WAZIRI
MKUU, Mizengo Pinda amewataka Watanzania wenye uwezo wa kifedha waangalie
uwezekano wa kuanzisha viwanda hapa nchini badala ya kuendelea kuwa wachuuzi wa
kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kuziuza hapa nchini.
Ametoa
wito huo jana jioni (Jumatano, Mei 6, 2015) baada ya kutembelea maonyesho ya
biashara ya Syria yanayoendelea kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania pamoja na wafanyabiashara
kadhaa, Waziri Mkuu Pinda alisema mtindo unaoendelea wa kuuza mazao ghafi nje
ya nchi hauisaidii Tanzania kama nchi na badala yake unanemeesha viwanda na uchumi
wa nchi zinazonunua mazao hayo.
“Watazania
lazima wajiulize hivi bidhaa zote wanazoagiza kutoka nje ya nchi haziwezi
kabisa kuzalishwa hapa nchini ili kupunguza matumizi mkubwa ya fedha za kigeni,
kukuza uchumi na kuongeza ajira?,” alihoji Waziri Mkuu.
Alisema
wakati umefika sasa wa Tanzania kufikiria kuanzisha mpango mahsusi wa kulinda
viwanda vya ndani kwa kuweka vivutio vitakavyowashawishi wawekezaji na
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuanzisha viwanda vitakavyotumia
malighafi inayozalishwa hapa nchini hatua ambayo itawafanya wafanyabiashara wasiende
nje kununua bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini.
Mapema, Balozi wa Syria nchini, Mhe.
Abdulmounem Annan alimweleza Waziri Mkuu kuwa nchi yake inavyo viwanda vya nguo
za pamba zaidi ya 100 na pamba ghafi yote inayotumika kwenye viwanda hivyo
inalimwa nchini humo.
Balozi
Anan alisema yuko tayari kuandaa utaratibu utakaowawezesha wafanyabiashara,
wawekezaji na viongozi wa Serikali kwenda Syria ili kukutana na wenzao kwa
lengo la kujifunza na kuwashawishi waje kuwekeza Tanzania kwenye viwanda vya
nguo na vya kusindika vyakula.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
No comments:
Post a Comment