UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
kwamba kutokana na Taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Wenyeviti
wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Uchumi,
Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya
Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2014/2015 na Mwelekeo kwa Mwaka
2015/2016. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya
Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Bunge, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu
- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mafungu ya Taasisi zilizo chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu ambazo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Kudhibiti
UKIMWI Tanzania, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Msajili wa Vyama vya
Siasa kwa mwaka 2015/2016.
2.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, kumekuwepo na matukio mbalimbali ambayo yamewagusa Watanzania. Katika
kipindi hiki Bunge lilipata msiba wa Mheshimiwa Kapteni John Damiano Komba aliyekuwa
Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, aliyefariki dunia tarehe 28 Machi, 2015. Tutamkumbuka
marehemu kwa utendaji wake mzuri wa kazi na pia kwa nyimbo zake zenye
mafundisho na kuvuta hisia za watu wengi pamoja na michango yake mizuri kwa Bunge lako Tukufu. Aidha, tarehe 20
Aprili 2015, tulipata msiba wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mheshimiwa Luteni
Kanali Mstaafu, Benedict Kitenga. Vilevile, tarehe 26 Aprili 2015 tulimpoteza ndugu
yetu, mpigania haki na maendeleo kwa nchi za Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita, ambaye aliwahi kuwa
Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika. Pia, kumetokea
vifo, majeruhi na uharibifu wa mali kutokana na ajali za
barabarani pamoja na maafa ya mvua na mafuriko.Tunamwomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka Majeruhi
wote na aziweke Roho za Marehemu Mahali Pema Peponi. Amina! Nitumie fursa hii pia kuwashukuru kwa dhati wale wote waliotoa misaada ya
hali na mali kwa walioathirika na matukio hayo.
3.
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Wajumbe
wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa michango na ushauri waliotoa
wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala,
Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, nitumie fursa
hii kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Jason Samson Rweikiza, Mbunge
wa Bukoba Vijijini ; Kamati ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa
Dkt. Hamisi Andrea Kigwangala, Mbunge wa Nzega; Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa
Joelson Luhaga Mpina, Mbunge wa Kisesa na Kamati ya Masuala ya UKIMWI chini ya
Uenyekiti wa Mheshimiwa Lediana Mafuru
Mng’ong’o, Mbunge wa Viti Maalum, kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya
Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Tume ya
Kudhibiti Dawa za Kulevya na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Maoni na Ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti
ninayowasilisha leo.
4.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu, Serikali ya
Awamu ya Nne inahitimisha kipindi chake cha miaka kumi kuanzia mwaka 2005. Hivyo,
katika Hotuba yangu, nitaelezea kwa muhtasari baadhi ya Mafanikio yaliyopatikana
katika kipindi cha takribani miaka 10 ya
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 na
2010. Aidha, Hotuba hii imeainisha baadhi ya kazi zilizotekelezwa na Sekta mbalimbali
kwa kuzingatia MKUKUTA, Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka
2011/2012 hadi 2015/2016 na Malengo ya Milenia katika kufikia Malengo ya Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025 ya kuwa nchi ya kipato cha kati.
5.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepata
mafanikio makubwa ambayo matokeo yanaonekana katika Ukuaji Uchumi, Kuimarika
kwa Huduma za Kiuchumi na Kijamii na Utawala Bora. Nitumie fursa hii kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa uongozi wake mahiri katika kusimamia vizuri Serikali ya Awamu ya Nne na utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 na 2010. Ninawapongeza pia Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Pia, ninampongeza
Mheshimwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa
kusimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM kwa upande wa Zanzibar. Aidha, ninawashukuru Viongozi na
Watendaji wa Wizara, Taasisi za Serikali, Mikoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali
za Mitaa pamoja na Wananchi wote kwa kutekeleza Ilani kwa mafanikio makubwa. Ni dhahiri kwamba,
mafanikio yaliyopatikana yametokana na wananchi kuikubali na kushiriki
kikamilifu kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
HALI YA SIASA
6.
Mheshimiwa Spika, hali ya kisiasa
nchini imeendelea kuimarika, demokrasia imekua na mwamko wa Wananchi kushiriki
katika shughuli za siasa umeongezeka. Idadi ya Vyama vya Siasa vyenye usajili
wa kudumu imeongezeka kutoka 17 mwaka 2005/2006 hadi 22 mwaka 2014/2015. Katika mwaka 2014/2015,
Chama cha Wananchi na Demokrasia (CHAWADE), Chama cha Maridhiano na Uwiano
(CMU) na Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (CKUT) vimepata usajili wa muda.
Aidha, hadi kufikia mwezi Februari 2015, vyama vingine nane vimewasilisha
maombi ya usajili wa muda.
7.
Mheshimiwa Spika, kukua kwa demokrasia
nchini kumeambatana na changamoto mbalimbali zinazotokana na ukuaji wa Mfumo wa
Demokrasia na matumizi yasiyo sahihi ya demokrasia iliyopo. Ni muhimu sote
tukumbuke kwamba, demokrasia ya vyama vingi inatoa fursa kwa Viongozi na
Wanachama wa Vyama vya Siasa kujenga
hoja za kunadi sera za vyama vyao ili Wananchi wafanye uamuzi sahihi. Katika
kunadi Sera hizo, ni lazima kuheshimiana, kuvumiliana na kuzingatia misingi ya
Sheria na Utawala Bora. Maana ya haya yote ni kupingana kwa hoja bila kupigana.
Hivyo, tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu natoa wito kwa Viongozi na Wanachama
wa Vyama vya Siasa na Wananchi kwa ujumla kuzingatia utii wa Katiba ya Nchi,
Sheria za Nchi ikiwemo Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama
vya Siasa ili kuhakikisha kwamba amani na utulivu uliopo nchini unaendelea kudumishwa.
ULINZI NA USALAMA
Jeshi la Wananchi wa Tanzania
8.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2015, Serikali imeliimarisha na kuliboresha
Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia zana na vifaa mbalimbali vya
kijeshi pamoja na mafunzo. Jeshi limehakikisha kuwa mipaka ya nchi yetu inakuwa
shwari na pia limeshiriki katika shughuli za uokozi wakati wa maafa na
kuwasaidia wananchi kurejea katika hali ya awali. Pia, Serikali imekarabati
miundombinu katika makambi ya jeshi na kujenga Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College). Aidha, Serikali
imekamilisha ujenzi wa nyumba 3,096 kati ya nyumba 6,064 zitakazojengwa katika
Awamu ya Kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba 10,000 za makazi kwa Askari katika
vikosi mbalimbali nchini. Ili kuimarisha amani barani Afrika na kwingineko, Jeshi
la Wananchi wa Tanzania limeshiriki katika Operesheni mbalimbali za Ulinzi wa
Amani huko Darfur – Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Lebanon. Aidha, Jeshi
letu limetuma Waangalizi wa Amani na Maafisa Wanadhimu katika nchi mbalimbali na
kushiriki mazoezi ya pamoja katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na zile
za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Ushiriki huo umewaongezea Wanajeshi
wetu uwezo na uzoefu katika masuala ya ulinzi wa Kimataifa.
Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
9.
Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2013, Serikali
ilirejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mujibu wa Sheria kwa Vijana
waliohitimu Kidato cha Sita. Hadi sasa, jumla ya Vijana 31,635 wamehitimu
mafunzo hayo. Kurejeshwa kwa mafunzo hayo, kumewezesha kuwajengea vijana wetu
ukakamavu, uzalendo, utii na ari ya kulitumikia Taifa. Aidha, mafunzo hayo
yamewajengea vijana wengi stadi na maarifa ya kujiajiri wenyewe. Hivyo, natoa
wito kwa vijana waliopitia mafunzo ya JKT kutumia vizuri stadi na maarifa hayo
kubuni na kuanzisha miradi mbalimbali kama njia ya kujiendeleza na kujikwamua
kiuchumi.
Usalama wa Raia
10.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi
limeendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Katika kipindi cha mwaka
2005 hadi 2015, Serikali imeliimarisha Jeshi hilo kwa kulipatia mafunzo, zana
na vitendea kazi muhimu. Pia, Serikali imejenga Ofisi saba za Makamanda wa
Polisi wa Mikoa na kuboresha makazi ya askari kwa kukarabati na kujenga nyumba
mpya 394 na mabweni 14 katika Mikoa mbalimbali nchini. Aidha, Jeshi la Polisi
limefanikiwa kuhamasisha ulinzi shirikishi na usalama katika jamii kupitia
Dhana ya Polisi Jamii ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Napenda
kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi kuanzisha vikundi 8,876
vya ulinzi shirikishi nchini pamoja na Dawati la Jinsia kwenye Vituo vyote vya
Polisi. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea na ukarabati na ujenzi wa
makazi ya askari na miundombinu pamoja
na kulipatia vifaa na vitendea kazi muhimu. Nitumie fursa hii kuwakumbusha
wananchi wote kwamba msingi wa usalama wa Raia na Mali zao nchini Tanzania ni
wa Watanzania wenyewe. Hivyo, tuna wajibu wa kushirikiana na vyombo vya usalama
kubaini wahalifu pamoja na vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao
na kutoa taarifa kwenye Vyombo vya Sheria kwani hivyo vyote vipo katika maeneo
tunayoishi.
Mauaji ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi
11.
Mheshimiwa Spika, vitendo vya mauaji
ya watu wenye ulemavu wa ngozi na wengine kukatwa viungo kwa sababu ya imani za
kishirikina vimeendelea kulitia doa Taifa letu. Taarifa zilizopo zinaonesha
kuwa, vitendo hivyo vilianza mwaka 2006 ambapo kulikuwa na tukio la mauaji ya mtu
mmoja. Matukio hayo yaliongezeka na kufikia saba (7) mwaka 2007 na 18 mwaka
2008. Mwaka 2009 matukio hayo yalipungua kutokana na juhudi za Serikali na
Wananchi za kupambana na watu wanaofanya vitendo hivyo. Mwaka huo kulikuwa na
matukio tisa (9), mwaka 2010 tukio moja (1) na mwaka 2011 hapakuwa na tukio
lolote. Mwaka 2012 kulikuwa na tukio moja (1); mwaka 2013 tukio moja (1), mwaka
2014 matukio manne (4) na mwaka wa 2015 tukio moja (1). Takwimu hizo zinaonesha
kuwa kuanzia mwaka 2006 hadi 2015, jumla ya watu 43 wameuawa
kutokana na ukatili huo. Hali hiyo imesababisha watu wenye ulemavu wa ngozi
pamoja na familia zao kuishi kwa hofu, mashaka na kushindwa kushiriki
kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Aidha, vitendo hivyo vimeleta taswira
isiyo nzuri kwa nchi yetu ikizingatiwa kwamba watu wengi ndani na nje ya nchi
wanafahamu kuwa Watanzania wanaishi kwa upendo, kuheshimiana na kuthamini
amani, jambo ambalo nchi nyingi zinaendelea kuiga.
12.
Mheshimiwa Spika, katika kupambana na
ukatili huo, jumla ya watuhumiwa 181 walikamatwa na kuhojiwa kati ya mwaka 2006
na 2015. Kati yao, watuhumiwa 133 wamefikishwa Mahakamani na kufunguliwa kesi
za mauaji na 46 kwa makosa ya kujeruhi. Watuhumiwa 13 kati hao wamehukumiwa
kunyongwa hadi kufa, mtuhumiwa mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kosa
la kujeruhi na watuhumiwa 73 wameachiwa huru na Mahakama baada ya kukosekana
kwa ushahidi. Watuhumiwa sita hawajakamatwa na upelelezi wa kesi 10 bado unaendelea.
Aidha, watuhumiwa wawili waliuawa na wananchi kabla ya kufikishwa Polisi.
13.
Mheshimiwa Spika, chanzo kikubwa cha
mauaji hayo ni imani za kishirikina kwa tamaa za kupata utajiri au cheo. Mimi siamini kwamba cheo, wadhifa, mali au
utajiri hupatikana kwa njia haramu kama hizo. Utajiri hupatikana kwa kufanya
kazi kwa juhudi na maarifa na siyo vinginevyo. Serikali itaendelea kupambana na
watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa nguvu zake zote. Naomba ushirikiano wa
Wananchi na Viongozi wa Dini zote, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wote
wa Maendeleo katika vita hivi. Aidha, niwaombe watu wote wenye mapenzi mema na
nchi yetu kutoa taarifa zinazohusu vitendo hivyo kwa vyombo vya Dola ili
kusaidia kubaini wahusika wote wa vitendo hivyo. Niwaombe Viongozi wa Madhehebu
ya Dini kuendelea kuhubiri na kuelimisha jamii kuondokana na imani potofu za
kishirikina. Ninaamini tukiunganisha nguvu zetu dhidi ya ukatili huo
tutashinda.
Ajali za Barabarani
14.
Mheshimiwa Spika, ajali za barabarani
zimeendelea kuongezeka nchini na kusababisha vifo, majeruhi, ulemavu wa kudumu
pamoja na upotevu na uharibifu wa mali za wananchi. Hivi karibuni tumeshuhudia
mfululizo wa ajali ambazo zingeweza kuzuilika. Ajali
nyingi kati ya hizo zimesababishwa na uzembe wa madereva kutozingatia Sheria za
Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na mwendo kasi, ulevi, ubovu wa magari na
pia kuendesha magari bila kujali watumiaji wengine wa barabara. Kuanzia mwezi Julai,
2014 hadi Machi 2015, kulikuwa na matukio 8,072 ya ajali za barabarani ambayo
yalisababisha vifo vya watu 2,883 na majeruhi 9,370. Hali hiyo siyo nzuri na
haiwezi kuachwa kuendelea bila kuchukuliwa hatua madhubuti. Jeshi la Polisi na
vyombo vingine vya Dola vinafanya utafiti wa kina kuhusu ajali hizo. Matokeo ya
utafiti huo yataiwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki. Vilevile, Serikali
inaendelea kutoa elimu kuhusu usalama barabarani. Nawasihi madereva wote na
watumiaji wengine wa barabara kuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani
ili kuiepusha nchi yetu na janga hili kubwa la ajali. Aidha, natoa wito kwa Wananchi
kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za madereva wanaokiuka Sheria za
Usalama Barabarani kupitia namba za simu zilizotolewa na Jeshi hilo.
SHUGHULI ZA BUNGE, TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI, MUUNGANO, MABADILIKO YA KATIBA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Bunge
15.
Mheshimiwa Spika, Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania limeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya Kutunga
Sheria pamoja na Kuisimamia na Kuishauri Serikali. Aidha, Bunge linatekeleza
Mpango Mkakati wa Muda wa Kati unaolenga kujenga uwezo wa Wabunge na Watumishi
wake. Katika mwaka 2014/2015, Bunge limefanya mikutano minne ambapo Miswada ya
Sheria 24 ilipokelewa na kujadiliwa. Kati ya hiyo, Miswada ya Sheria 17 ilisomwa
kwa hatua zake zote na kupitishwa kuwa Sheria za Nchi, na miswada saba ilisomwa
kwa mara ya kwanza. Aidha, Maazimio mawili yaliridhiwa na Kauli saba za
Mawaziri ziliwasilishwa. Vilevile, maswali ya kawaida 536 ya Waheshimiwa
Wabunge yaliulizwa na kujibiwa na Serikali pamoja na Maswali ya Msingi 39 ya
Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Pia, Kamati za Kudumu za Bunge zimetekeleza
shughuli zake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutembelea na kukagua Miradi ya
Maendeleo.
16.
Mheshimiwa Spika, baada ya Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba, 2015 tutapata Bunge jipya la 11. Ni imani yangu kuwa litakuwa Bunge imara na litakaloendeleza mazuri yote
yaliyofanywa na Bunge hili ambalo muda wake utamalizika katika kipindi kifupi
kijacho. Ninawatakia kila la kheri wale wote wanaojipanga kugombea nafasi za
ubunge katika majimbo yao ili warudi tena humu ndani baada ya Uchaguzi Mkuu.
Ofisi ya Bunge itafanya maandalizi yote muhimu ya kulipokea Bunge jipya kwa
kuboresha miundombinu ya Ofisi na pia kuimarisha huduma za utafiti, maktaba na
sheria ili Bunge lifanye kazi zake kikamilifu.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
17.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 pamoja na maandalizi
ya kupiga Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa. Maandalizi hayo yanahusisha
zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa Kisasa
unaojulikana kama Biometric Voters
Registration (BVR). Uzinduzi rasmi wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura kwa kutumia BVR ulifanyika katika Mji wa Makambako Mkoani Njombe,
tarehe 23 Februari, 2015.
18.
Mheshimiwa Spika, uboreshaji huo utahusisha kuandikisha wananchi wote wenye sifa za
kuandikishwa kuwa wapiga kura. Wananchi hao ni pamoja na wale wenye
vitambulisho vya mpiga kura na watu wote watakaokuwa wamefikisha umri wa miaka
18 wakati wa Uchaguzi Mkuu. Mfumo huo utaiwezesha Tume kuwa na taarifa sahihi
za mpiga kura na kuondoa uwezekano wa mtu kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Utaratibu huo wa uandikishaji utaondoa malalamiko kutoka kwa wadau wa uchaguzi
kuhusu udanganyifu katika upigaji kura.
19.
Mheshimiwa Spika, napenda kulikumbusha Bunge lako Tukufu na Wananchi wote kwamba, Tanzania itatumia Mfumo wa BVR kwa
ajili ya uandikishaji tu na hautatumika kwa ajili ya kupiga au kuhesabu kura
kama wengine wanavyoamini. Wale wote
wenye sifa watapiga kura kwa utaratibu wa kawaida wa kutumia karatasi maalum na
matokeo yatatolewa na kubandikwa vituoni kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye
Chaguzi zilizopita. Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaendelea kutoa elimu, taarifa na
ratiba kwa Umma kuhusu zoezi la uandikishaji linavyofanyika katika maeneo yote
nchini.
20.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2015/2016, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
itaendelea na zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kutoa elimu
ya Mpiga Kura, kusimamia na kuendesha zoezi la
Kura ya Maoni kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa na kufanikisha
Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2015. Natoa wito kwa Wananchi
wote wenye sifa kujiandikisha ili waweze kupiga Kura ya Maoni juu ya Katiba
Inayopendekezwa na kuchagua Viongozi wao ifikapo Oktoba, 2015.
Muungano
21.
Mheshimiwa Spika, Muungano wetu
umedumu kwa zaidi ya nusu karne. Katika kipindi hicho tumepata mafanikio
makubwa na ya kujivunia. Hii imetokana na misingi imara iliyowekwa na Waasisi
wa Taifa letu pamoja na utamaduni wetu wa kujadiliana na kutatua changamoto
kila zinapojitokeza. Kinachotia moyo ni kwamba, hata wakati wa mchakato wa
kuandaa Katiba Mpya, mjadala ulijikita kwenye aina ya Muungano tunaoutaka na
siyo kuwepo au kutokuwepo kwa Muungano. Hii inadhihirisha kuwa Muungano ni
jambo muhimu na unakubalika na Watanzania wa pande zote mbili. Hivyo, tuna kila
sababu ya kuulinda na kuudumisha Muungano wetu na kujivunia Utaifa
tuliouanzisha sisi wenyewe.
22.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu
ya Nne, kupitia Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT)
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imeendelea
kushughulikia hoja za Muungano. Kupitia Kamati hiyo, jumla
ya hoja 15 zilipokelewa na kujadiliwa ambapo hoja tisa (9) zilipatiwa ufumbuzi
na hoja sita (6) zipo katika hatua za utatuzi. Hoja zilizo kwenye hatua za
utatuzi ni pamoja na Mgawanyo wa mapato ambao unajumuisha suala la mgawo wa
misaada kutoka nchi za nje, misamaha ya mikopo, hisa za SMZ zilizokuwa katika
Bodi ya Sarafu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu. Hoja
nyingine ni Utafutaji na Uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; Ushiriki wa Zanzibar katika Taasisi za Nje; Ajira ya
watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano;
Usajili wa vyombo vya moto na Tume ya
Pamoja ya Fedha. Ni dhamira ya Serikali zetu mbili kuzipatia ufumbuzi hoja hizo
haraka inavyowezekana.
23.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Serikali itaanza utekelezaji wa utaratibu wa muda (interim) wa
mgao wa ajira kwa Taasisi za Muungano. Aidha, itaendelea kuratibu Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ vya
kushughulikia masuala ya Muungano; kuratibu masuala ya kiuchumi, kijamii,
kisheria na mambo yanayohusiana na Katiba kwa faida ya pande mbili za Muungano.
Pia, juhudi zitaendelezwa katika kutoa elimu kwa Umma na kuratibu masuala
yasiyo ya Muungano kwa kuhakikisha kwamba Sekta, Wizara na Asasi zisizo za
Muungano zinakutana angalau mara nne kwa mwaka.
Mabadiliko ya Katiba
24.
Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba 2011
mchakato wa kuandaa Katiba Mpya ulianza baada ya Bunge lako Tukufu kupitisha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 8 ya Mwaka 2011. Sheria hiyo iliwezesha
kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa na Wajumbe 32 kutoka pande
mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwakilisha Makundi mbalimbali
katika jamii. Tume hiyo ilifanya kazi iliyowezesha kupatikana kwa Rasimu ya
Katiba Mpya na Bunge Maalum la Katiba lilijadili na kuandaa Katiba
Inayopendekezwa.
25.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Katiba Inayopendekezwa itatakiwa kupigiwa Kura
ya Maoni ili kupata ridhaa ya wananchi. Katika kufanikisha zoezi hilo, Serikali
imechapisha Katiba Inayopendekezwa kwenye Gazeti la Serikali na pia imechapisha
na kusambaza jumla ya nakala milioni mbili za Katiba hiyo
kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuisoma na kuielewa vizuri. Ili wananchi wengi zaidi wapate fursa
ya kuisoma Katiba hiyo, vilevile, Serikali imechapishwa kwenye magazeti ya kawaida
na pia imewekwa katika tovuti mbalimbali za Serikali kwa wale ambao wanatumia
mitandao. Ili kuwezesha Watanzania wenye mahitaji maalum ya kusoma, Serikali
ilichapisha nakala 400 za Katiba Inayopendekezwa kwa watu
wa aina hiyo. Pia, nakala za Katiba Inayopendekezwa zenye maandishi makubwa
zimeandaliwa kwa ajili ya watu wenye uoni hafifu. Serikali inaendelea
kuelimisha umma kupitia Vyombo vya Habari kuhusu Katiba Inayopendekezwa na
umuhimu wa kuipigia kura.
26.
Mheshimiwa Spika, upigaji wa kura ya
maoni kwa Katiba Inayopendekezwa utafanyika baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kukamilisha zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Natoa wito kwa Watanzania wote waisome Katiba
Inayopendekezwa kwa makini na kuielewa vizuri ili waweze kufanya uamuzi sahihi
wakati wa kuipigia kura. Nawasihi wananchi wote waliojiandikisha kutumia haki
yao ya msingi na ya kikatiba kupiga kura bila kulazimishwa na mtu yeyote au
kikundi chochote.
Vitambulisho Vya Taifa
27.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/2012,
Serikali ilianza zoezi la usajili na utambuzi wa raia wa Tanzania na wageni
waishio nchini kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Awamu ya Kwanza ilihusisha uandikishaji wa
watumishi wa umma pamoja wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro,
Lindi na Mtwara ambapo hadi Aprili, 2015 zaidi ya watu Milioni Tano
wameandikishwa Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar, watu 600,000
wameandikishwa. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea na zoezi la
uandikishaji katika Mikoa iliyobaki, kujenga kituo cha kutunza kumbukumbu pamoja na kujenga Ofisi 13 za Usajili za
Wilaya Tanzania Bara na Zanzibar.
MASUALA YA UCHUMI
Hali ya Uchumi
28.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014,
uchumi ulikua kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.7 mwaka
2006, ukuaji ambao ni mzuri ikilinganishwa na nchi nyingi zinazoendelea. Kutokana
na ukuaji huo, Pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka Shilingi 360,865
mwaka 2005 hadi Shilingi 1,725,290 mwaka 2014.
Aidha, kwa mujibu wa Utafiti wa Mapato na Matumizi katika Kaya uliofanyika
mwaka 2012, umaskini wa kipato umepungua kutoka
wastani wa asilimia 34.4 mwaka 2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2012, sawa
na asilimia 6.2.
29.
Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa Bei
umepungua kutoka asilimia 6.1 Machi 2014 hadi asilimia 4.3 Machi 2015. Kupungua
kwa Mfumuko wa Bei kumetokana na sera nzuri za fedha, kuimarika kwa upatikanaji
wa chakula, pamoja na kushuka kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia. Serikali
inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta za kipaumbele kukua kwa
kushirikisha Sekta Binafsi. Sekta hizo ni pamoja na kilimo, mifugo na uvuvi.
Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
30.
Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ya CCM
ni kuifanya Tanzania kuwa Nchi yenye hadhi ya Kipato cha Kati ifikapo mwaka
2025 kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Ili
kuhakikisha kuwa lengo hilo linafikiwa, Serikali iliandaa Mpango wa Maendeleo
wa Miaka Kumi na Tano (2011 - 2026) ambao unatekelezwa kwa vipindi vya Miaka
Mitano Mitano. Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano ulianza kutekelezwa mwaka
2011/2012 na utamalizika mwaka 2015/2016. Ili kuharakisha utekelezaji wa Mpango
huo, Serikali imeainisha miradi michache ya kipaumbele yenye uwezo wa kutoa
matokeo makubwa kwa kipindi kifupi. Utekelezaji wa miradi hiyo unafanywa chini
ya mfumo ujulikanao kama “Tekeleza Sasa kwa
Matokeo Makubwa” (Big Results Now – BRN!). Miradi
katika maeneo ya kipaumbele ya Elimu, Maji, Uchukuzi, Kilimo, Nishati na Gesi Asilia,
Kuongeza Mapato ya Serikali imeanza kutekelezwa chini ya
utaratibu huo. Aidha, Serikali imeongeza eneo la Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara
na Uwekezaji katika BRN! Vilevile, uimarishaji wa
upatikanaji wa huduma za afya ni eneo lingine ambalo litashughulikiwa kwa
utaratibu wa BRN!
31.
Mheshimiwa Spika, lengo la Mfumo wa
Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa ni kuhakikisha kuwa vipaumbele vya Kitaifa
vyenye uwezo wa kuharakisha maendeleo vinatekelezwa kwa kasi na kuleta matokeo
makubwa haraka. Katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji wa Mfumo huo
kuanzia Mwaka 2013/2014 hadi 2014/2015 mafanikio makubwa yamepatikana.
Katika Sekta ya Elimu utekelezaji wa miradi na
malengo yaliyokusudiwa ulifikia asilimia
81; Maji asilimia 80, Nishati asilimia 79, Kilimo asilimia 77, Uchukuzi asilimia
64, na Utafutaji Rasilimali Fedha asilimia 54. Mawaziri wa Sekta watatoa
ufafanuzi wa utekelezaji katika maeneo hayo watakapowasilisha Hotuba za Bajeti
za Wizara husika katika Mkutano huu wa Bunge la Bajeti.
Maendeleo ya Sekta Binafsi
32.
Mheshimiwa Spika, Sekta Binafsi ni moja ya nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa soko. Kwa
kutambua umuhimu huo, Serikali imetekeleza Programu na Miradi mbalimbali kwa lengo la kukuza
ushindani wa Sekta Binafsi nchini. Programu hizo ni pamoja na Mpango wa
Kuboresha Mazingira ya Biashara
na Uwekezaji, Mradi wa Kukuza Ushindani wa Sekta Binafsi na Mpango wa Kuimarisha Mashauriano na Majadiliano
baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
Programu hizo zinatekelezwa kwa
kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ili kuongeza ushiriki
wa Sekta Binafsi katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa mikakati na kupata
ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta
hiyo. Dhamira ya Serikali ni kuijengea Sekta Binafsi uwezo wa kuwa mhimili wa
ukuaji wa uchumi na kuongeza ushindani wake katika kuzalisha mali na kufanya
biashara kwa ufanisi. Pia, Serikali imeendelea kufanya majadiliano na Sekta
Binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara katika ngazi za Taifa, Mikoa na
Wilaya. Kwa kutumia utaratibu huo wa majadiliano, Serikali kwa kushirikiana na
wadau wengine hujadili masuala ya Kisera na Kisheria yanayoathiri uendeshaji wa
Sekta Binafsi na kutolewa mapendekezo kwa ajili ya maboresho.
33.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa
mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa programu hizo ni pamoja na
kuanzisha Vituo vya Utoaji wa Huduma kwa Pamoja Mipakani. Kuanzishwa kwa Vituo
hivyo kumewezesha huduma za kiforodha, uhamiaji, udhibiti wa ubora, viwango na
usalama kupatikana katika kituo kimoja (one
stop centre). Utaratibu huo ni tofauti na ule wa awali ambapo kila Taasisi
ilikuwa inatoa huduma katika Kituo chake. Vilevile, kwa sasa huduma hizo
hutolewa upande mmoja tu wa mpaka badala ya utaratibu wa awali
ambapo huduma hizo zilifanyika katika pande zote mbili za mpaka. Hatua hizo
zimeongeza ufanisi katika uingizaji na utoaji wa mizigo mipakani na kuongeza kiwango
cha biashara baina ya nchi
jirani. Hii ni pamoja na muda wa kukamilisha taratibu
za kiforodha kuwa mfupi ikilinganishwa na hapo awali.
34.
Mheshimiwa Spika, ili Sekta Binafsi iweze kushamiri, ufanisi katika upatikanaji wa huduma
za kifedha ni muhimu. Serikali imeimarisha usimamizi wa Sekta ya Fedha pamoja
na kuongeza fursa za upatikanaji wa huduma za kifedha Mijini na Vijijini. Idadi
ya Benki na Taasisi za Fedha zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka 32 mwaka 2005 hadi
58 mwaka 2015 zikiwa na matawi 660 nchi nzima. Vilevile, upatikanaji wa huduma
za kifedha kupitia simu za kiganjani na Huduma za Uwakala wa Benki umekua kwa
kiwango kikubwa. Kwa mfano, kuanzia
mwezi Julai, 2013 hadi Aprili 2014, jumla ya miamala Milioni 972.6 yenye
thamani Shilingi Trilioni 28.3 ilifanyika kupitia mawasiliano ya simu za
kiganjani. Hali hiyo imechangia kuweka mazingira wezeshi ya biashara, hususan
biashara ndogo na za kati. Aidha, huduma hizo zimesogezwa karibu zaidi na Wananchi
na hivyo kuongeza ufanisi. Hii ni pamoja na kutumia muda mfupi na haraka katika
kupata huduma hizo na pia kuzifikisha kwa Wananchi wengi hasa Vijijini.
Uwekezaji
35.
Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada za Serikali za kuweka mazingira wezeshi ya
uwekezaji, kati ya mwaka 2005 na 2014, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili Miradi
7,159 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 74,274 na kutoa ajira
869,635. Katika mwaka
2014, Kituo cha Uwekezaji kilisajili
miradi 698 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 11,871.6. Kati ya miradi
hiyo, miradi ya wawekezaji wa ndani ilikuwa 328, miradi ya wawekezaji wa nje
211 na miradi ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje ilikuwa 159. Kati
ya miradi hiyo, miradi 33 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 214.11
ilikuwa ya kilimo na ilitoa ajira 13,373. Miradi 109 yenye thamani ya Dola za
Marekani Milioni 294.72 ilikuwa ya Sekta ya Utalii na ilitoa ajira 5,436. Ili
kuvutia uwekezaji zaidi katika Sekta ya Kilimo, Serikali inakamilisha Sera
mahsusi itakayohusu uwekezaji katika Sekta ya Kilimo.
36.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuihamasisha Sekta Binafsi kushiriki kikamilifu
katika utekelezaji wa Miradi ya Ubia. Ili kufikia azma hiyo, mwezi Novemba
2014, Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ilifanyiwa
marekebisho ili kurahisisha upatikanaji wa miradi husika. Kutokana na hatua
hiyo, Vitengo vya Uratibu na Fedha vimeunganishwa na kuunda Kituo kimoja kwa
ajili ya kuratibu utekelezaji wa miradi itakayotekelezwa kwa Ubia na Sekta Binafsi.
Vilevile, Mfuko wa Kuwezesha Maandalizi ya Miradi ya Ubia umeanzishwa, na pia
Sheria hiyo itaweka utaratibu mzuri wa usimamizi wa masuala ya ununuzi katika
miradi ya ubia ili kuongeza ufanisi.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
37.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza
Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 kwa kuwahamasisha
wananchi kubaini fursa kwa ajili ya kuleta maendeleo yao na hivyo kuchangia
katika ukuaji wa uchumi. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, juhudi kubwa
zilielekezwa kuwajengea uwezo wajasiriamali kubuni, kuanzisha na kuendesha
miradi yao ya maendeleo na kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia
Programu mbalimbali. Kwa mfano, kupitia Mpango wa
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira ulioanzishwa mwaka 2006/2007,
mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 50.6 ilitolewa kwa
Wajasiriamali 74,790. Mikopo hiyo ni endelevu kwa vile kiasi kinachorejeshwa
hutolewa tena kama mikopo kwa Wajasiriamali wengine. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Fedha na Mifuko ya
Hifadhi za Jamii imewawezesha Wananchi 256,602 kupata mikopo yenye jumla ya Shilingi Bilioni 105.
Mikopo hiyo ilitolewa kupitia SACCOS, vikundi na watu binafsi na hivyo
kuwanufaisha Watanzania wengi. Pia, Serikali kwa kushirikiana na Wadau imewezesha
uanzishwaji wa takribani vikundi vya VICOBA 23,000 vyenye Wanachama 700,000 na
mtaji wa Shilingi Bilioni 86.
38.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali
imetoa mafunzo ya Ujasiriamali kwa Wanachama wa SACCOS na vikundi vingine vya
kijamii wapatao Milioni 1.6. Kati ya hao, Wanawake ni asilimia 53 na Wanaume ni
asilimia 47. Vilevile, Serikali
imeanzisha Mafunzo ya Ujasiriamali kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu ili kuwawezesha
kujiajiri wenyewe kwa kutumia fursa zilizopo. Kutokana na uzoefu uliopatikana
katika utekelezaji wa programu za uwezeshaji Wananchi kiuchumi, Serikali kwa
kushirikiana na Wadau wengine imeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Ufundishaji
Ujasiriamali. Mwongozo huo utasaidia kutoa Mafunzo ya Ujasiriamali kuanzia Shule
za Msingi hadi Vyuo Vikuu kwa lengo la kuwafikia Wananchi wengi zaidi.
39.
Mheshimiwa Spika, kwa
kuzingatia kwamba dhana ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni pana na utekelezaji
wake unahusisha Wadau wengi, Serikali imeandaa Mpango Jumuishi wa Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (National
Multi-Sectoral Economic Empowerment Framework). Mpango huo umeainisha majukumu ya Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi yanayopaswa kutekelezwa na Wadau katika Sekta
mbalimbali. Serikali inaendelea
kuwahimiza Wadau wote ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara na Taasisi za Serikali,
Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini na Taasisi za Sekta Binafsi kujumuisha
suala la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwenye Mipango na Bajeti zao za kila
mwaka ili tufikie malengo yetu ya kuwafikia Wananchi wengi zaidi.
40.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kuwahamasisha Wananchi kuanzisha na
kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali, Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa
(SACCOS, Benki za jamiii Vijijini (VICOBA) na vikundi vingine vya kiuchumi ili
kwa umoja wao waweze kukopesheka na kuongeza nguvu zao za kiuchumi. Vilevile, Serikali itaendeleza Program za
kijasiriamali kwa Vijana nchini.
AJIRA KWA VIJANA
41.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa
ajira bado ni changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi nchini. Kwa mujibu wa Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya Vijana nchini ni
Milioni 16.2, sawa
na asilimia 35.1 ya Watanzania wote. Takwimu hizo zinabainisha
kuwa, Vijana walioajiriwa katika Sekta
ya Umma ni 188,087, walioajiriwa katika Sekta Binafsi ni Milioni 1.03. Hivyo, sehemu
kubwa ya vijana takribani Milioni 15 wamejiajiri katika shughuli za kilimo,
mifugo, uvuvi na biashara ndogo ndogo. Hata hivyo, Vijana wengi wanakabiliwa na
changamoto ya tija ndogo kwenye uzalishaji na biashara kutokana na matumizi ya
teknolojia duni, ukosefu wa mitaji na elimu ya ujasiriamali. Ili kukabiliana na
changamoto hizo, Serikali imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriamali na mikopo kwa
vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mifuko mingine ili kuwawezesha
kuanzisha au kupanua miradi yao ya uzalishaji mali. Kupitia Mfuko
wa Maendeleo ya Vijana, Serikali imetoa mikopo ya masharti
nafuu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.8 kwa SACCOS 244
na Vikundi vya Vijana 667. Aidha, jumla
ya Vijana 20,626 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za maisha.
42.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu
wa vijana ambao ni kundi kubwa la nguvu kazi kwa nchi yetu, Serikali itaimarisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kutoa ajira
ili fedha za mfuko huo zilenge zaidi katika kuwawezesha kiuchumi Vijana wasomi
na Vijana wengineo walio tayari kujituma na kujiajiri wenyewe kwa kutumia elimu
na vipaji vyao.
Serikali inakamilisha mapitio ya Sera ya Taasisi Ndogo za Fedha ili kurahisisha
upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali wadogo. Natoa wito kwa Vijana kujiunga
katika vikundi vya ujasiriamali na kutumia fursa hiyo ili waweze kupata mikopo
na kuweza kujiajiri.
UZALISHAJI MALI
43.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za
kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo, yanayolenga kuongeza tija na uzalishaji
wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula, Serikali ya Awamu ya Nne imeandaa upya
Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013. Aidha, imetekeleza azma ya KILIMO KWANZA kupitia
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo; Programu ya Kuendeleza Umwagiliaji;
Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya pamoja na Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika na pia BRN! Kupitia Mipango na Programu hizo, Serikali
imeongeza
upatikanaji
na usambazaji wa mbolea kutoka tani 241,753 mwaka 2005/2006 hadi tani 343,687
mwaka 2013/2014, sawa na ongezeko la asilimia 42.2. Aidha, Serikali kwa
kushirikiana na Sekta Binafsi imeongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima
kutoka tani 10,477 za mwaka 2005/2006 hadi kufikia tani 32,340 mwaka 2013/2014,
ikiwa ni sawa na asilimia 208.7 ya mahitaji.
44.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa Mpango wa ruzuku ya mbolea na
mbegu bora, wakulima walionufaika kwa utaratibu wa vocha wameongezeka kutoka takribani
Kaya 737,000 mwaka 2008/2009 hadi Kaya Milioni 2.5 mwaka 2013/2014. Mfumo huo
wa ruzuku ya pembejeo umewezesha wakulima kuongeza tija katika
uzalishaji wa mahindi
kutoka wastani wa gunia 5
hadi gunia 15
kwa ekari moja; na uzalishaji wa mpunga kutoka wastani wa gunia 4 hadi gunia 20
kwa ekari moja.
Matumizi ya Zana Bora za Kilimo
45.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua
umuhimu wa zana bora za kilimo katika kuongeza eneo la uzalishaji na
kumpunguzia mkulima harubu ya jembe la mkono, Serikali ilianzisha mpango wa
kukopesha matrekta kwa wakulima wadogo kwa masharti nafuu. Kutokana na
utekelezaji wa mipango hiyo na uhamasishaji wa Sekta Binafsi kuingiza Matrekta
nchini, matrekta makubwa yameongezeka kutoka 6,168 mwaka 2005 hadi 10,064 mwaka
2014; na matrekta ya mkono (Powertillers) kutoka 166 mwaka 2005 hadi 6,348 mwaka
2014. Kuongezeka
kwa zana hizo kumechangiwa na uamuzi wa Serikali wa kuingiza nchini matrekta na
kuyakopesha kwa wakulima kwa bei nafuu katika Vyama vya Ushirika na Vikundi vya
Wakulima.
Huduma za Ugani
46.
Mheshimiwa Spika, ili kuwawezesha wakulima
kupata teknolojia za kisasa
zitakazowawezesha kuongeza tija katika kilimo, Serikali imeongeza idadi ya
maafisa ugani wa kilimo kutoka 3,379 mwaka 2006/2007 hadi 9,778 mwaka
2013/2014, sawa na ongezeko la asilimia 189. Aidha, ili kuongeza mbinu shirikishi
katika huduma za ugani, Mwongozo wa Kuanzisha na Kuendesha Mashamba Darasa kwenye
Halmashauri zote nchini umeandaliwa. Mashamba Darasa yameongezeka kutoka 1,965
yenye Wakulima 51,623 mwaka 2006 hadi Mashamba Darasa 16,512 yenye jumla ya Wakulima
345,106 mwaka 2014.
47.
Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi za Serikali za kuongeza mbolea, mbegu
bora, zana bora za kilimo na huduma za ugani, uzalishaji wa mazao
nchini hususan ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 9.66 mwaka 2005/2006
hadi tani milioni 16.01 mwaka 2013/2014, sawa na ongezeko la asilimia 66.4. Ongezeko
hilo, limeliwezesha Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 125
mwaka 2014 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 95 mwaka 2005.
Hifadhi ya Taifa ya Chakula
48.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(National Food Reserve Agency - NFRA) umeongezewa uwezo wa kuhifadhi chakula
kutoka tani 241,000 mwaka 2004/2005 hadi tani 246,000 mwaka 2014/2015 ili
kuiwezesha Serikali kukabiliana ipasavyo na upungufu wa chakula wakati wa njaa
na majanga. Kutokana na uzalishaji mkubwa wa chakula katika msimu wa 2013/2014,
kuanzia mwezi Julai 2014, Serikali ililazimika kununua tani 304,514 za nafaka
zikiwemo tani 295,900 za
mahindi, tani 4,674 za mtama; na tani 3,940 za mpunga ili kuokoa mazao hayo
yasiharibike na wakulima kupata hasara. Hadi kufikia mwezi Machi 2015, NFRA ilikuwa
na tani 494,007 zilizokuwa zimehifadhiwa katika maghala yake na kiasi kingine kuhifadhiwa katika Maghala
ya watu binafsi.
49.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo itabakia kuwa ya muhimu sana katika
nchi yetu kwa miaka mingi ijayo kwani ndiyo inayotegemewa na Watanzania
wengi kwa ajili ya chakula na kipato.
Juhudi zaidi zitawekwa katika kuikuza na kuendeleza Sekta hiyo hususan, kuwawezesha
wakulima wadogo ili kilimo kiwe cha tija zaidi na kuongeza pato lao. Huu ndiyo
Mwelekeo wa Sera za Chama cha Mapinduzi katika miaka ya 2010 hadi 2020 ambazo
zitaendelea kutekelezwa katika mwaka 2015/2016. Pamoja na kuwawezesha wakulima kupata zana bora za kilimo kwa gharama nafuu na
kuwaunganisha na masoko, Serikali itaendelea na ujenzi wa maghala yenye uwezo
wa tani 5,000 Wilaya ya Mbozi na tani 10,000 Songea Mjini. Aidha, Serikali
itaanza ujenzi wa vihenge vya kisasa (silos)
vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 160,000 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mpango wa SAGCOT
50.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Serikali
ilianzisha Mpango wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania – (Southern Agricultural Growth Corridor of
Tanzania - SAGCOT). Mpango huo unaohusisha ubia kati ya Sekta Binafsi na
Sekta ya Umma unalenga kuchochea uwekezaji mkubwa wa Sekta Binafsi kwa
kushirikisha wakulima wadogo ili kubadili kilimo na kukifanya kuwa cha kisasa,
chenye tija na cha kibiashara kwa kutumia mitaji, teknolojia na ubunifu. Ili
kutekeleza azma hiyo, Kituo Maalum kinachoratibu uwekezaji wa kilimo katika
eneo hilo kijulikanacho kama SAGCOT
Centre kimeanzishwa. Kituo hicho kimekuwa chachu ya kuvutia uwekezaji
kwenye kilimo katika ukanda huo na kuhamasisha wakulima wadogo kushiriki
kikamilifu katika uwekezaji huo. Uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Mpango
huo unaonesha kwamba, pale ambapo wakulima wadogo wameshirikishwa kikamilifu
katika utekelezaji, tija imeongezeka kwa kiwango kikubwa kwani wakulima wadogo
hupata fursa za kupata pembejeo, huduma za ugani na masoko. Kwa mfano, uwekezaji
uliofanywa na Kampuni ya Kilombero Plantation Limited (KPL) katika uzalishaji
wa mpunga katika shamba la Mngeta, Wilayani Kilombero umewezesha wakulima
wadogo 8,000 kutoka katika Vijiji vinavyozunguka shamba hilo kuongeza
uzalishaji wa mpunga kutoka tani mbili (2) hadi tani nane (8) kwa hekta.
Wakulima hawa wadogo pia wameunganishwa na masoko na wamewezeshwa kupata
pembejeo kwa uhakika zaidi.
Uendelezaji wa Miundombinu ya Masoko
51.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya masoko
katika Mikoa na mipakani ili kukuza biashara ya ndani na kikanda. Ili
kufanikisha azma hiyo, Serikali inatekeleza Programu ya Uendelezaji Miundombinu
ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).
Kupitia Programu hiyo, Serikali imekarabati barabara za Vijijini zenye urefu wa
kilometa 555.3 kwa kiwango cha changarawe. Aidha, imejenga maghala 11 katika
Halmashauri 10 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,000 za mazao kila moja. Vilevile,
kupitia Programu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Masoko ya Mipakani, Serikali
imejenga jumla ya masoko 10 katika maeneo ya kimkakati ya mipakani. Masoko
yaliyojengwa ni pamoja na Nyamugali na Kagunga yaliyopo katika mpaka wa
Tanzania na Burundi; na Masoko ya Mkenda na Mtambaswala yaliyopo katika mpaka
wa Tanzania na Msumbiji. Nitoe wito kwa wananchi kutumia fursa za masoko hayo
kufanya biashara na nchi jirani ili kujiongezea kipato na kukuza mauzo yetu ya
nje.
52.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2015/2016, Serikali itaboresha miundombinu mbalimbali ya masoko kama vile
barabara, maghala, huduma za fedha na kuweka huduma nyingine muhimu kama umeme,
maji na ulinzi hasa katika maeneo ya masoko ya mpakani.
Maendeleo ya Sekta ya Mifugo
53.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuongeza tija katika Sekta
ya Mifugo ili wafugaji waondokane na uchungaji na kuwawezesha kufuga kisasa.
Ili kufikia lengo hilo, Serikali inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini ambayo inalenga kuboresha
uzalishaji wa mifugo bora, kupambana na magonjwa ya mifugo na kuimarisha
miundombinu ya mifugo. Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imekarabati
na kujenga Majosho 847 na hivyo kuongeza idadi ya Majosho kutoka 2,177 mwaka
2006/2007 hadi 3,637 mwaka 2014/2015. Aidha, Serikali imetoa ruzuku ya dawa za
kuogesha mifugo dhidi ya magonjwa
yaenezwayo na Kupe na Mbung’o ambapo jumla ya lita milioni 1.2 za dawa zimenunuliwa.
Matumizi ya dawa hizo yamechangia kupunguza vifo vya ndama
kutoka wastani wa asilimia 40 mwaka 2006/2007 hadi chini ya asilimia 10 mwaka
2014/2015.
54.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kuweka mazingira mazuri ya
uwekezaji kwa Sekta Binafsi, viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka
viwanda 22 hadi 74 kati ya mwaka 2005 na 2014. Viwanda hivyo vimeongeza uwezo wa
usindikaji wa maziwa kwa siku kutoka lita 56,580 mwaka 2005 hadi lita 139,800
mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 147. Aidha, uzalishaji wa vyakula vya
mifugo umeongezeka kutoka tani 559,000 mwaka 2005 hadi tani 915,000 mwaka
2013/2014; na viwanda vya kuzalisha vyakula hivyo vimeongezeka kutoka viwanda sita
(6) mwaka 2005 hadi 80 mwaka 2014 vyenye uwezo wa kusindika tani milioni 1.4
kwa mwaka.
55.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imejaliwa
kuwa na mifugo mingi ambayo ikitumika vizuri inaweza kubadili maisha ya
wafugaji. Hata hivyo, tunahitaji kufanya mapinduzi makubwa katika Sekta hii ili
wafugaji wetu waweze kufuga kisasa. Kazi iliyoanza ya kuzalisha mifugo bora na
kuisambaza kwa wafugaji pamoja na kutenga maeneo maalum ya wafugaji itaendelezwa
kwa nguvu zaidi ili kuongeza tija kwenye Sekta ya Mifugo. Vilevile, uwekezaji
kwenye machinjio ya kisasa utahamasishwa ili mazao yatokanayo na mifugo yaweze
kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Sekta ya Uvuvi
56.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Kuendeleza
Sekta ya Uvuvi nchini ili kuwawezesha wavuvi kuzitumia fursa za viumbe hai
vilivyomo katika bahari, maziwa na mito kuinua hali zao za maisha. Kupitia
Programu hiyo, uzalishaji wa mazao ya uvuvi umeongezeka kutoka tani 341,109 mwaka
2006 hadi tani 375,158 mwaka 2014. Katika mwaka 2014/2015, tani 43,354 za mazao
ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 42,100 ziliuzwa nje ya nchi na kuiingizia
Serikali mapato ya Shilingi bilioni 7.5 ikilinganishwa na tani 38,574 na samaki
hai wa mapambo 44,260 zilizouzwa nje ya nchi mwaka 2013/2014 na kuiingizia
Serikali kiasi cha shilingi bilioni 6.1. Kutokana na sera nzuri za uwekezaji na
uwezeshaji, Viwanda vya Kuchakata Samaki vimeongezeka kutoka viwanda 25 hadi 48
na maghala ya kuhifadhi mazao ya uvuvi kutoka Maghala 40 hadi 84. Katika
kipindi cha mwaka 2015/2016, Serikali itaimarisha ufuatiliaji na doria ili
kudhibiti uvuvi na biashara haramu
katika mito, maziwa, bahari na maeneo ya mipakani.
Wanyamapori
57.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kuboresha miundombinu ndani ya Mapori ya Akiba, Hifadhi za
Wanyamapori, kuimarisha ulinzi na usalama wa wanyamapori pamoja na kuziwezesha jamii zinazoishi jirani na
maeneo ya hifadhi kunufaika na rasilimali
za wanyamapori. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imeanzisha
Mamlaka ya Wanyamapori ili kuimarisha uhifadhi na kukabiliana na ujangili
nchini. Ili kuendeleza juhudi za kudhibiti ujangili wa wanyamapori, Serikali kwa
kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imeongeza uwezo wa Mamlaka za Serikali kwa
kuwapatia vifaa vya kisasa ikiwa ni pamoja na helikopta moja, magari 35, silaha
na mitumbwi minne. Vilevile, Serikali imeajiri askari wa wanyamapori 608.
58.
Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba, 2014
Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kikanda kuhusu kukomesha ujangili.
Katika mkutano huo uliofanyika Arusha, nchi za Tanzania, Burundi, Kenya,
Malawi, Msumbiji, Sudani ya Kusini, Uganda na Zambia zilisaini Azimio la Kikanda la Kushirikiana
katika Kuhifadhi na Kudhibiti Vitendo vya Ujangili. Tanzania pia ilisaini Mkataba
wa Makubaliano ya Ushirikiano katika kuhifadhi ushoroba wa wanyamapori na nchi
za Kenya (Serengeti-Masai Mara), Msumbiji (Selous-Niassa) na Zambia (Miombo – Mapane
Woodland).
59.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kushirikiana na Wananchi kusimamia
maliasili kupitia Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori na kuweka alama za wazi
kwenye mipaka ya hifadhi za wanyamapori na ardhioevu. Tanzania kama Nchi, tunalo
jukumu kubwa la kulinda urithi mkubwa wa wanyamapori tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu
kwa nguvu zote. Jukumu hili haliwezi kuachiwa Maafisa Wanyamapori pekee,
linahitaji nguvu zetu wote na viongozi kuanzia ngazi ya Vitongoji hadi Taifa.
Tushirikiane kuwafichua majangili ili kuokoa Rasilimali hizo ambazo ni utajiri
mkubwa kwa nchi yetu.
Ufugaji Nyuki
60.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeweka msukumo mkubwa katika kuendeleza ufugaji nyuki kibiashara na kuongeza
tija katika kuzalisha Asali na Nta ili kuwawezesha wafugaji kujiongezea kipato.
Kazi kubwa iliyofanyika ni kutoa elimu na
kuhamasisha wananchi kuanzisha vikundi na miradi ya ufugaji nyuki. Mwezi
Novemba 2014, Serikali iliandaa Maonesho Maalum ya Asali ambayo yaliambatana na
Kongamano la Kimataifa la Ufugaji Nyuki kwa lengo la kujadili maendeleo ya Sekta
ya Ufugaji Nyuki nchini. Pia, Serikali imeadhimisha mwaka wa tatu wa Siku Maalum ya Kitaifa
ya Kutundika Mizinga iliyofanyika Wilayani Handeni, tarehe 25 Machi, 2015. Siku
hii huadhimishwa Kitaifa, Kimkoa na Kiwilaya ili kuhamasisha Wananchi kuanzisha
ufugaji nyuki katika maeneo yao kwa lengo la kuwapatia kipato kwa njia ambayo
ni rafiki kwa mazingira.
61.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imetoa mafunzo kuhusu mbinu mpya za ufugaji nyuki, matumizi ya mizinga ya
kisasa, utundikaji wa mizinga na usimamizi wa manzuki kwa Wananchi 7,320 katika
Vikundi 921 vya wafugaji nyuki kutoka Vijiji 242 kwenye Wilaya 30. Vilevile, Serikali
imegawa Mizinga ya kisasa 14,076 kwa Wananchi na vituo kumi (10) vya ukusunyaji
asali vimeanzishwa katika Wilaya tano. Katika mwaka 2015/2016, Serikali
itaendelea kutoa elimu ya ufugaji nyuki, kuboresha mifumo ya kukusanya
maduhuli, kujenga maabara ya ufugaji nyuki na kuhimiza kuanzisha Chama Kikuu cha
Ushirika cha Ufugaji Nyuki.
Utalii
62.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imefanya juhudi kubwa za kutangaza vivutio vya Utalii Nchini, kuboresha huduma
za kitalii hususan hoteli, miundombinu
na mawasiliano na kushiriki maonesho ya kimataifa. Vilevile, Serikali imefanikiwa kuyashawishi Mashirika ya Ndege ya Qatar Airways, Fly Dubai na Turkish Airlines kuongeza idadi ya
safari zao nchini Tanzania. Juhudi hizo zimesaidia
kuwashawishi watalii wengi zaidi kuitembelea Tanzania. Idadi ya watalii wa nje imeongezeka kutoka 1,095,884 mwaka 2013 hadi watalii
1,102,026 mwaka 2014/2015. Mapato
yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1,853 mwaka
2013 hadi Dola za Marekani 1,983 mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia saba
(7).
63.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya
Utalii ndiyo inayoongoza sasa kuliingizia Taifa fedha
za kigeni. Hivyo, juhudi kubwa zinafanyika kuongeza kasi
ya kutangaza vivutio vilivyopo na kuimarisha utoaji wa
huduma muhimu, ikiwa ni pamoja na
kufundisha watoa huduma
mbinu za kisasa
za kuhudumia watalii. Aidha, juhudi zaidi zinahitajika ili kufikia masoko mapya
na kutangaza vivutio vingine vinavyopatikana maeneo ambayo
hayajatangazwa sana. Hii ni pamoja na
kuhimiza utalii wa ndani kwa kuhamasisha wazawa kutembelea vivutio vingi
vinavyopatikana nchini kote.
Madini
64.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Madini ni
kati ya sekta muhimu zenye mchango mkubwa kiuchumi na kijamii. Katika kipindi cha miaka
kumi iliyopita, mapato yatokanayo na madini yameongezeka kila
mwaka kutokana na mchango wa uchimbaji
mkubwa na pia uchimbaji wa kati na mdogo. Katika kipindi hicho, thamani ya
madini yaliyozalishwa nchini na kuuzwa nje iliongezeka kutoka Dola za Marekani
milioni 655.5 mwaka 2005 hadi kufikia Dola za Marekani Milioni 1,794 mwezi
Desemba 2014. Ili kuwezesha Taifa kunufaika zaidi na rasilimali za madini,
Serikali imekamilisha majadiliano na Wawekezaji wa Migodi mikubwa ya Geita,
Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi ambapo Kampuni hizo zimeanza kulipa ushuru wa
huduma kwa Halmashauri za Wilaya husika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa.
Ulipaji wa ushuru huo umeongeza uwezo wa Halmashauri wa kutekeleza miradi mingi
ya maendeleo badala ya kutegemea malipo ya Dola za Marekani 200,000 kwa mwaka
kama ilivyokuwa ikifanyika awali. Vilevile, majadiliano hayo yamewezesha Migodi
yote mikubwa kulipa mrabaha wa asilimia 4 kama ilivyo kwenye Sheria ya Madini
ya Mwaka 2010.
65.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali iliendeleza juhudi za kuboresha mfumo wa utoaji leseni za
madini ikiwa ni pamoja na kujenga mfumo wa huduma za leseni kwa njia ya
mtandao. Kufuatia jitihada hizo, muda wa kushughulikia maombi mapya umepunguzwa
kutoka miezi 18 hadi kufikia miezi mitatu (3). Kuanzia mwezi Julai, 2014 hadi
Machi 2015, jumla ya leseni 3,449 zilitolewa kwa wachimbaji wa madini ya
aina mbalimbali nchini. Vilevile, Serikali imeanzisha Ofisi
mbili zaidi za Kanda ya Ziwa Nyasa (Songea) na Kanda ya Ziwa Viktoria
Mashariki (Musoma) ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Aidha, zimeanzishwa Ofisi nne
za Afisa Madini Mkazi katika Miji ya Bariadi,
Njombe, Moshi na Nachingwea. Ni imani yangu kuwa
wananchi watatumia kikamilifu huduma zinazotolewa na Maafisa wa Madini wa
maeneo hayo ili waweze kunafaika na Rasilimali za madini zilizopo nchini.
Wachimbaji Wadogo wa Madini
66.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwawezesha Wachimbaji Wadogo kuboresha shughuli
za utafutaji, uchimbaji na kuongezea thamani madini. Hatua zinazochukuliwa ni
pamoja na kutoa mafunzo kwa vitendo, kuwatengea maeneo maalum ya uchimbaji
madini na kutoa ruzuku ya zana na vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Serikali
imetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa Wachimbaji Wadogo yenye thamani ya Shilingi
Bilioni 1.4 na kutenga jumla ya kilometa za mraba 1,639 katika maeneo 22 hapa
nchini kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo wa madini. Aidha, Serikali imeanzisha
soko la Kimataifa la vito na usonara na imekarabati Kituo cha Jimolojia
Tanzania kilichopo Jijini Arusha ili kukuza tasnia ya
Uongezaji Thamani Madini Nchini badala ya madini hayo kusafirishwa
nje ya nchi yakiwa ghafi. Hatua hizo zimetoa fursa kwa Wachimbaji Wadogo na wafanyabiashara
wa nje kuanzisha uhusiano wa kibiashara.
Viwanda
67.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda ni
mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi na kichocheo kikubwa cha ukuaji wa
ajira. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Sekta ya Viwanda
imekua kwa wastani wa asilimia 7.7. Ukuaji huo umetokana na kuongezeka kwa
uzalishaji wa viwandani, hususan usindikaji wa vyakula na uzalishaji wa
vinywaji, saruji, sigara na bidhaa za chuma. Katika kipindi hicho, mchango wa Viwanda
Vidogo na vya Kati umeongezeka kwa kiwango kikubwa. Matokeo ya utafiti
uliofanywa mwaka 2012 unaonesha kuwa, Viwanda Vidogo na vya Kati na Biashara
Ndogo vinachangia asilimia 27.9 ya Pato la Taifa na vimefanikisha kuzalisha
ajira za moja kwa moja kwa Watanzania zaidi ya Milioni 5.2. Hii inathibitisha kuwa
Viwanda Vidogo na vya Kati vina mchango mkubwa katika Pato la Taifa. Serikali
itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kukuza Viwanda Vidogo na vya Kati
ikiwemo kutoa msukumo zaidi kwa Viwanda vya Kuongezea Thamani ya Mazao Ghafi
yanayozalishwa nchini.
68.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali imeanza kufanya Sensa ya Viwanda Nchini. Lengo la Sensa
hiyo ni kupata takwimu na taarifa za kina za viwanda zitakazotumiwa kubuni na
kuchukua hatua stahiki za kisera na kuandaa programu za kuendeleza Sekta ya Viwanda
Nchini. Ukusanyaji wa takwimu hizo pia utatumika kuandaa Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umelenga kuinua Sekta ya Viwanda nchini ili
kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
69.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa na
mabadiliko na mahitaji makubwa ya matumizi ya ardhi kwa watumiaji mbalimbali. Mahitaji
hayo makubwa na kutokuwepo kwa Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi tangu awali
vimesababisha kuongezeka kwa migogoro ya matumizi ya ardhi, ugomvi baina ya
watumiaji mbalimbali na uharibifu wa mazingira. Ili kudhibiti hali hiyo, mwezi
Agosti 2013, Serikali iliidhinisha Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (2013 –
2033). Mpango huo umeweka utaratibu mzuri na unaofaa wa Matumizi ya Ardhi kwa
kuainisha Programu 12 za Matumizi ya Ardhi, Usimamizi wa Uendelezaji wa Miji na
Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya na Vijiji. Utekelezaji wa Programu hizo
umewezesha Vijiji 1,560 vilivyopo katika Wilaya 92 kuandaliwa Mipango ya
Matumizi ya Ardhi nchini.
70.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali iliahidi kuanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi
Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land
Management Information System - ILMIS) ambao unalenga kuboresha utaratibu
wa upatikanaji wa Hatimiki za Ardhi na kusogeza huduma za upimaji, upangaji na
usimamizi wa ardhi karibu na wananchi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu
kwamba, kazi ya ujenzi wa Mfumo huo imeanza kwa awamu. Katika Awamu ya Kwanza,
Ofisi zote Nane za Kanda za Ardhi zitaunganishwa na Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi.
Awamu ya Pili itahusisha kufunga Mfumo huo kwenye Ofisi za Ardhi za Halmashauri
zote Nchini. Hatua hizo zitasaidia kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za ardhi,
kurahisisha utoaji wa Hatimiliki na kukadiria kodi ya pango la ardhi.
71.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendeleza
juhudi za kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi, hususan baina ya wakulima na
wafugaji na maeneo ya hifadhi kwa kuwezesha zoezi la kupanga, kupima na
kumilikisha ardhi katika Vijiji vya Halmashauri kwa awamu. Halmashauri zilizohusishwa
katika awamu ya kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Kiteto. Katika
Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, mipaka ya Vijiji vyote imepimwa ikijumuisha Vijiji
vilivyokuwa kitovu cha migogoro ya ardhi katika eneo hilo. Kazi iliyobaki ni
kwa Serikali kujiridhisha na usahihi wa upimaji huo na kutoa maelekezo stahiki
kabla ya zoezi hilo kuanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero. Aidha,
uhakiki wa mipaka katika Wilaya za Gairo, Chemba na Bagamoyo umefanyika.
Uhakiki huo ambao ulikuwa shirikishi umeondoa migogoro ya mipaka iliyokuwa
inawakabili wananchi na Watendaji katika maeneo hayo. Kazi ya kuhakiki mipaka
katika maeneo mengine itaendelezwa katika mwaka 2015/2016.
72.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kadri
idadi ya watu na shughuli za kiuchumi zinavyoongezeka, mahitaji ya ardhi nayo
yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, wakati ambapo eneo la ardhi linabaki lilelile. Hali
hiyo imesababisha kuwepo kwa migogoro baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi. Kwa
mantiki hiyo, sote tunatakiwa kutumia ardhi tuliyonayo kwa ufanisi na tija
zaidi. Serikali itaendeleza juhudi za kupima ardhi na kuweka mipango bora ya matumizi yake sambamba na kutoa elimu ya
kutumia ardhi ndogo kuzalisha kisasa zaidi. Ni muhimu watumiaji wote wa ardhi wakashirikiana
na Serikali kuweka mipango endelevu itakayohakikisha kwamba kila mmoja
ananufaika na ardhi iliyopo kwa maendeleo na ustawi wa jamii na Taifa kwa
ujumla.
Barabara, Madaraja na Vivuko
73.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya
imefanya kazi kubwa ya kuimarisha na kuboresha mtandao wa barabara na madaraja nchini. Tangu ilipoingia madarakani mwaka 2005,
Serikali ya Awamu ya Nne imekamilisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa Kilometa
1,226 zilizoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu. Aidha, jumla ya Kilometa
1,305 za barabara kuu zimejengwa upya kwa kiwango cha lami na Kilometa 960
kufanyiwa ukarabati. Vilevile, Kilometa 393 za Barabara za Mikoa zimejengwa kwa
kiwango cha lami. Hivyo, jumla ya barabara kuu na za mikoa zilizojengwa na
kukarabatiwa kwa kiwango cha lami katika kipindi hicho ni Kilometa 3,884 na Kilometa
6,636 zimekarabatiwa kwa kiwango cha changarawe.
74.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa
barabara mpya, Serikali pia imeendelea
kujenga madaraja madogo na makubwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kati ya
mwaka 2006 na
2015, Serikali
imekamilisha ujenzi wa madaraja makubwa ikiwa ni pamoja na la Mwatisi
(Morogoro), Ruvu (Pwani), Nangoo (Mtwara), Nanganga (Mtwara), Ruhekei (Ruvuma) na
Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi (Kigoma). Aidha, ujenzi wa madaraja mengine
makubwa sita ya Kigamboni, Mbutu, Maligisu, Kavuu, Kilombero na Sibiti
unaendelea.
75.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekarabati na kununua Vivuko vipya kwa ajili
ya kurahisisha usafiri wa majini nchini. Vivuko vilivyofanyiwa ukarabati ni
pamoja na MV Ukara, MV Sabasaba, MV Kome
na MV Geita vyote vya Mwanza na MV Chato (Geita). Vivuko vipya vilivyonunuliwa
ni pamoja na MV Ruvuvu (Kagera), MV
Ujenzi (Mwanza), MV Musoma (Mara), MV
Kilambo (Mtwara) na MV Malagarasi (Kigoma). Pia, Serikali imenunua Vivuko kwa ajili ya Kahunda
– Maisome (Mwanza), Msangamkuu (Mtwara) na Kivuko cha Dar es Salaam - Bagamoyo kitakachosaidia
kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
76.
Mheshimiwa Spika, kazi iliyofanywa na
Serikali ya Awamu ya Nne kwenye ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko ni kubwa
na ya kujivunia. Nchi yetu sasa imeunganishwa na mtandao wa barabara za lami
kutoka kona moja ya nchi hadi nyingine. Muda wa kusafiri na kusafirisha mizigo
nchini na nchi jirani umepungua sana. Kazi hii inahitaji kuendelezwa kwa nguvu
na kasi zaidi kwa miaka ijayo ili hatimaye mikoa na wilaya zote ziunganishwe
kwa barabara za lami. Hivyo, kazi ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa
barabara zenye urefu wa kilometa 3,419 ambazo zipo kwenye hatua za usanifu
itaendelea kufanywa na Serikali ili barabara hizo zikamilishwe.
Reli
77.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha
miundombinu ya Reli ya Kati kwa kununua vifaa mbalimbali zikiwemo injini mpya
(locomotives) 13 za treni, Mabehewa mapya 22 ya abiria, Mabehewa 150 ya mizigo,
Mabehewa 34 ya breki, Mabehewa 25 ya kubebea kokoto na Mtambo wa kunyanyulia
mabehewa. Aidha, imekarabati injini saba (7) za treni, mabehewa 82 ya mizigo na
mabehewa 31 ya abiria pamoja na kukamilisha kazi ya kujenga upya injini nane
(8) za treni katika Karakana ya Reli iliyopo Morogoro. Kazi ya upembuzi wa kina
wa ujenzi wa reli mpya ya Dar es Salaam – Isaka – Kigali/Musongati kwa kiwango
cha standard gauge ilikamilika
Aprili, 2014. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea na mpango wa
kuimarisha na kuboresha vitendea kazi na huduma katika Reli ya Kati. Aidha,
itaanzisha huduma ya block train ya
kusafirisha mizigo ya nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.
Bandari
78.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina fursa kubwa ya kuongeza mapato kutokana
na huduma za Bandari ikizingatiwa kuwa tunazungukwa na nchi sita ambazo hazina
bandari. Kwa kutambua fursa hiyo, Serikali imeimarisha bandari zake ili ziweze
kutoa huduma kwa ufanisi na tija. Kupitia Mpango wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo
Makubwa, Serikali inatekeleza miradi muhimu ambayo imesaidia kuongeza uwezo wa
bandari kuhudumia mizigo kutoka tani milioni 12 mwaka 2012 hadi tani milioni
14.6 mwaka 2014/2015. Vilevile, muda wa meli kukaa bandarini umepungua kutoka
wastani wa siku 6.3 mwaka 2012 hadi wastani wa siku 2.9 Januari, 2015. Katika
mwaka 2015/2016, Serikali itaanza ujenzi wa bandari mpya ya Mbegani Bagamoyo
itakayokuwa kubwa kuliko bandari zote katika Ukanda wa Afrika Mashariki na
Kati. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha bandari za Tanga na Mtwara na zile
za maziwa ili ziweze kutoa huduma bora kwa ufanisi zaidi.
Viwanja vya Ndege
79.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya
jitihada kubwa kuimarisha usafiri wa anga kwa kujenga, kupanua na kukarabati
viwanja vya ndege na kuweka mazingira mazuri kwa Sekta Binafsi
kutoa huduma za usafiri wa anga. Viwanja
vya ndege vya Arusha, Bukoba, Kigoma, Mafia, Mpanda, Musoma, Mwanza na Tabora vimekarabatiwa. Aidha, Kiwanja kipya
cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe, Mbeya kimejengwa na kuanza kutoa huduma
mwezi Januari 2013. Kazi ya kupanua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere kwa kujenga jengo la tatu la abiria (Terminal III) imeanza na Awamu ya Kwanza inayohusisha ujenzi wa
jengo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 3.5 kwa mwaka inatarajiwa
kukamilika Oktoba, 2015.
80.
Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa Viwanja
vya Ndege nchini kumewezesha kampuni zinazotoa huduma za usafiri wa anga ndani
na nje ya nchi kuongezeka kutoka 29 mwaka 2005 hadi 55 hivi sasa. Ongezeko hilo
limeendana na ongezeko la abiria wanaowasili na kuondoka katika Viwanja vya Ndege
nchini kutoka Abiria milioni 2.2 mwaka
2005 hadi zaidi ya Abiria milioni 4.7 hivi sasa. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la
Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere pamoja na kuendelea na ukarabati wa
Viwanja vingine vya ndege nchini.
Nishati
81.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali imekamilisha utekelezaji wa miradi ya kuimarisha
upatikanaji wa umeme kupitia Mpango wa Changamoto za Milenia katika Mikoa ya
Dodoma, Iringa, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe na Tanga. Serikali
pia, imekamilisha kwa asilimia 84 utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Kufua Umeme
wa Kinyerezi utakaozalisha Megawati 150 kwa kutumia gesi asilia. Utekelezaji wa
Awamu ya Tatu ya Mradi wa Kinyerezi utakaozalisha Megawati 300 unaendelea.
Vilevile, Serikali imesaini Mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme
kutoka Mto Rusumo utakaozalisha Megawati 80 kwa lengo la kuyapatia umeme wa
uhakika maeneo yaliyo nje ya Gridi ya Taifa,
hususan Mikoa ya Kagera na Kigoma.
82.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha miundombinu ya
uzalishaji umeme nchini kwa kiwango kikubwa na kuwezesha uzalishaji wa umeme kuongezeka
kutoka Megawati (MW) 891 mwaka 2005 hadi MW 1,226.3 Machi, 2015. Ili kuongeza
kasi ya kusambaza umeme Vijijini, Serikali ilianzisha Wakala wa Nishati
Vijijini (Rural Energy Agency - REA) Oktoba
2007. Wakala umetekeleza miradi mingi kupitia Mradi Kabambe wa Kusambaza umeme Vijijini.
Katika Awamu ya Kwanza ya utekelezaji wa mradi huo, Wilaya 17 zimeunganishiwa
huduma za umeme na kufanya Makao Makuu
ya Wilaya zilizopata umeme kufikia 120 kati ya Wilaya 133 zilizopo. Aidha,
kupitia REA, Serikali imepeleka umeme kwenye maeneo mbalimbali ya uzalishaji
mali na huduma za jamii na Vijiji 3,734. Vilevile, jumla ya Shule za Sekondari 1,845;
zahanati na Vituo vya Afya 898 na Hospitali 96 zilipatiwa umeme katika maeneo
mbalimbali ya Tanzania Bara. Awamu ya pili inaendelea kutekelezwa kwa lengo la
kufikisha umeme katika makao makuu ya Wilaya zote nchini na maeneo mengi ya
Vijijini na Mijini.
83.
Mheshimiwa Spika, sambamba na juhudi hizo, Serikali
ilichukua hatua nyingine ya kupunguza gharama za kuunganisha umeme Mijini na
Vijijini kwa kiwango kikubwa kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wa wateja waishio
Vijijini walio nje ya Mpango wa REA, gharama zilipunguzwa kutoka
Shilingi 455,108/= hadi Shilingi 177,000/= na kwa maeneo ya Mijini, gharama
zilipungua kutoka Shilingi 455,108/= hadi Shilingi 320,960/= kwa wateja wanaojengewa
njia moja (single phase) kwa umbali
usiozidi Meta 30 bila kuhitaji nguzo. Kwa miradi inayotekelezwa na Wakala wa Usambazaji Umeme
Vijijini, gharama za uunganishwaji umeme
zilipunguzwa hadi kufikia Shilingi 27,000/= tu kwa kipindi ambacho Mkandarasi
anakuwa kwenye eneo la
mradi. Jitihada hizo zimechangia
kuongeza idadi ya Wananchi wanaopata huduma za umeme nchini kutoka asilimia 13
ya Watanzania wote mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 36 mwezi Machi, 2015 na
hivyo kuvuka lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM la kufikia asilimia 30 mwaka
2015.
Gesi Asilia
84.
Mheshimiwa Spika, ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia nchini
umeiweka Tanzania katika orodha ya nchi zinazozalisha Gesi Asilia nyingi
duniani na kutoa matumaini makubwa ya kukuza uchumi wetu. Hadi kufika Desemba, 2014, Gesi Asilia yenye Futi za Ujazo Trilioni
53.28 ilikuwa imegunduliwa na kazi ya utafutaji inaendelea. Kiasi hiki ni
takriban mara tano ya Gesi Asilia iliyokuwa imegunduliwa mwaka 2005. Kutokana
na ugunduzi huo, Serikali imetunga Sera ya Gesi Asilia ya Mwaka 2013 na kuandaa
Muswada wa Sheria ya Gesi Asilia ili kuhakikisha kunakuwepo usimamizi imara wa
Sekta ya Gesi Asilia nchini, na kuwawezesha
wananchi kunufaika kikamilifu na rasilimali za Gesi Asilia.
85.
Mheshimiwa Spika, ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo, Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia lenye urefu wa Kilometa
542 kutoka Mtwara na Lindi hadi
Dar es Salaam kupitia Somanga
Fungu. Utekelezaji wa mradi huo ulioanza mwezi Julai,
2012 ulikuwa umefikia asilimia 98 mwezi Machi, 2015 na utakamilika
mwezi Julai, 2015. Vilevile, ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi
asilia katika maeneo ya Madimba Wilayani Mtwara Vijijini na Songo Songo
Wilayani Kilwa unaendelea. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaongeza uwezo wa kufua
umeme hasa unaotokana na Gesi Asilia na nishati jadidifu. Vilevile, itaongeza
kasi ya kupeleka umeme Vijijini pamoja na kupunguza kiwango cha upotevu wa
umeme katika Gridi ya Taifa. Lengo ni kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata umeme
wa uhakika.
Huduma za Mawasiliano
86.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Mawasiliano
inakua kwa kasi na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.
Idadi ya
watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu nchini imeongezeka kutoka
laini za simu za kiganjani milioni 2.9 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 32 mwezi
Desemba, 2014. Gharama za kupiga simu zimepungua katika kipindi hicho kutoka Shilingi 112
hadi Shilingi 34.9 kwa dakika. Kupungua kwa gharama hizo kumetokana na Sera na
mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowezesha kuongezeka kwa watoa huduma na
hivyo kuongeza ushindani wa kibiashara. Pamoja na mazingira hayo mazuri, uamuzi
wa Serikali kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umewezesha watoa huduma
kutumia huduma za mkongo huo badala ya kila mmoja kujenga miundombinu yake. Aidha, kumekuwa
na ongezeko la huduma nyingine kupitia mawasiliano ya simu za mkononi kama
vile, miamala ya kifedha na ununuzi wa huduma na bidhaa kwa kutumia miamala ya
kibenki. Inakadiriwa
kuwa watumiaji wapatao milioni 12.3 wanatumia huduma za miamala ya kibenki kwa
kutumia simu za kiganjani. Vilevile, watumiaji wa huduma za intaneti wameongezeka kutoka milioni 3.6 mwaka 2008 hadi watumiaji milioni 11.3
mwaka 2014.
87.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Awamu ya Kwanza na ya Pili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano wenye
urefu wa kilomita 7,560 ambao uliunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote Tanzania, baadhi
ya Makao Makuu ya Wilaya na pia kuunganisha na nchi jirani. Awamu ya Tatu ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa utaziunganisha
Wilaya zote nchini na kukamilisha uunganishaji wa maeneo ya Unguja na Pemba. Awamu
hiyo itahusisha pia ujenzi wa Kituo Mahiri cha Kutunzia Kumbukumbu katika Jiji la Dar
es Salaam, Zanzibar na Dodoma. Katika Awamu ya Nne, Serikali kwa kushirikiana
na watoa huduma za mawasiliano ambao ni Airtel, Tigo, Vodacom na Zantel,
inajenga Mikongo ya Mijini (Metro Fibre
Ring Networks), ambapo hadi mwezi Machi 2015, jumla kilomita 91 zilikuwa zimekamilika katika Jiji
la Dar es Salaam. Aidha, ujenzi wa Mikongo unaendelea katika Miji ya Arusha na Mwanza
ambapo jumla ya kilomita 94 zimejengwa. Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
utakapokamilika, utawezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa haraka
zaidi, uhakika na kwa gharama nafuu. Vilevile, utaboresha mawasiliano baina ya
Tanzania na nchi jirani pamoja na nchi nyingine duniani baada ya kuunganishwa
na Mikongo ya Kimataifa ya SEACOM, EASSy na SEAS ambayo tayari imefika hapa nchini.
88.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeingia
Makubaliano ya Ushirikiano na Kampuni ya VIETTEL (Viettel Joint Stock Company – VIETTEL) ya Vietnam kuwekeza katika
maeneo yasiyokuwa na mawasiliano vijijini. Kampuni hiyo itajenga kwa awamu
miundombinu ya Mkongo wenye urefu wa kilometa 13,000 kwa kutumia teknolojia
rahisi katika Wilaya zote nchini pamoja
na kujenga miundombinu ya mawasiliano katika vijiji 4,000 visivyokuwa na
mawasiliano. Vilevile, Kampuni hiyo itaziunganisha Ofisi za Wakuu wa Wilaya,
Hospitali za Wilaya, Ofisi za Polisi za Wilaya na Ofisi 65 za Posta katika mkongo
pamoja na kupeleka na kutoa huduma za intaneti
bila malipo katika
shule tatu za Serikali katika kila Wilaya kwa kipindi cha miaka mitatu.
Uwekezaji huo utakapokamilika utaleta mapinduzi makubwa ya mawasiliano katika
maeneo ya vijijini, jambo ambalo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo.
89.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2015/2016, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mikongo ya Mijini katika Miji ya
Morogoro, Arusha, Mwanza na Dodoma kwa kushirikiana na watoa huduma za
mawasiliano nchini. Aidha, itaanza Awamu ya Tano ya ujenzi wa Mkongo ambao utahusu
kupeleka huduma kwa watumiaji wa mwisho (last
mile connectivity) ambao ni pamoja na watu binafsi, Shule za Msingi,
Sekondari na Vituo vya Afya ili kuwawezesha kutumia fursa za TEHAMA katika
elimu mtandao, maktaba mtandao na afya mtandao.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
90.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu
ya Nne imepata mafanikio makubwa katika Sekta ya Elimu kutokana na utekelezaji
wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya
Sekondari na pia kuingizwa kwa Sekta ya Elimu katika Mpango wa Tekeleza Sasa kwa
Matokeo Makubwa. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko la Shule za
Msingi za Serikali kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi Shule 16,538 mwaka 2015 na
idadi ya Wanafunzi imeongezeka kutoka 7,541,208 hadi 8,202,892 katika kipindi
hicho. Vilevile, idadi ya Walimu wa Shule za Msingi imeongezeka kutoka Walimu
135,013 mwaka 2005 hadi Walimu 190,957 mwaka 2015 hatua ambayo imeimarisha
uwiano wa Mwalimu kwa Mwanafunzi kutoka 1:56 mwaka 2005 hadi 1:43 mwaka 2015.
91.
Mheshimiwa Spika, katika Elimu ya
Sekondari, idadi ya Shule za Sekondari za Serikali imeongezeka kutoka Shule
1,745 mwaka 2005 hadi Shule 4,753 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia
172.4 Idadi ya Wanafunzi wa Shule za Sekondari wa Kidato cha Kwanza hadi cha
Sita (6) imeongezeka kutoka Wanafunzi 524,325 mwaka 2005 hadi Wanafunzi
1,704,130 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 225. Idadi ya Walimu wa
Sekondari pia imeongezeka kutoka 20,754 mwaka 2005 hadi Walimu 80,529 mwaka
2015, sawa na ongezeko la asilimia 288. Pia kumekuwa na ongezeko la idadi ya
vyumba vya madarasa kutoka 5,795 mwaka 2005 hadi 49,882 mwaka 2015, sawa na
ongezeko la asilimia 760.8. Aidha, kufuatia Agizo la Mheshimiwa Rais, Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete la kuboresha elimu ya sayansi nchini, ujenzi wa vyumba
vya maabara ya sayansi umeongezeka kwa
kasi hadi kufikia 5,979 mwaka 2015
ikilinganishwa na 247 mwaka 2005, sawa na ongezeko la asilimia 2,321. Ongezeko
hilo kubwa ni matokeo ya utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM. Nawapengeza sana
Wananchi kwa kushirikiana vizuri na Serikali yao kufikia hatua hiyo.
92.
Mheshimiwa Spika, udahili katika Vyuo
vya Elimu ya Ufundi na Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi umeongezeka kutoka
Wanafunzi 78,586 mwaka 2005/2006 hadi kufikia Wanafunzi 145,511 mwaka 2013/2014,
sawa na ongezeko la asilimia 85. Aidha, Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki
vimeongezeka kutoka 23 mwaka 2005 hadi Vyuo Vikuu 49 mwaka 2013/2014. Pia,
udahili katika Vyuo vya Elimu ya Juu umeongezeka kutoka Wanafunzi 40,719 mwaka
2005/2006 hadi Wanafunzi 204,175 mwaka 2013/2014. Wanafunzi wanaopata Mikopo ya
Elimu ya Juu wameongezeka kutoka Wanafunzi 42,729 mwaka 2005/2006 hadi takriban
Wanafunzi 94,000 mwaka 2013/2014. Mafanikio haya makubwa yametokana na
utekelezaji madhubuti wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. Serikali
itaendelea kuimarisha elimu katika ngazi zote kwa kutambua umuhimu wa elimu
katika maendeleo ya Taifa na kufikia malengo ya nchi yetu ya kuwa na kipato cha
kati ifikapo mwaka 2025.
Afya
93.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha
Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa mwaka 2007 – 2017 ili
kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote. Chini ya Mpango
huo, kila Kijiji kinatakiwa kuwa na Zahanati, kila Kata kuwa na Kituo cha Afya
na kila Wilaya kuwa na Hospitali ya Wilaya. Kutokana na utekelezaji mzuri wa Mpango
huo, idadi ya Vituo vya Kutolea Huduma za Afya nchini vimeongezeka kutoka Vituo
5,172 mwaka 2005 hadi 7,247 mwaka 2014 na Wataalamu 55,608 wa Kada ya Afya wamepangiwa
kufanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi hicho. Katika mwaka
2014/2015, Serikali imeajiri jumla ya Watumishi 8,119 ili kuongeza kasi ya
utoaji huduma katika Sekta ya Afya. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea
kuongeza idadi ya Vituo vya Kutolea Huduma za Afya, dawa na vifaa tiba pamoja
na kuajiri Watumishi zaidi wa Sekta ya Afya.
94.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha
huduma za tiba za kibingwa katika Hospitali za Kanda, Hospitali Maalum na
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kutoa huduma bora za afya na kupunguza
idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Huduma zilizoanzishwa nchini ni pamoja na upasuaji mkubwa wa moyo, upasuaji wa
mgongo na ubongo, kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo na huduma
ya mionzi. Hadi sasa, jumla ya wagonjwa 605 wamepatiwa huduma ya upasuaji
mkubwa wa moyo na wagonjwa 1,198 walisafishwa damu katika hospitali hizo.
95.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu
ya Nne, pia imepata mafanikio makubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa Mpango
Mkakati Mpya wa Kudhibiti Malaria Nchini na Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza
Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto Wenye Umri chini ya miaka mitano.
Kupitia Mpango wa Kudhibiti Malaria, jumla ya Vyandarua Milioni 40.7 vyenye Viuatilifu
vya muda mrefu vilisambazwa nchini. Juhudi hizo pamoja na mpango wa kuangamiza
viluwiluwi vya mbu na ongezeko la upatikanaji wa dawa mseto za malaria katika Vituo
vyote vya Kutolea Huduma ya Afya nchini zimewezesha kupungua kwa maambukizi ya
ugonjwa wa malaria kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 18 mwaka
2007 hadi asilimia 9.5 mwaka 2012. Kupungua kwa maambukizi hayo pamoja na kuimarishwa
huduma za chanjo kwa watoto na wajawazito kumechangia kupungua kwa vifo
vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 578 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2005
hadi vifo 432 mwaka 2012. Vilevile, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka
mitano vimepungua kutoka vifo 112 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2005 hadi
vifo 52 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2012. Juhudi hizo zimeiwezesha Tanzania
kuwa miongoni mwa nchi tano Barani Afrika ambazo zimepunguza vifo vya watoto
wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa theluthi mbili na hivyo kuvuka Lengo
Namba Nne la Malengo ya Milenia.
96.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua
kubwa iliyofikiwa katika udhibiti wa magonjwa hapa nchini, tunakabiliwa na
ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani. Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka
wanagundulika wagonjwa wapya wa saratani 44,000 na kati yao, wagonjwa 35,000
hufariki kutokana na ugonjwa huo. Hii ni changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa
ipasavyo ili kuokoa maisha ya wananchi wetu. Serikali kwa kushirikiana na wadau
imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na
kutoa elimu ya utambuzi wa dalili za awali na umuhimu wa kuwahi kupata huduma. Hatua
nyingine ni pamoja na kuimarisha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kutoa matibabu na tiba shufaa kwa wagonjwa wa
saratani. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa
huduma za uchunguzi wa awali wa saratani katika ngazi ya Kanda. Aidha,
itaelimisha wananchi kutambua dalili za awali za saratani na umuhimu wa kuwahi Vituo
vya Afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina kwa saratani za aina
mbalimbali zikiwemo saratani za matiti, shingo ya uzazi na tezi dume. Pia, Serikali
itaimarisha huduma kwa wagonjwa wa saratani kwa kununua mashine za mionzi tiba
ili kusogeza huduma karibu na wananchi na pia kupunguza gharama za kupeleka
wagonjwa wa saratani nje ya nchi.
Huduma kwa Wazee na Watu Wenye Ulemavu
97.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne inatambua kwamba watu wenye ulemavu
wanayo haki ya kuthaminiwa utu wao, kuendelezwa, kuheshimiwa na kutobaguliwa.
Pia, inatambua uwezo mkubwa walio nao katika kujiendeleza na kuchangia katika
uchumi na maendeleo ya nchi yetu. Serikali pia inatambua mchango wa wazee na
umuhimu wao kama hazina na chemchem ya busara katika jamii. Kwa kutambua
umuhimu huo, Serikali imeendelea kuwapatia huduma muhimu wazee na watu wenye
ulemavu kupitia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee na Sheria ya Usimamizi ya
Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010. Pia, Serikali imepanua na kuimarisha fursa ya
ushiriki wa walemavu katika siasa na uendeshaji wa uchumi pamoja na kuongeza
fursa za ajira kwa walemavu. Aidha, imeimarisha upatikanaji wa huduma za msingi
kama vile elimu, afya, mikopo na ujenzi wa majengo ya umma yanayozingatia
mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu.
98.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa jamii na
kupiga vita mila na desturi ambazo hazitoi fursa katika kulinda utu, ushiriki,
ulinzi na maendeleo ya watu wenye ulemavu na wazee. Natoa wito kwa jamii kuwa
na moyo wa kuwasaidia na kuwatunza wazee na watu wenye ulemavu. Vilevile, jamii
haina budi kuondokana na mila potofu zinazoathiri upatikanaji haki na maslahi
ya wazee na watu wenye ulemavu kama ilivyo kwa makundi mengine. Katika kipindi kijacho, Serikali ya CCM
itaweka mkazo zaidi katika kuhudumia wazee na watu wenye ulemavu kwa kuwapatia
huduma stahiki na fursa zitakazoweza kuinua hali zao za maisha.
Lishe
99.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti
wa Hali ya Afya nchini uliofanyika mwaka 2010 yalionesha
kwamba hali ya lishe nchini siyo ya kuridhisha, hususan kwa watoto wenye umri
wa chini ya miaka mitano (5). Vilevile, utafiti huo ulibaini kuwa hali ya lishe
ya wanawake walio kwenye umri wa kuzaa siyo ya kuridhisha kwa kuwa zaidi ya
nusu ya wanawake hao wana upungufu wa damu na mmoja kati ya 10 wana lishe duni.
Kutokana na hali hiyo, Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Lishe wa mwaka
2011/2012 hadi 2015/2016 ambao niliuzindua tarehe 19 Septemba, 2011. Ili
kutekeleza Mkakati huo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Lishe yenye
jukumu la kusimamia na kuratibu masuala yote ya lishe nchini. Pia, Serikali imeanzisha Dawati la Lishe
katika Wizara zinazojishughulisha na masuala ya lishe na katika Halmashauri
zote nchini. Aidha, Wizara ya Fedha imetoa Kasma maalum kwa ajili ya Halmashauri
kutenga fedha za lishe. Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kuendelea kusimamia
utekekelezaji wa Kanuni za Kusindika Chakula
kwa Kuongeza Virutubishi.
100.
Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada
hizo, Tathimini ya Kitaifa ya Hali ya Lishe Nchini iliyofanyika mwaka 2014
imeonesha kuwa hali ya lishe kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano
imeanza kuimarika. Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha udumavu kwa watoto walio
chini ya umri wa miaka mitano kimepungua kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi
asilimia 34.7 mwaka 2014, ukondefu umeshuka kutoka asilimia 4.9 hadi asilimia
3.8 na uzito pungufu umeshuka kutoka
asilimia 16.2 mwaka 2010 hadi asilimia 13.4 mwaka 2014.
101.
Mheshimiwa Spika, pamoja na matokeo hayo ya kutia moyo, hasa ya kushuka
kwa kiwango cha udumavu Kitaifa, bado kuna Mikoa tisa ya Tanzania Bara ambayo
ina viwango vya zaidi ya asilimia 40 ya watoto waliodumaa. Mikoa hiyo ni Iringa,
Njombe, Kagera, Dodoma, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita. Matokeo hayo
yamebainisha pia kupungua kwa matumizi ya chumvi yenye madini joto katika Kaya
kutoka asilimia 81.7 mwaka 2010 hadi asilimia 64.4 mwaka 2014. Hii siyo habari
njema ikizingatiwa kwamba upungufu wa madini joto una madhara makubwa ikiwemo
tatizo la tezi ya shingo na watoto kuvia kiakili. Ili kukabiliana na hali hiyo, Mamlaka za Udhibiti
zikiwezo Mamlaka ya Chakula na Dawa na Shirika la Viwango Tanzania zimeagizwa zihakikishe
kwamba chumvi inayozalishwa na kuuzwa nchini imeongezewa madini joto kwa
viwango vinavyokubalika kimataifa. Aidha, ninatoa wito kwa jamii kuhakikisha
kuwa zinapata chakula chenye lishe bora na kutumia chumvi yenye madini joto. Katika
mwaka 2015/2016, Serikali itakamilisha Sera ya Taifa ya Lishe na kuandaa Mpango
wa Utekelezaji utakaonesha gharama na jukumu la kila mdau katika kupambana na
tatizo la lishe duni.
Maji
102.
Mheshimiwa Spika,
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mkakati wa Kuendeleza
Sekta ya Maji na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Ili kuongeza kasi ya
utekelezaji wa miradi ya maji nchini, Sekta ya Maji ilijumuishwa katika Mpango
wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Kutokana na utekelezaji mzuri wa programu
na miradi ya maji, mafanikio makubwa yamepatikana Mjini na Vijijini. Hadi mwezi Februari 2015, miradi ya maji ya Vijiji 931 ilikamilika ikilinganishwa na miradi 248
iliyotekelezwa mwaka 2013/2014. Aidha, miradi mingine katika Vijiji 607 ipo
katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Utekelezaji wa miradi hiyo umeongeza upatikanaji
wa huduma za maji Vijijini hadi kufikia asilimia 53 ambapo jumla ya watu
milioni 19.9 wamenufaika ikilinganishwa na watu 2,390,000 walionufaika na
huduma hiyo Desemba, 2013. Katika mwaka 2015/2016, Serikali imepanga kujenga
miradi ya maji 731 katika Vijiji 1,189 na kujenga Vituo vya kuchotea maji
25,790 ambavyo vitanufaisha takribani watu milioni saba (7). Kukamilika kwa
miradi hiyo kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji Vijijini kufikia asilimia
71.
103.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza wastani wa upatikanaji wa
huduma ya maji katika Miji Mikuu ya Mikoa kutoka asilimia 78 mwaka 2005 hadi
asilimia 86 mwezi Desemba, 2014. Aidha, kupitia Mpango wa Kuboresha Huduma ya
Majisafi na Majitaka Jijini Dar es Salaam, hadi Januari, 2015 Serikali imekamilisha
mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini. Vilevile, imekamilisha ulazaji
wa kilomita 53 za bomba kuu kutoka mtambo wa maji wa Ruvu Chini hadi matanki ya
Chuo Kikuu cha Ardhi, sawa na asilimia 94 ya urefu wa bomba lote. mradi huo
utakapokamilika utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 180 hadi lita
milioni 270 kwa siku. Serikali pia imeendelea kutekeleza mradi wa upanuzi wa
mtambo wa maji wa Ruvu Juu ambao unahusisha upanuzi na ulazaji wa bomba kuu kutoka kwenye mtambo huo hadi Kibamba na ujenzi wa tanki
jipya la Kibamba. Mradi huo utakapokamilika, utaongeza uzalishaji wa maji
kutoka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 kwa siku. Katika mwaka 2015/2016,
Serikali itakamilisha utekelezaji wa mradi huo.
MAENEO MAPYA YA UTAWALA
104.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu
ya Nne imeendelea na jitihada za kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa
kuanzisha maeneo mapya ya utawala katika ngazi mbalimbali. Katika kipindi hiki,
Serikali imeanzisha Mikoa mipya minne ya Geita, Katavi, Njombe na Simiyu.
Aidha, imeanzisha Wilaya mpya 19, Halmashauri mpya 36 na Mamlaka za Miji Midogo
mpya 12. Pia, Serikali imeanzisha Kata 497 na hivyo kuongeza idadi ya Kata
zilizopo nchini kutoka Kata 3,337 mwaka 2005 hadi 3,834 mwaka 2015. Vilevile,
Serikali imeongeza Vijiji kutoka 11,795 hadi Vijiji 12,300 na Mitaa kutoka
2,995 hadi 3,939. Idadi ya Vitongoji nchini nayo imeongezeka kutoka 60,359 hadi
kufikia 64,691 katika kipindi hicho. Ni imani yangu kwamba kuanzishwa kwa maeneo
hayo kutawawezesha Wananchi kupata huduma muhimu za kiutawala na za kijamii kwa
ufanisi zaidi karibu na maeneo wanayoishi.
USTAWISHAJI MAKAO MAKUU DODOMA
105.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu
ya Nne imejenga
barabara za lami zenye urefu wa Kilometa 47.7 na kuboresha huduma ya umeme,
maji safi na majitaka katika Mji wa Dodoma. Aidha, imeandaa mipango ya matumizi
bora ya ardhi, ramani za makazi na maeneo ya uwekezaji kulingana na kasi ya maendeleo
ya Mji. Vilevile, imeboresha na kuhalalisha maeneo yaliyojengwa kiholela. Kuanzia
mwaka 2005 hadi 2014, jumla ya viwanja 20,394
vimepimwa na kumilikishwa kwa waendelezaji na vibali vya ujenzi wa nyumba 2,869
vimetolewa. Katika mwaka 2015/16,
Serikali imepanga kusanifu miundombinu ya barabara zenye urefu wa kilometa 55
na mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 13 pamoja na kujenga barabara
zenye urefu wa kilometa tisa (9) kwa kiwango cha lami na Kilometa saba (7) kiwango
cha changarawe. Pia, Serikali itapima Viwanja 3,786 na kuandaa Hatimiliki 1,200
za viwanja.
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
106.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu
imeendelea kujenga mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi na nchi na
vyombo mbalimbali vya Kikanda na Kimataifa unaozingatia maslahi makubwa ya
Taifa letu. Mafanikio makubwa yamehusishwa na ziara za Viongozi wa Kitaifa
katika nchi mbalimbali ambazo zimeimarisha ushirikiano kati ya nchi yetu na
nchi hizo. Ziara hizo pia zimechochea na kukuza biashara, utalii na kuvutia
uwekezaji. Vilevile, ziara hizo zimekuwa chachu kwa Viongozi wengi wa Nchi na Mashirika
mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda kutembelea Tanzania wakiwemo Viongozi wa
Mataifa makubwa ya China, Marekani, Ujerumani, Japan na Uingereza. Ziara
zilizofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania zimeleta mafanikio makubwa hasa kuvutia wawekezaji katika Sekta
za Miundombinu ya barabara na uchukuzi, nishati, gesi asilia, elimu, afya, maji
na maliasili na utalii.
107.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza
diplomasia ya kiuchumi, Serikali inatumia Balozi zake kuitangaza nchi ili
kuvutia wawekezaji, kutangaza vivutio vya utalii na kutafuta fursa za masoko
ndani na nje ya nchi. Sambamba na hatua hizo, Serikali imeendelea kuhakikisha Watanzania
wanaoishi nje ya nchi wanapata fursa za kuchangia maendeleo ya nchi yao. Mwezi
Agosti 2014, Serikali iliandaa Mkutano wa Kwanza wa ‘Diaspora’ uliofanyika Dar es Salaam kwa lengo la kuwakutanisha
pamoja Watanzania waishio nje ya nchi ili kujadili namna wanavyoweza kuchangia
kukuza uchumi wetu kulingana na fursa zinazopatikana nje ya nchi. Serikali
itaendelea kuwashirikisha Watanzania waishio nje ya nchi kwenye shughuli za
maendeleo ili waweze kutoa mchango mkubwa kwa Taifa kwa kutumia fursa na uzoefu
wanaopata kwenye nchi wanazoishi.
108.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu inashiriki
kikamilifu katika kuimarisha ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mtangamano wa Afrika Mashariki unahusisha hatua zifuatazo: Umoja wa Forodha,
Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na Shirikisho la Kisiasa. Katika hatua ya
kwanza, Tanzania imefanikiwa kukuza biashara kati yake na nchi wanachama
kutokana na kuondolewa kwa ushuru wa forodha. Hatua hiyo imesaidia Tanzania
kuongeza mauzo ya bidhaa zake katika Nchi Wanachama. Mfano, katika mwaka 2013,
Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 1,120 na
imenunua bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 397. Katika hatua ya
pili ambayo ni Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, Tanzania imefungua fursa za
uwekezaji na ajira hasa katika Sekta zinazokabiliwa na uhaba wa Wataalam kama
vile Wahadhiri wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Walimu wa Shule za Sekondari katika
fani ya hisabati, fizikia, baiolojia na kemia.
109.
Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba, 2013
Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walitia saini Itifaki ya Umoja wa
Fedha ambayo ni hatua ya tatu ya Mtangamano. Kwa sasa nchi wanachama
zinatekeleza Mpango Kazi wa Miaka Kumi wa Kuelekea kwenye Eneo Huru la Sarafu Moja
ifikapo mwaka 2024. Katika Mwaka
2015/2016, Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa Himaya Moja ya Forodha;
Mpango Kazi wa Miaka Kumi wa Kuelekea Sarafu Moja; na kuongeza kasi ya kuondoa
vikwazo visivyo vya kiushuru katika biashara baina ya nchi wanachama.
MASUALA MTAMBUKA
Jinsia
110.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya
Nne inatambua uwezo na nguvu kubwa ya wanawake katika kusukuma kasi ya
maendeleo na kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kwa msingi huo,
Serikali imeongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi wa
kisiasa na nafasi za maamuzi. Katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa
Serikali ya Awamu ya Nne, idadi ya Mawaziri wanawake imeongezeka kutoka 6 kati
ya Mawaziri 25 katika mwaka 2005 hadi kufikia 10 kati ya Mawaziri 30 mwaka
2015; Wakuu wa Mikoa wameongezeka kutoka 2 kati ya Wakuu wa Mikoa 21 mwaka 2005
hadi 7 kati ya Wakuu wa Mikoa 25 mwaka 2015; Wakuu wa Wilaya wanawake
wameongezeka kutoka wanawake 20 kati ya
Wakuu wa Wilaya 104 mwaka 2005 hadi kufikia Wakuu wa Wilaya wanawake 46 kati ya
Wakuu wa Wilaya 133 mwaka 2015. Majaji wanawake wameongezeka kutoka 8 kati ya
50 mwaka 2005 hadi kufikia 24 kati ya Majaji 67
mwaka 2015; na Wabunge Wanawake
wameongezeka kutoka 62 kati ya Wabunge 288 mwaka 2005 hadi kufikia 127 kati
Wabunge 357 mwaka 2015.
111.
Mheshimiwa Spika, pia, Serikali imeendelea kuwahamasisha
wanawake kujiendeleza kielimu na kujenga uelewa wao katika kuweka nguvu za
kutetea haki zao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo. Vilevile,
Serikali imewajengea uwezo wa ujasiriamali, utaalam wa biashara, jinsi ya
kupata mitaji zaidi, masoko pamoja na kutoa mikopo mbalimbali. Idadi ya
wanawake waliopata mikopo kupitia Benki ya Wanawake Tanzania imeongezeka kutoka
wanawake wajasiriamali 689 mwaka 2010 hadi kufikia 42,648 mwaka 2014.
Vita Dhidi ya Rushwa
112.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea
na mapambano dhidi ya rushwa kwa kutekeleza
Mpango Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti Rushwa Nchini (NACSAP). Katika mwaka
2014/2015, Serikali imeendelea kushughulikia uchunguzi wa tuhuma 3,311 za
rushwa ambapo uchunguzi wa tuhuma 528 ulikamilika. Vilevile, majalada 187 ya
rushwa zilizotokana na Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali yalichunguzwa na kati ya hayo 31 yalikamilika na kuombewa kibali cha
mashtaka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, na tisa (9) yalipata kibali cha
kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani. Ili kuimarisha udhibiti wa Rushwa, Serikali
imeandaa Mkakati wa Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma, kwa kushirikisha Sekta
ya Umma na Sekta Binafsi. Pia, Serikali imeandaa rasimu ya Muswada wa
Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
113.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016,
TAKUKURU itaendelea kuchunguza tuhuma za makosa ya rushwa, kuwafikisha watuhumiwa
mbele ya Vyombo vya Sheria na kuishauri Serikali namna ya kuziba mianya ya
rushwa. Aidha, itachunguza tuhuma 2,783 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kukamilisha
chunguzi za tuhuma kumi (10) za rushwa kubwa na kuendesha Kesi 659 zilizopo Mahakamani
na zitakazoendelea kufunguliwa, na pia kutoa elimu kuhusu rushwa kwa Wananchi.
Hifadhi ya Mazingira
114.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Wananchi imeendelea na
juhudi za kupambana na uharibifu wa mazingira
kwa kuchukua hatua mbalimbali. Hatua
hizo ni pamoja na kusimamia sheria zinazozuia ukataji miti kiholela na uchomaji
moto na kuharibu vyanzo vya maji; kuweka mazingira safi Mijini na Vijijini pamoja
na kuhimiza na kusimamia zoezi la upandaji miti kila mwaka ambapo kati ya mwaka
2006 na 2013, jumla ya miti bilioni 1.3 ilipandwa.
Vilevile, Serikali imeandaa na kutekeleza Mpango wa Kudhibiti Hewa Ukaa na Mabadiliko
ya Tabia Nchi. Aidha, Serikali inatekeleza Mkakati Maalum wa Kuhifadhi Mazingira
katika Mito, Bahari, Maziwa na Ukanda wa Pwani. Hatua hizo zimeleta mwamko wa Wananchi
wengi kuhifadhi mazingira. Napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Mikoa na Halmashauri
ambazo zimefanya juhudi kubwa kuhimiza na kusimamia masuala ya hifadhi ya
mazingira na usafi katika maeneo yao.
115.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015,
Serikali imeimarisha ukaguzi wa athari za mazingira kwa kukagua Viwanda na Taasisi 30 pamoja na Migodi 13. Katika
ukaguzi huo, jumla ya viwanda 11 vya Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro
vilivyobainika kuchafua mazingira vilipewa notisi ya kurekebisha mifumo ya
majitaka na uchafuzi hewa. Vilevile, Viwanda 19 vya Mikoa ya Kanda ya
Ziwa, Dar es Salaam na Mtwara vimetozwa faini kwa kukiuka Sheria ya
Mazingira ya mwaka 2004. Ukaguzi unaendelea katika maeneo mengine nchini na
wale watakaobanika kukiuka Sheria ya Mazingira watachukuliwa hatua stahiki. Naagiza
Viongozi
katika ngazi zote kushirikiana na Wananchi kusimamia suala la kutunza na
kuhifadhi mazingira katika maeneo yao.
Menejimenti ya Maafa
116.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekumbwa
na maafa mbalimbali katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Maafa hayo ni
pamoja na mafuriko, ukame, maporomoko ya udongo na migodi ya wachimbaji wadogo,
kuporomoka kwa majengo, milipuko ya mabomu, radi, mvua ya mawe iliyoambatana na
upepo mkali na ajali za barabarani na majini. Serikali ya Awamu ya Nne kwa
kushirikiana na wadau imefanya jitihada za kukabiliana na maafa hayo kwa
kuwapatia waathirika huduma za msingi kama vile chakula, maji, matibabu, makazi
ya muda, msaada wa maziko kwa waliofiwa na fidia kwa uharibifu wa nyumba na
samani.
117.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
mwaka 2006 hadi 2014, Serikali ilitoa jumla ya tani 336,378 za chakula zenye
thamani ya Shilingi Bilioni 128.2 na Shilingi Bilioni 24.2 za usafiri kwa ajili
ya kukabiliana na uhaba wa chakula katika maeneo mbalimbali nchini. Pamoja na
msaada wa chakula, Serikali ilitumia Shilingi Bilioni 25.7 kulipa fidia na
kifuta machozi kwa wananchi walioathirika na maafa mbalimbali yakiwemo ya mlipuko
wa mabomu Mbagala na Gongolamboto Jijiji Dar es Salaam. Aidha, Serikali imeendelea
kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na maafa nchini kwa kutoa mafunzo ya kujiandaa
na kukabiliana na maafa kwa Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya pamoja na vikosi
vya Majeshi. Vilevile, Serikali imehakikisha kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula umehifadhi chakula cha kutosha
wakati wote. Katika mwaka 2014/2015, Sheria ya Menejimenti
ya Maafa ilitungwa na Bunge ili kuongeza ufanisi katika kuzuia, kujiandaa,
kukabili na kurejesha hali ya kawaida baada ya maafa kutokea. Sheria hiyo pia
imeweka utaratibu wa kuanzisha Wakala wa Menejimenti ya Maafa pamoja na kuunda
Kituo cha Utendaji na Mawasiliano wakati wa Dharura. Serikali inakamilisha
Kanuni za Sheria hiyo ili kurahisisha matumizi na usimamizi wa Sheria hiyo.
118.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka
ya Hali ya Hewa ilitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa upungufu wa
mvua za vuli na masika. Kwa kuzingatia tahadhari hiyo, mwezi Januari 2015,
Serikali ilifanya tathmini ya hali ya chakula nchini. Tathmini hiyo ilibaini
kwamba, Halmashauri za Wilaya 23 katika Mikoa 12 zimeonesha dalili ya upungufu wa chakula kutokana na
mvua kidogo za vuli. Tathmini inaonesha kuwa zaidi ya watu 400,000 watakabiliwa na upungufu wa chakula. Serikali imetenga tani 10,000 za chakula cha msaada kwa wananchi hao na tani 294.3 za mbegu bora za mazao mbalimbali zinazokomaa katika muda
mfupi. Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika kwa kushirikiana na Mikoa, Wilaya na
Halmashauri zinaendelea kufanya tathmini
nyingine ya hali ya chakula nchini kwa lengo la kupata takwimu sahihi za Wananchi
wenye upungufu wa chakula ili wapatiwe chakula kwa wakati.
119.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016,
Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wake katika Menejimenti ya Maafa kwa kutoa
elimu kwa wadau, na kuanza maandalizi ya kuanzisha Wakala wa Menejimenti ya
Maafa kama ilivyoainishwa na Sheria ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2014.
Udhibiti wa UKIMWI
120.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya
Nne imeendeleza jitihada za kupambana na ugonjwa wa UKIMWI ambao umekuwa tishio
kubwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Serikali imetekeleza Mkakati wa Taifa wa Pili
na wa Tatu wa Kudhibiti UKIMWI na kuanza maandalizi ya Sera Mpya ya Taifa ya
Kudhibiti UKIMWI. Mabaraza 92 ya Wilaya ya Watu Waishio na Virusi vya UKIMWI yameundwa
kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi yao na kufanya uraghabishi ili kuongeza
mwitikio wa jamii katika udhibiti wa VVU na UKIMWI. Vilevile, Serikali
inatekeleza Mpango wa Matunzo na Matibabu kwa Waishio na Virusi vya UKIMWI
ambapo vituo vinavyotoa huduma hiyo vimeongezeka kutoka Vituo 700 vilivyokuwepo
mwaka 2008 hadi kufikia Vituo 1,209 mwaka 2014. Katika kipindi hicho, idadi ya
watu waliosajiliwa katika Mpango huo imeongezeka kutoka 403,378 hadi milioni
2.2 na kati yao, waathirika 850,274 wanapata huduma za tiba na matunzo katika Vituo
vya Afya kote nchini. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imeanzisha Mfuko wa
Kudhibiti UKIMWI kwa lengo la kuhakikisha kuwa upatikanaji wa fedha kwa ajili
ya udhibiti wa UKIMWI unakuwa endelevu.
121.
Mheshimiwa Spika, wanawake wajawazito
75,866 waishio na VVU walipata huduma ya dawa za kuzuia maambukizi ya VVU
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kutoa elimu
ya VVU na UKIMWI kwa jamii na kuhamasisha upimaji wa hiari wa afya na tohara ya
hiari ya kitabibu kwa wanaume ambapo hadi mwaka 2014, jumla ya wanaume 676,225
wamepatiwa huduma hiyo. Kutokana na juhudi hizo, utafiti uliofanyika mwaka
2011/2012 umeonesha kuwa kiwango cha ushamiri wa Virusi vya UKIMWI kwenye jamii
kimepungua kutoka asilimia 7.0 mwaka 2003/2004 hadi asilimia 5.7 mwaka 2007/2008
na asilimia 5.1 mwaka 2011/2012. Maambukizi mapya yamepungua kutoka wastani wa
watu 140,000 mwaka 2009 hadi 74,000 mwaka 2014 na maambukizi mapya kwenye rika
la watoto wa umri wa miaka 0 hadi 14 yamepungua kutoka 33,000 hadi 17,000 mwaka
2013. Hii inaashiria kupungua kiwango cha maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto kwa kipindi hicho. Vilevile, vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kutoka
145,000 mwaka 2005 hadi 80,000 mwaka 2013.
122.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika
mwaka 2015/2016, itaimarisha mapambano dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, hususan kwa
Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, kupunguza kasi ya maambukizi kwenye
Mikoa 12 yenye mzigo mkubwa wa ugonjwa wa UKIMWI, kukamilisha maandalizi ya taratibu
za uendeshaji wa Mfuko wa Kudhibiti
UKIMWI, na kutoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI. Aidha, kuendelea kutekeleza vipaumbele
vilivyoainishwa kwenye Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI. Serikali kwa kushirikiana na wadau
itafanya Utafiti wa nne wa Kutambua Kiwango cha Maambukizi kwa kila Mkoa.
Udhibiti wa Dawa za Kulevya
123.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya Dawa za
Kulevya ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili wananchi wetu na kuathiri
afya za watumiaji ambao wengi wao ni vijana na kudhoofisha nguvu kazi na uchumi
wa Taifa letu. Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto
hiyo. Hatua hizo ni
pamoja na kuimarisha uwezo wa Tume ya Kuratibu
Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini, kuanzisha Kikosi Kazi cha Udhibiti wa Dawa
za Kulevya na kutekeleza programu mbalimbali za uelimishaji Vijana juu ya
athari za matumizi na biashara ya Dawa za Kulevya. Aidha, huduma za matibabu ya
dawa ya Methadone kwa wanaotumia dawa
za kulevya aina ya Heroin zimeanzishwa
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Mwananyamala na Temeke
ambapo hadi Machi 2015 watumiaji 2,223 walikuwa wakipata huduma za matibabu. Vilevile,
suala la dawa za kulevya limeingizwa kwenye mitaala ya Shule za Msingi. Serikali
pia inajenga Kituo cha Waathirika wa Dawa za Kulevya katika Hospitali ya Rufaa
ya Mirembe, Dodoma.
124.
Mheshimiwa Spika, operesheni
zilizoendeshwa na Kikosi Kazi cha Kupambana na Dawa za Kulevya kuanzia mwezi
Julai 2014 hadi Machi 2015, zimewezesha kukamatwa kwa kilo 126.4 za dawa za
kulevya aina ya Heroin, kilo 1.8 za Cocaine na kilo 8,210 za bangi. Jumla ya watuhumiwa 39 wamekamatwa
na kufikishwa kwenye Vyombo vya Sheria. Katika kipindi hicho, Tume ya Kuratibu
Udhibiti wa Dawa za Kulevya ilitoa elimu kwa umma wakiwemo waandishi wa habari,
wasanii na Wanafunzi wa Shule za Sekondari na Vyuo Vikuu. Pia, katika mwaka
2014/2015 Sheria Mpya ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ilitungwa na Bunge lako
Tukufu ili kuimarisha udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
125.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa mwaka
2015/2016, itaimarisha utoaji wa elimu kwa umma juu ya athari za biashara na
matumizi ya dawa za kulevya na kukijengea uwezo zaidi Kikosi Kazi cha Kupambana
na Dawa za Kulevya Nchini. Serikali pia itakamilisha Kanuni za utekelezaji wa Sheria
Mpya ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kuendeleza ushirikiano na nchi nyingine
katika mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya.
HITIMISHO
126. Mheshimiwa Spika, nimeeleza kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali ya Awamu ya Nne imetekeleza
kwa kipindi cha miaka kumi. Aidha, nimetoa mwelekeo wa kazi zitakazofanyika
katika mwaka 2015/2016. Ningependa kusisitiza mambo muhimu yafuatayo:
(a)
Ili Nchi yetu iendelee,
ni lazima tukuze Uchumi kwa kuongeza Uzalishaji na Tija katika Sekta zote. Tunahitaji
kutoa kipaumbele zaidi katika Sekta ya Kilimo kwa maana ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, ufugaji, uvuvi
na matumizi sahihi ya misitu yetu. Hii
ni kwa sababu zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea Kilimo.
Kwa hiyo, Azma ya “Kilimo Kwanza”
iwe ni kichocheo cha kuhimiza mipango na mikakati tuliyojiwekea ya kuendeleza
Kilimo katika Nchi yetu. Natoa wito kwa Viongozi na Wadau wa Maendeleo
kushirikiana na Serikali kuwahimiza Wananchi kuhusu matumizi ya teknolojia
sahihi ikiwemo mbolea, dawa za kuua wadudu, mbegu bora na zana za kisasa
za kilimo ili kuongeza
uzalishaji katika kilimo na kukibadili kutoka kilimo cha
kujikimu kuwa chenye tija na cha kibiashara. Pia, tuwahimize kuhusu umuhimu wa
kutumia wataalamu wa kilimo waliopo katika maeneo yao. Serikali itaweka
mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji kutoka Sekta Binafsi, kuimarisha masoko
pamoja na utafiti na kuhimiza Kilimo cha Umwagiliaji, ujenzi wa viwanda vya
kusindika mazao na kuweka utaratibu madhubuti wa mikopo.
(b)
Tumeona mafanikio
yaliyopatikana kwa kutekeleza Awamu ya Pili ya MKUKUTA iliyoanza Julai, 2010 na
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Aidha, tumeshuhudia kuongezeka kwa kasi ya
utekelezaji wa miradi ya kipaumbele chini ya mfumo wa BRN! Matokeo ya
utekelezaji wa mfumo huo ni mazuri na yanatia matumaini na inabidi tuendelee
kufuatilia kwa karibu miradi ya kipaumbele na kufanya tathmini za mara kwa mara
ili kupima matokeo. Nawaomba tuendeleze mafanikio yaliyopatikana ili
kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea. Pia, hatuna budi kutumia rasilimali
adimu tulizonazo kwa umakini na uangalifu mkubwa ili kufikia malengo hayo.
(c)
Tumefanya kazi nzuri ya kujenga
madarasa ya Shule za Sekondari kwa ajili ya Wanafunzi waliofaulu mtihani wa
darasa la saba. Kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ijipange vizuri kuhakikisha
kwamba Wanafunzi wote wanaofaulu wanapata nafasi ya
kujiunga na kidato cha kwanza. Aidha, ujenzi wa madarasa uende sambamba
na ujenzi wa nyumba za Walimu, maabara, maktaba, hosteli na vyoo vya kutosha.
Nazihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa
nyumba za Walimu, maabara na hosteli za Wanafunzi ili kupanua na kuimarisha
miundombinu ya Shule nchini.
(d)
Ardhi tuliyonayo
ni hazina kubwa inayohitaji kuwa na Mpango wa Matumizi Bora. Hivyo,
nazihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuandaa na
kutekeleza kwa kasi mipango ya matumizi
bora ya ardhi katika maeneo yao ikiwemo kupima vijiji, mashamba na viwanja.
Aidha, nawakumbusha Wananchi kutii Sheria, Kanuni na Taratibu za Ardhi zilizopo
ili kuepuka migogoro ya ardhi hasa ile ya wafugaji na wakulima; wananchi na
wawekezaji; na wafugaji/wakulima na maeneo ya Hifadhi.
(e)
Tunayo changamoto
ya kuyasaidia makundi maalum
katika jamii yetu kama vile Watu wenye Ulemavu wa Ngozi na vikongwe
ambao bado wanaendelea kuuawa kikatili. Tuendelee kushirikiana kumaliza kabisa
tatizo hilo kwa kuwafichua wale wanaofanya vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua
za kisheria. Naomba tusichoke kuwasaidia Watu wenye Ulemavu kwa kuwapa moyo, kuwaondolea
hofu, na kuwasaidia pale inapobidi ili waweze kujiletea maendeleo.
(f)
Tunaelekea katika
Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2015. Serikali itahakikisha amani, utulivu na
umoja katika nchi yetu unadumishwa. Natoa wito kwa wale wote watakaogombea
nafasi mbalimbali za Uongozi na Wananchi wote kuepuka kujihusisha na vitendo
vya rushwa wakati wa uteuzi, kampeni na Uchaguzi Mkuu. Aidha, Viongozi wa Vyama
vya Siasa na Wanachama wao wanadi Sera na mikakati ya Vyama vyao kwa kutumia
lugha ya kistaarabu badala ya kutumia lugha zisizo na staha zinazoweza
kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu nchini. Tujenge Taifa moja lenye
msingi wa kuheshimiana na kuenzi amani na utulivu uliopo nchini.
127. Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hoja yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman
Ghasia (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi
Zilizofanyika katika Mwaka 2014/2015 na Mwelekeo wa Kazi za Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa kwa Mwaka 2015/2016. Ni matumaini yangu kwamba maelezo hayo yatawezesha
Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kufahamu kwa upana shughuli
zinazotekelezwa na Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
SHUKRANI
128. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru timu nzima ya Mawaziri na Naibu Mawaziri
kwa ushauri wao ambao umewawezesha Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais
na Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yao ya Kitaifa kwa ufanisi katika kipindi
cha Miaka Mitano iliyopita. Aidha, niwashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na
Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana
Sefue pamoja na vyombo vyote vya dola kwa kuiwezesha Serikali kutekeleza
majukumu yake ipasavyo na kukamilisha maandalizi yote ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2015/2016, pamoja na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya kila
Wizara, Mikoa, Wakala na Taasisi za Serikali Zinazojitegemea. Ninawashukuru Watanzania
wote na Washirika wa Maendeleo kwa michango yao ambayo imewezesha Serikali
kufanikisha kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
129. Mheshimiwa
Spika, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Mhandisi Christopher Kajoro Chiza,
Mbunge wa Buyungu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji na
Uwezeshaji) ; Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho,
Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge) ; Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara
Vijijini, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ;
Mheshimiwa Aggrey Joshua
Mwanri, Mbunge wa
Siha, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) kwa msaada mkubwa na
ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Shukrani za pekee kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa jitihada walizoonesha
katika kipindi hiki. Ninawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri
Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Florens M. Turuka na Bwana
Jumanne A. Sagini na Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Regina L. Kikuli na Bwana
Kagyabukama E. Kiliba, Bwana Zuberi M. Samataba na Dkt. Deo M. Mtasiwa, kwa
ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na
Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Ninawashukuru kwa
kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya
Waziri Mkuu kwa mwaka 2015/2016.
130. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, nchi yetu imepata Misaada na Mikopo kutoka kwa
Wahisani mbalimbali. Misaada na Mikopo hiyo imetoka kwa Nchi Rafiki, Nchi Wahisani,
Taasisi za Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mifuko mbalimbali ya Fedha
Duniani, Madhehebu ya Dini, Mashirika Yasiyo ya Serikali, Mashirika ya
Umma na Kampuni Binafsi za ndani. Misaada na Mikopo hiyo imechangia sana katika
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ninapenda kuwashukuru wote kwa dhati na kuwahakikishia kuwa Watanzania
tunathamini Misaada na Mikopo waliyotupatia na tutaendelea kushirikiana nao
katika harakati za kuleta maendeleo ya Taifa letu.
131. Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wapiga kura wangu wa
Jimbo la Katavi kwa imani na heshima kubwa waliyonipa ya kunichagua kuwa Mbunge
wao tangu mwaka 2000. Aidha, ninawashukuru Viongozi wenzangu wote na Wananchi
wote kwa ushirikiano wa dhati walionipa
katika kipindi chote cha uongozi wangu. Kipekee, ninapenda kumshukuru sana
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa imani kubwa kwangu kuniteua kuwa
Waziri Mkuu kwa vipindi viwili tangu tarehe 8 Februari, 2008. Ninamshukuru sana
Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake makini alioutoa kwangu na pia kwa kufanya kazi naye kwa karibu na kwa upendo mkubwa na
hivyo kuniwezesha kujifunza mengi kutoka kwake katika kipindi hiki.
Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano walionipa ambao umeniwezesha
kuwatumikia Watanzania katika nafasi hii kwa takriban Miaka Saba na Miezi Saba!
132. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninawashukuru viongozi wenzangu
wote wa kitaifa na viongozi wa ngazi nyingine zote kwa ushirikiano ambao
umeniwezesha kutekeleza jukumu kubwa la kusimamia Utendaji wa Serikali katika
Sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Nirudie tena
kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano mkubwa
mlionipa katika kipindi changu cha kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali
Bungeni. Nasema Asanteni sana!
133.
Mheshimiwa Spika, mwisho ningependa kutoa shukrani
kwa familia yangu, Mama Tunu Pinda na watoto wote kwa uvumilivu wao mkubwa na
kuniombea pamoja na kutia moyo jambo ambalo limeniwezesha kutekeleza majukumu
yangu ipasavyo.
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2015/2016
134. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2015/2016, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge
lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Tatu Kumi na Moja, Milioni Mia Saba Sitini na Tatu, Mia Sita
Themanini na Moja Elfu (311,763,681,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili Sitini na Nne,
Milioni Mia Nne Themanini, Mia Tatu na Sabini na Saba Elfu
(264,480,377,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Arobaini na Saba, Milioni Mia Mbili na Themanini na
Tatu, Mia Tatu na Nne Elfu (47,283,304,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
135.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu -
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Taasisi zake inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Nne na Tano, Milioni Mia
Moja na Moja, Mia Moja Tisini na Tano Elfu (405,101,195,000). Kati ya fedha
hizo, Shilingi Bilioni Hamsini, Milioni
Mia Tano na Thelathini na Tano, Mia Tano Sitini na Tisa Elfu (50,535,569,000)
ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni
Mia Tatu Hamsini na Nne, Milioni Mia Tano Sitini na Tano, Mia Sita Ishirini na
Sita Elfu (354,565,626,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
136. Mheshimiwa
Spika, Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Mbili na Themanini, Milioni Mia Mbili Kumi na
Nane, Mia Sita Sitini na Moja Elfu (280,218,661,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili Ishirini na
Tisa, Milioni Mia Tatu Kumi na Tatu, na Sabini Mbili Elfu (229,313,072,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Hamsini, Milioni Mia Tisa
na Tano, Mia Tano Themanini na Tisa Elfu (50,905,589,000) ni za Miradi ya
Maendeleo. Halmashauri zote zinaombewa jumla ya Shilingi Trilioni Nne, Bilioni Mia Saba Sitini na Sita, Milioni Mia
Saba, Mia Tano Thelathini na Tatu Elfu (4,766,700,533,000). Kati ya fedha
hizo, Shilingi Trilioni Nne, na Bilioni
Ishirini na Tatu, Milioni Mia Mbili Hamsini na Tano, Mia Moja Themanini na Moja
Elfu (4,023,255,181,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Saba Arobaini na Tatu, Milioni Mia Nne Arobaini
na Tano, Mia Tatu Hamsini na Mbili Elfu (743,445,352,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
137. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Saba,
Milioni Mia Tatu Thelathini na Saba, Mia Tatu na Tisa Elfu
(177,337,309,000) kwa ajili ya Mfuko
wa Bunge ambapo
Shilingi Bilioni Mia Moja na
Sitini na Tisa, Milioni Mia Tatu Thelathini na Saba, Mia Tatu na Tisa Elfu
(169,337,309,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Nane (8,000,0000,0000) ni za Miradi ya Maendeleo.
MUHTASARI
138.
Mheshimiwa
Spika, kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha
Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2015/2016 ya jumla ya Shilingi Trilioni Tano, Bilioni Mia Saba
Sitini na Tatu, Milioni Mia Saba Themanini na Nne, na Sabini Elfu
(5,763,784,070,000) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa; na jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Sabini na Saba, Milioni Mia Tatu Thelathini na Saba, Mia Tatu
na Tisa Elfu (177,337,309,000) kwa
ajili ya Mfuko wa Bunge, ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za
Ndani na Nje kwa ujumla wake.
139. Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo yanafafanua kwa kina Makadirio
ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Ofisi ya Waziri
Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge.
No comments:
Post a Comment