WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameishukuru taasisi
ya Kimataifa ya Lions Club kwa misaada ambayo imekuwa ikiitoa hapa nchini
katika nyanja za afya, utunzaji mazingira na uokoaji wakati wa maafa.
Akifungua kongamano la 12 la mwaka
linalojumuisha wadau wote wa Lions Club District 411 leo asubuhi (Jumamosi, Mei
9, 2015), Waziri Mkuu alisema anawashukuru wana Lions wote kwani miradi mingi
wanayoifanya huwa ni kwa kujitolea tu.
“Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi
hii kwani kwa sehemu kubwa wanachokifanya ni kile ambacho sisi kama Serikali
tulipaswa tukifanye. Wanatoa huduma bure za macho, matibabu ya moyo, wanatoa
misaa ya mahema, vyandarua, vyakula pale tunapokumbwa na maafa. Wanafanya kazi
nzuri,” alisema.
Akitolea mfano huduma za kijamii kama vile
Heart Baby Project, Waziri Mkuu alisema: “Mradi wa Heart Baby Project umedumu kwa miaka karibu 30. Wameshawachukua watoto
zaidi ya 3,000 wenye matatizo ya moyo na kuwapeleka India kuwapatia matibabu
kwa gharama zao,” alisema.
“Jambo kubwa zaidi la kushukuru ni kwamba asilimia
99.5 ya watoto waliofanyiwa upasuaji, wamepona na hivyo kuweza kuokoa maisha ya
watoto wetu,” alisema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na
wajumbe zaidi ya 500 waliohudhuria Kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Lions
International, Raju Manwani alisema taasisi hiyo ina wanachama zaidi ya milioni
1.4 duniani waliosambaa katika nchi 210 ambao hufanya kazi kwa kujitolea.
Naye Mwenyekiti wa Lions Multiple Council, Bw. Teja
Kalsi alisema wanapojiandaa kuadhimisha miaka 100 ya kuanzishwa kwa Lions Club,
wamejiwekea lengo la kuhakikisha wanatoa huduma kwa watu milioni 100 kwa katika
Nyanja zao nne kuu. Hivi sasa taasisis hiyo imetimiza mika 98 tangu kuanzishwa
kwake.
“Uanachama ndiyo nguzo yetu kuu lakini pia tuna
shauku ya kutimiza watu milioni 100 waliopata huduma zetu katika nyanja za
vijana, afya na hasa huduma ya macho, utunzaji wa mazingira na kuwalisha wenye
njaa. Tujielekeze huko ili tutimize kaulimbiu yetu isemayo palipo na uhitaji,
mwana-lion yupo (Where there’s a need, there’s a lion),” alisema.
Kongamano hilo limehudhuriwa na washiriki
kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia, Seychelles, Sudan Kusini, India na wenyeji
Tanzania.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment