichocheo kwa wengine kuongeza bidii zaidi ili waweze kufikia na
hata kuzidi viwango vyao vya ubora mwakani.
Risala ya Wafanyakazi
Ndugu Rais wa TUCTA na Wafanyakazi Wenzangu;
Nimeisikiliza na kuifuatilia kwa makini sana risala ya wafanyakazi
iliyowasilishwa kwa ufasaha na Katibu Mkuu wenu mahiri, Ndugu Nicholas
Mgaya. Nawapongeza kwa risala nzuri
iliyobeba maneno ya shukrani, changamoto, faraja na karaha za wafanyakazi. Risala yenu pia imekuwa na maoni yakinifu
kuhusu namna ya kuyapatia ufumbuzi baadhi ya matatizo yaliyotajwa. Nataka kuwahakikishieni kuwa nimeisikiliza
neno kwa neno na kituo kwa kituo.
Nimeyasikia yale mliyosema kwa uwazi na hata yale mliyoyasema kwa
mabano. Nimeyapokea, tumeyapokea na kama
ilivyo kawaida yetu tutayashughulikia kwa uzito unaostahili. Baadhi yake nitayazungumzia katika hotuba
yangu hii.
Kauli Mbiu
Ndugu Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Nimefurahishwa na kauli mbiu ya Sherehe za mwaka
huu isemayo “Jiandikishe, kura yako ni
muhimu kwa maendeleo”. Kauli mbiu
hii ni muafaka kabisa na wakati tulionao sasa.
Ni kauli mbiu inayokumbusha wajibu muhimu wa kila mfanyakazi na kila
Mtanzania. Kupiga kura kuchangua viongozi na, kwa ajili ya kuamua mambo muhimu
kitaifa, yanayotakiwa kuamuliwa kwa Kura ya Maoni kama ilivyo Katiba
Inayopendekezwa, ni haki na wajibu wa msingi wa raia. Lakini, ili mtu aweze
kuitumia haki yake hiyo na kutimiza wajibu wake huo lazima awe na kitambulisho
cha mpiga kura. Kitambulisho hicho hupatikana kwa kujiandikisha katika Daftari
la Mpiga Kura.
Naungana nanyi kuwahimiza wafanyakazi mjitokeze
kujiandikisha pale mtakapotangaziwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya
hivyo. Ni muhimu sana kuitumia fursa
hiyo vizuri kwani haitarudi itakapopita.
Narudia kukumbusha kuwa watakaopiga kura mwaka huu ni wale tu wenye
vitambulisho vipya vya mpiga kura. Vya zamani havitambuliki.
Ndugu wafanyakazi;
Ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo yanategemea
kuwa na Katiba nzuri na viongozi wazuri. Hivyo basi, usiipoteze fursa hii
adhimu kwa ajili ya kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa na kuchagua Rais,
Mbunge, Mwakilishi na Diwani unayemuona anafaa. Hali kadhalika, ninyi mna
ndugu, marafiki na kama viongozi wa kaya mnao wategemezi majumbani mwenu ambao
wengine wanazo sifa za kuwa wapiga kura. Nawaomba muwakumbushe na kuwahimiza wajitokeze kujiandikisha
na siku ikifika waende kupiga kura.
Ndugu Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Hii ndiyo sherehe ya Siku ya Wafanyakazi ya mwisho kwangu
kuhudhuria nikiwa Rais wa nchi yetu.
Nimekuwa nanyi kwenye maadhimisho haya kila mliponialika. Katika miaka
10 ya uongozi wangu tumefanya jitihada kubwa kukuza ajira na kuinua hali za
wafanyakazi nchini. Nafarijika sana
kuona kuwa naondoka wakati ambapo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyatekeleza
yale tuliyopanga kufanya.
Ndugu Rais wa TUCTA;
Leo hii tukitazama tulikotoka na tulipo sasa
tunaiona tofauti kubwa. Ninaposema hayo
sina maana kuwa matatizo na changamoto zote za wafanyakazi zimekwisha. La
hasha! Natambua pia kuwa isingelikuwa rahisi kumaliza mambo yote yanayowasibu
wafanyakazi katika kipindi hiki. Tunachojivunia, ni kule kuweza
kuzishughulikia kwa ufanisi changamoto za msingi za wafanyakazi. Hata hivyo ni
muhimu kutambua kuwa bado tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Katu tusibweteke
na kulevywa na mafanikio haya. Hatujafika katika safari yetu. Madamu tuko
katika mwendo, tutafika.
Kuboresha Mazingira ya Kazi
Ndugu Wafanyakazi;
Kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali
yetu tumefanikiwa kujenga taasisi, mifumo na sheria zinazoweka misingi imara ya
utatuzi wa changamoto za wafanyakazi. Tumetunga Sheria na Kanuni mbalimbali kwa
lengo la kulinda haki za msingi za wafanyakazi pamoja na kuweka mazingira bora
ya kazi ikiwemo uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa. Sheria na Kanuni hizi ni zile zinazohusu
viwango vya kazi, hifadhi ya jamii, na ajira. Kanuni za kutekeleza Sheria ya
Ajira na Mahusiano Na.6 ya 2004 zilitengenezwa na kuanza kutumika mwaka
2007.
Kuanza kutekelezwa kwa Sheria hii kumewezesha kuanzishwa
na kuimarishwa kwa Taasisi mbalimbali za kazi, zikiwemo Idara ya Usimamizi Kazi
na Huduma za Ukaguzi (Idara ya Kazi), Usajili wa Vyama vya Waajiri na
Wafanyakazi, Mahakama ya Kazi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya
Kikazi (CMA), Bodi za Mshahara za Kisekta, Kamati ya Huduma Muhimu (Essential
Services Committee) ya CMA na Baraza la Ushauri la Kazi, Uchumi na Jamii
(LESCO). Kuwepo kwa vyombo hivi
kumesaidia sana kuweka uwanja wa majadiliano kuwa sawa kati ya waajiri na
waajiriwa.
Ushirikishwaji wa Wafanyakazi
Ndugu
wafanyakazi;
Tangu
tulipoingia madarakani katika awamu hii, tumetoa kipaumbele cha juu katika
kuhakikisha kwamba ushirikishwaji wa Wafanyakazi unakuwa sehemu ya utamaduni
katika sehemu za kazi. Kwa maneno mengine ni kwamba tumesisitiza utekelezaji wa
matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano
Kazini Na.6 ya 2004.
Juhudi
zetu hizo zimezaa matunda. Tumeshuhudia Vyama
vya Wafanyakazi vikiongezeka kutoka vyama vya Wafanyakazi 18 hadi 30 ambavyo
vimesajiliwa ili kutetea maslahi ya Wafanyakazi. Aidha, Mashirikisho mawili (2)
na Chama cha Waajiri kimoja (1) vimesajiliwa.
Kwa lugha nyepesi tumewapa wafanyakazi sauti juu ya maslahi, hatima na
mustakabali wao. Hata kwenye Bunge la Katiba wafanyakazi walishirikishwa kwa
ukamilifu.
Mabaraza ya Wafanyakazi
Ndugu wafanyakazi;
Kwa upande wa utumishi wa umma, takwimu zinaonyesha
kwamba Mabaraza ya Wafanyakazi yameundwa katika Wizara zote 26; Idara za Serikali 19; Wakala za Serikali 25 na Mamlaka za mikoa 21 na Halmashauri za Wilaya na Miji 168.
Mengi ya Mabaraza hayo yamekuwa yanakutana kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Hata
hivyo zipo Idara za Serikali 4;
Wakala za Serikali 7; Mikoa 5;
na Mamlaka za Serikali za Mitaa 34
bado hazijaunda Mabaraza hayo kwa sababu mbalimbali.
Nimemuelekeza Waziri wa Kazi na Ajira na Katibu
Mkuu Kiongozi wawabane wale wote ambao bado hawajaunda Mabaraza ya Wafanyakazi
ili wafanye hivyo bila kuchelewa zaidi.
Pia, kwa wote, waliounda Mabaraza na wale wote watakaounda ihakikishwe kuwa
mabaraza hayo yanakutana mara mbili kwa mwaka kama Sheria inavyotaka. Kisingizio cha uhaba wa fedha hakiniingii
akilini hata kidogo. Mbona sijawahi kusikia viongozi wamekosa posho za safari
na vikao vyao! Hayo ni matakwa ya
kisheria, na ni agizo la Rais hivyo lazima kupewa kipaumbele katika utekelezaji.
Ndugu wafanyakazi;
Jambo
jingine zuri ambalo tumelifanya kwa ufanisi katika kipindi hiki ni kuwa na utaratibu
wa Rais kukutana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi. Tulianza kwa kukutana mara
moja baadae tukaongeza na kuwa mara mbili kwa mwaka. Japo wakati mwingine imekuwa sio rahisi sana
kukutana mara mbili kwa sababu ya ratiba za Rais, lakini hatukukosa kukutana angalau
mara moja.
Mimi
na viongozi wa vyama vya wafanyakazi ni shahidi kwamba vikao hivi vimesaidia
sana kuleta maelewano baina ya Serikali na Vyama vya Wafanyakazi na hivyo baina
ya Serikali na wafanyakazi. Vikao hivi vimekuwa fursa maalum ya
kuzungumzia masuala mbalimbali yanayowahusu wafanyakazi na kuyatafutia
ufumbuzi. Ukweli ni kwamba matatizo
mengi tumeweza kuyatatua hata yale ambayo wakati mwingine yalionekana kuwa
magumu sana.
Mwaka
huu tumeshakutana mara moja. Ni matumaini yangu kuwa tutapata fursa ya kukutana
tena, kabla sijang’atuka. Utakuwa mkutano wa kuagana. Nitamnong’oneza Rais
ajaye kuhusu manufaa ya utaratibu huu, ili ikimpendeza auendeleze. Huu ni utaratibu wa kisheria, umekuwa na manufaa
makubwa sana. Kama mlivyosema, umesaidia kujenga maelewano mazuri na
ushirikiano baina ya Serikali na wafanyakazi, jambo ambalo ni muhimu sana
katika kuleta mustakabali mwema nchini.
Naikumbuka pia ahadi yangu ya kukutana na viongozi wa Chama cha Waajiri.
Nitatafuta wasaa hivi karibuni tukutane.
Usuluhishi wa Migogoro ya kikazi
Ndugu Wafanyakazi;
Katika awamu hii tumejitahidi sana kushughulikia
migogoro ya kikazi kwa kupunguza muda wa mashauri kusikilizwa na hivyo
kuwezesha wafanyakazi kupata haki zao kwa wakati. Kama nilivyosema awali, mwaka 2008 tulianzisha
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambayo jukumu lake ni kushughulikia migogoro
ya kikazi. Tangu kuanzishwa kwake Taasisi hii imefanikiwa kushughulikia migogoro
ya kikazi 10,281 ambapo migogoro 6,057 imeshatolewa uamuzi. Tume imeweza
kupunguza muda wa kusuluhisha na kusikiliza mashauri ya migogoro ya kazi kutoka
wastani wa siku 30 hadi 12 na muda wa kuamua umepungua kutoka wastani
wa siku 90 hadi 85.
Kupungua kwa muda wa mashauri kusikilizwa na
kuamuliwa maana yake ni kupunguza usumbufu na madhila kwa mfanyakazi ambaye
hapo awali alichelewa sana kupata haki yake. Wakati mwingine kuchelewa kupata
haki kwa wakati kulitafsiriwa kama haki iliyodhulumiwa. Utaratibu huu umepunguza pia mlundikano wa
kesi za masuala ya kazi mahakamani. Kasoro mlizozitaja katika risala yenu
kuhusu utendaji wa CMA tutazifanyia kazi.
Usimamizi wa Ajira
Ndugu Wafanyakazi;
Kumekuwepo na malalamiko ya wafanyakazi juu ya
kukithiri kwa idadi ya wageni wasio na sifa za kufanya kazi nchini ambao
wanaajiriwa. Niliahidi katika hotuba yangu
ya Mei Mosi mwaka jana kwamba tutatunga Sheria maalum na kuweka utaratibu wa
kisheria wa kusimamia ajira za wageni nchini.
Aidha, nilimwelekeza Waziri wa Kazi na Ajira akamilishe kanuni za
kusimamia mawakala binafsi wa huduma za ajira.
Nafurahi kuwa ahadi yangu ile imetimia kwa kutungwa
kwa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni katika Bunge la Machi, 2015. Kilichobakia sasa ni Waziri wa Kazi na Ajira
kutengeneza Kanuni za utekelezaji wa Sheria hiyo. Ningependa kazi hiyo ikamilike mapema ili Sheria
ianze kutumika mapema iwezekanavyo.
Ndugu Wafanyakazi;
Kuhusu makampuni ya mawakala wa ajira, Serikali imekwishaweka
utaratibu mzuri wa kuyatambua, kuyasajili upya na kuyatengenezea kanuni za
kuongoza utendaji wao. Kwa ajili hiyo,
hivi sasa Wizara inaweza kuyakagua na kujiridhisha iwapo yanafuata sheria za
kazi. Tayari makampuni 96 yameshasajiliwa. Hata hivyo, ili
shughuli hii iweze kufanikiwa ushirikiano wa wafanyakazi ni muhimu.
Inasikitisha kusikia kuwa, wapo wafanyakazi wanaokataa kutoa taarifa za
ukiukwaji wa Sheria unaofanywa na makampuni haya kwa kuogopa kupoteza ajira
zao.
Napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali itasimamia kwa
nguvu zote utekelezaji wa jambo hili. Haitasita kuchukua hatua stahiki dhidi ya
Mawakala watakaokiuka sheria za ajira nchini, watakapobainika kufanya hivyo. Tafadhalini timizeni wajibu wenu wa kutoa
taarifa kuhusu wale wanaovunja Sheria na taratibu.
Hifadhi ya Jamii
Ndugu Wafanyakazi;
Katika
kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne tumeboresha sana huduma
ya hifadhi ya jamii ambayo ni moja ya haki za msingi kwa wafanyakazi. Hivi sasa
tunaangalia uwezekano wa kujumuisha makundi mengine wakiwemo wakulima na wazee.
Mabadiliko
ya kisheria na kisera tuliyochukua yameongeza wigo wa mafao, aina ya mafao na
ongezeko la mafao kwa wafanyakazi. Takwimu
zinaonyesha kwamba idadi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeongezeka toka Mifuko 5 mwaka 2005 hadi mifuko 7 hivi sasa. Hali kadhalika, kumekuwepo na ongezeko kubwa la
wanachama na wale wanaofaidika na huduma za hifadhi ya jamii hususan wafanyakazi
na wategemezi wao. Idadi imeongezeka kutoka 690,000 mwaka 2005 hadi 6,400,000
mwaka 2014. Haya ni mafanikio makubwa sana.
Ndugu Rais wa TUCTA na wafanyakazi;
Habari
nyingine njema ni kuwa hatimaye kile kilio chenu cha kutaka kuoanisha mafao ya
mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwa na kokotoo la aina moja kimepata ufumbuzi. Matokeo yake ni kwanza, kwamba mafao ya malipo ya pensheni ya mwezi sasa yameongezeka
kwa asilimia 5 kutoka asilimia 67 hadi asilimia 72.5. Pili, ni kuwekwa kwa kiwango cha chini cha asilimia 40 ya mshahara hata kwa
mwanachama ambaye pensheni yake ingekuwa chini ya asilimia 40 ya mshahara. Hii
ina maana kuwa hakuna mwanachama wa mfuko wowote atakayepata pensheni ya chini
ya asilimia 40 ya mshahara hata kama
kwa masharti ya mfuko wake kabla ya uamuzi huu angestahili kupata chini ya hapo.
Uamuzi huu unajenga usawa wa mafao kwa
wanachama wote wa mifuko yote.
Ndugu Wafanyakazi;
Napenda
kusisitiza kuwa mabadiliko haya hayataathiri wanachama wa mifuko ya PSPF na
LAPF ambao waliajiriwa kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa ukokotoaji
tulioanza tarehe 1 Julai, 2014. Najua ipo
hofu fulani ambayo na hata katika mkutano wangu na viongozi wa Vyama vya
Wafanyakazi ilijitokeza (na leo pia imeelezwa kwenye risala yenu). Tulikubaliana mazungumzo zaidi yafanyike kati
ya TUCTA na SSRA kuhusu jambo hili.
Hivyo nawaomba muwe na subira.
Heri itapatikana kama walivyosema Wahenga.
Nafurahi
kutoa taarifa kuwa ufumbuzi umepatikana kuhusu suala la mafao kwa wale wafanyakazi
ambao wakati wa utumishi wao, kabla ya kustaafu walichangia mifuko tofauti. Hawa
ni wale ambao walihama au kuhamishwa kutoka Halmashauri za Wilaya na Miji na
kwenda Serikali Kuu au kinyume chake. Kwa sababu hiyo wamechangia katika mifuko
tofauti. Wanapostaafu wamekuwa wanapata ugumu katika malipo na kujikuta
wanapoteza haki na stahili za utumishi wao wa muda mrefu. Mwongozo wa kuunganisha michango ya wanachama
waliochangia katika mfuko zaidi ya mmoja umeshatolewa na umeanza kutumika tangu
tarehe 25 Aprili, 2014. Tatizo limemalizika na tayari SSRA imeshatatua
malalamiko ya wanachama wapatao 11,070
waliokuwa wamekabiliwa na matatizo ya namna hii.
Mfuko wa Fidia
Ndugu Wafanyakazi;
Kile kilio cha siku nyingi cha fidia ya wafanyakazi
wanaoumia kazini nacho kimefutwa machozi.
Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi (Workers Compensation Fund) umeanzishwa kwa
mujibu wa Sheria ya Fidia ya Wafanyakazi Na.20 ya mwaka 2008. Nimeshafanya
uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Ndugu Masha Mshomba na Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini Ndugu Emmanuel Humba. Waziri wa Kazi na Ajira ameshateua Wajumbe wa
Bodi hivyo kazi imeanza. Kazi inayoendelea sasa ni kuandaa kanuni za uendeshaji
wa Mfuko huo zinazotarajiwa kukamilika Juni, 2015.
Kama nilivyosema mwaka jana, Mfuko huu utachangiwa
na waajiri wote yaani Serikali na wa sekta binafsi. Mfuko utaondoa ule mwanya wa baadhi ya waajiri
kukwepa wajibu wa kulipa fidia pale yanapotokea madhara kwa wafanyakazi wao.
Kwa hatua hii wafanyakazi sasa wana
hakika ya kulipwa fidia stahiki.
Maslahi ya Wafanyakazi
Ndugu
Rais wa TUCTA;
Wafanyakazi
Wenzangu;
Jambo lingine ambalo tumejitahidi kufanya bila
ajizi ni kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Pamoja na changamoto tulizonazo kwa
upande wa mapato na ukubwa wa majukumu ya serikali tumechukua hatua za makusudi
kuongeza kima cha chini cha mishahara katika utumishi wa umma kila mwaka tangu
tuingie madarakani. Kwa ajili hiyo, katika
utumishi wa umma, kwa mfano, kima cha chini cha mshahara mwaka 2005 kilikuwa shilingi 65,000, mwaka 2014 kima cha
chini kimeongezeka na kufikia shilingi 265,000.
Ni nyongeza ya zaidi ya mara nne. Najua kwa hali ilivyo sasa ongezeko hili bado
ni ndogo lakini si haba. Naahidi kuwa na
mwaka huu pia tutaongeza.
Punguzo la Kodi kwa Wafanyakazi (PAYE)
Ndugu wafanyakazi;
Tumeendelea kupunguza kiwango cha kodi ya mapato
kwa wafanyakazi (PAYE) mwaka hadi mwaka tangu 2005 hadi sasa. Kwa ajili hiyo, kodi hiyo iliyokuwa asilimia 18 sasa ni asilimia 12. Na mwaka huu pia tutaendelea kupunguza kodi
ya mapato kwa wafanyakazi. Natambua kuwa
maombi yenu ni kutaka iwe chini ya asilimia
10. Hatukuweza kufikia hapo mwaka
huu lakini safari tuliyoianza na hapo tutakapofikia itabakisha padogo sana
kufikia tunapopataka sote.
Ndugu Wafanyakazi;
Kama nilivyosema mwaka jana, kwa upande wa wafanyakazi
katika sekta binafsi kima cha chini kinapangwa na Bodi za Mishahara za kisekta zinazoundwa
na Waziri wa Kazi. Hadi kufikia mwaka 2011
tulikuwa nazo Bodi 12 ambazo zimewezesha
majadiliano na waajiri wa sekta binafsi kufanyika. Matokeo yake ni kima cha chini
cha mshahara kupanda kutoka shilingi
48,000 kwa mwezi hadi kati ya shilingi
100,000 na 400,000 kutegemeana na sekta.
Kwa kuwa bodi hizo zinakutana kila baada ya miaka mitatu, na mara ya
mwisho mishahara iliongezwa mwaka 2013
hivyo basi viwango vipya vinatarajiwa kutangazwa mwaka 2016.
Naambiwa kuwa bado wapo waajiri wasiolipa viwango
hivi ambavyo vimekubaliwa kwa pamoja baina yao na wafanyakazi. Hili si jambo la kiungwana na linalonihuzunisha
sana. Ndugu Almasi tusaidie tabia hii iachwe. Nazitaka mamlaka husika kutimiza ipasavyo
wajibu wao wa kuhakikisha maamuzi ya Bodi yanatekelezwa. Tusikubali watu hao wakaendelea kudhulumu
haki za wafanyakazi. Pendekezo la kutaka
kuwepo na Bodi moja badala ya kila sekta kuwa na Bodi yake limepokelewa na
litafanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA)
Ndugu Wafanyakazi;
Serikali yetu
imetoa umuhimu mkubwa kwa uimarishaji wa afya ya wafanyakazi na usalama mahala
pa kazi. Mafanikio makubwa yamepatikana.
Kati ya mwaka 2010 na 2015 Wakala wa Afya na Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) umefanya
kaguzi za kawaida 26,000 na kaguzi maalumu 53,000. Hali kadhalika, wafanyakazi wapatao 435,063 wamepimwa afya zao kwa lengo la
kubaini matatizo na athari wazipatazo wakati wakiwa kazini na hata baada ya
kuacha kazi. Mwaka 2014, OSHA imefanya ukaguzi kwenye
migodi yote nchini na kutoa maelekezo juu ya namna ya kuboresha hali katika
migodi hiyo. Tutaendelea kuiimarisha
OSHA ili iweze kufanya kaguzi nyingi zaidi na kwa wakati muafaka.
Marekebisho ya Miundo na Madai ya Wafanyakazi
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;
Katika kipindi cha miaka 10 hii, tumefanya marekebisho ya miundo ya utumishi
ya kada mbalimbali za utumishi wa umma.
Miundo miwili ninayopenda kuzungumzia leo ni ile ya walimu na
wauguzi. Kwa upande wa walimu, muundo wa
walimu umeidhinishwa na utekeleaji wake umeanza tangu Julai, 2014. Nimeambiwa kuwa utekelezaji haujaanza kote
kwa wakati mmoja, lakini nimehakikishiwa kuwa wote watahamia kwenye muundo mpya
katika mwaka ujao wa fedha.
Sambamba
na hili la muundo, malimbikizo ya stahili za walimu yameendelea kulipwa. Mwaka huu madai ya deni la walimu yalikuwa shilingi bilioni 53,185,440,406 yanayowahusu
na walimu 70,668 yalipokelewa. Uhakiki umefanyika na tayari, walimu 29,243 wamekwishalipwa jumla ya shilingi bilioni 23,233,654,025.
Madai mengine ya walimu 7,169
ya jumla ya shilingi 9,285,283,600 yataanza kulipwa mwezi
Agosti, 2015. Katika uhakiki uliofanywa,
madai ya walimu 30,807 yenye thamani
ya shilingi bilioni 17,346,593,468
yamekutwa na dosari na hivyo kurejeshwa kwenye Halmashauri na kwa wahusika
kufanyiwa masahihisho. Napenda
kuwahakikishia kuwa hizo zikirekebishwa malipo yatafanyika. Fanyeni hima jambo
hili tulimalize.
Ndugu Rais wa TUCTA;
Tumekwishapeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume
ya Utumishi wa Walimu (Teachers Service Commission) ambao tayari umesomwa kwa
mara ya kwanza. Aidha, tunakamilisha maandalizi ya kuwasilisha Bungeni Muswada
wa kuanzisha Bodi ya Taifa ya Taaluma za Walimu (National Teachers Professional
Board). Yote haya yanathibitisha dhamira na utashi wetu kushughulikia masuala
ya walimu na wafanyakazi kwa jumla.
Shemeji zangu walimu baada ya kufanya hayo nina hakika nawaacha pazuri.
Nimefurahishwa
na uamuzi wenu walimu wa kufungua Benki ya Walimu. Nawapongeza sana kwa hatua hii kubwa na ya
maendeleo. Sisi katika Serikali tunaunga mkono juhudi za walimu na tunaahidi
kutoa ushirikiano wa kuwezesha lengo lenu hili jema kutimia.
Ndugu Wafanyakazi;
Kwa
upande wa kada ya wauguzi, mtakumbuka kuwa tulirekebisha muundo ambao umeanza
kutumika tarehe 1 Julai, 2010. Tumepokea
malalamiko kuwa mabadiliko hayo yameathiri baadhi ya wauguzi kwa viwango vyao
vya mshahara kushuka baada ya kuanza kutumika kwa muundo mpya. Hili ni kosa ambalo halikustahili kutokea. Nimeelekeza lirekebishwe, mara moja. Nimeagiza wale ambao mishahara yao
imeshushwa, warejeshewe mishahara yao ya awali na malimbikizo yao walipwe. Hali
kadhalika, nafurahi kuwa yale maombi ya kutaka ianzishwe Kurugenzi ya kada ya
wauguzi na wafamasiya nayo yamefanyiwa kazi. Kibali kimetolewa na Menejimenti
ya Utumishi wa Umma kwa Kurugenzi hizo kuanzishwa. Kwa sasa ni kitengo.
Ndugu Wafanyakazi;
Katika
kipindi hiki, tumeendelea kushughulikia na kufanikiwa kutatua kero nyingine
nyingi za wafanyakazi. Kati ya mwaka
2005 na 2010, jumla ya watumishi 476,430
wamepandishwa vyeo. Aidha, kati ya mwaka
2012 na 2015, kwa mfano,jumla ya watumishi 125,372
wamelipwa malimbikizo ya jumla ya shilingi
bilioni 123,141,755,959.68. Nimewaagiza ndugu zetu wa Hazina waanze kulipa
madeni ya wafanyakazi wa Serikali za Mitaa yanayofikia shilingi bilioni 18,029,441,595.
Kwa
kweli, mtakubaliana nami kuwa tumejishughulisha kwa kadri ya uwezo wetu
kutafuta majawabu kwa kero na matatizo yanayowakabili wafanyakazi nchini. Hapajakuwako na upungufu wa dhamira upande wetu. Kwa yale ambayo hatukuweza
kuyafanya ni kwa sababu ya ugumu wa tatizo lenyewe kulipatia ufumbuzi au kwa
sababu ya uhaba wa pesa. Hakuna jambo ambalo
hatukujaribu kulishughulikia na juhudi zinaendelea.
Hata wakati huu ambapo nafikia ukingoni
mwa kipindi changu cha uongozi, naendelea na nitaendelea kuyashughulikia mambo
ya wafanyakazi mpaka nitakapokabidhi kijiti kwa kiongozi wetu mpya. Ninawaomba
tuendelee kushirikiana mpaka wakati huo na muendelee kushirikiana na Serikali
ya Awamu ya Tano kama mlivyofanya wakati wangu. Tena ningefurahi kuona
ushirikiano wenu ukiwa mkubwa zaidi hata kuliko wakati wangu. Ni jambo lenye
maslahi kwa pande zote: Serikali, wafanyakazi na nchi yetu.
Fursa za Ajira
Ndugu Wafanyakazi;
Serikali
imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la ajira nchini. Itakumbukwa kuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya
mwaka 2005 – 2010 Chama cha Mapinduzi kiliahidi ajira mpya milioni moja. Tulifanikiwa kuzalisha ajira milioni 1,271,923 ambazo ni zaidi ya lengo. Katika kipindi cha miaka mitano hii, tayari
tumeshazalisha ajira milioni 1,381,621.
Na hivyo kufikisha jumla ya ajira milioni 2,653,544 katika kipindi cha
miaka 10. Kati ya hizo ajira 600,547 zilitokana na sekta ya umma na ajira milioni 2,052,997 zimetokana na sekta binafsi.
Pamoja
na mafanikio hayo, bado tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa hapa nchini na hasa
miongoni mwa vijana. Hivyo basi, tutaendelea
na tunaendelea na utekelezaji wa mikakati na mipango ya kukuza ajira nchini. Wizara ya Kazi na Ajira ikishirikiana na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu, imefanya utafiti wa nguvu kazi nchini tangu mwezi
Februari, 2014 ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, 2015. Utafiti huu utatoa taarifa za soko la ajira
nchini ikijumuisha hali halisi ya kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana.
Napenda
kurudia maneno niliyowahi kuyasema awali kuwa, kwa wakati wa sasa uwezo wa
sekta ya umma kuajiri watu wengi si mkubwa na kwamba jawabu la ajira liko
katika sekta binafsi. Azma ya Serikali
ni kuendelea kujenga mazingira mazuri ya kurahisisha ukuaji wa sekta binafsi na
kuvutia wawekezaji kuongeza mitaji ili kuongeza ajira. Tumefanya hivyo, na matokeo yake tumeyaona. Tutaendelea kufanya hivyo, sasa na siku zijazo.
Hitimisho
Ndugu Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Naomba nimalize hotuba yangu kwa kurudia kuwashukuru
kwa dhati Wafanyakazi wote na viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi nchini kwa
ushirikiano mlionipa katika kipindi chote cha uongozi wangu. Kimsingi ushirikiano na ushauri wenu ulikuwa
wa msaada mkubwa sana kwangu na wenzangu wote katika Serikali kuhusu namna
iliyo bora ya kuzikabili changamoto mbalimbali za wafanyakazi nchini. Ushirikiano wetu huo ndio uliotuwezesha kwa
pamoja kuzitafutia ufumbuzi. Najua kwamba hazikuisha zote. Nawaahidi kuwa Rais
ajaye nitamkabidhi orodha ya yale ambayo bado ni kiporo. Ni imani yangu kwamba
mtaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Awamu ya Tano itakayokuwapo baada
ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015.
Ndugu wafanyakazi;
Narudia kuwashukuru tena kwa kunialika kwenye
sherehe za mwaka huu ambazo zinanipa nafasi ya kuagana nanyi kama Rais wa Jamhuri
ya Muungano Tanzania. Nawashukuru sana kwa wema wenu huo mlionifanyia.
Nawatakia kila la heri katika kutimiza majukumu yenu ya ujenzi wa nchi yetu.
Daima nitawakumbuka. Ninawapenda sana na nitaendelea kuwapenda.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment