WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka
maafisa mipango miji nchini kurekebisha utendaji wao wa kazi ili waweze
kubadili taswira mbaya iliyojengeka miongoni mwa jamii dhidi yao.
Ametoa kauli hiyo huo leo mchana (Alhamisi, Novemba 27, 2013) wakati akifungua
Mkutano wa Kwanza wa Wataalam wa Mipangomiji waliosajiliwa na Bodi ya
Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji ulioanza leo jijini Dar es Salaam.
“Taswira ya utendaji kazi katika taaluma ya mipangomiji
na katika sekta ya
ardhi kwa ujumla miongoni mwa wananchi na Serikali siyo
nzuri sana. Watafiti wanatueleza kuwa kati ya asilimia 60 na 80 ya makazi
kwenye miji yetu hapa nchini yamejengwa
kiholela. Na kwa kiwango hicho hicho wakazi wa mijini wako kwenye makazi hayo
na wanaishi kiholela,” alisema.
“Wako wanaosema ninyi ndiyo chanzo cha hiyo migogoro,
wako wanaosema ninyi kwa rushwa ndiyo wenyewe, mimi sishangai madai haya ila
ninawasihi muwe na roho ngumu katika kushinda vishawishi hivi,” alisisitiza.
Aliwataka wajadili masuala yanayohusu migogoro ya ardhi
bainaya wafugaji na wakulima, baina ya mipaka ya vijiji, baina ya wilaya, baina
ya wanavijiji na hifadhi za Taifa au maeneo ya uchumbaji madini na kujadili
njia za kutatua migogoro hiyo ili kuwa na mipamgo endelevu.
Aliwataka waangalie suala la ukuaji wa miji iliyokaribu
na Jiji la Dar es Salaam kwa kuangalia dhana ya miji mikubwa kubeba vijiji vinavyoizunguka
na hasa kuangalia uwezekano wa kupunguza mlundikano wa watu katika jiji hilo. “Miji
ya Kibaha, Mkuranga na Bagamoyo inatumikaje kusaidia kupunguza msongamnano
katika jiji la Dar es Salaam,” Waziri Mkuu alihoji
Alisema wataalamu wa mipango miji wanapaswa kuwa na maono
makubwa ya baadaye kama kweli wanataka kupunguza majanga katika siku za usoni. “Angalieni
utafiti wa gesi unaoendelea pale Mtwara na mjipange, angalieni mpango wa ujenzi
wa bandari ya Bagamoyo na kuunganisha na reli ya kati, angalieni Lindi na
upatikanaji wa Liquified Naturala Gas (LNG), pangeni miji kwa siku za baadaye
siyo sasa,” alisisitiza.
Aliwataka wanataaluma hao wasimamie vema taaluma yao
kwani katika miaka 37 ijayo, (mwaka 2050) inakadiriwa kwamba nusu ya watu wote
watakuwa wakiishi mijini. “Kuweni wakweli, tumieni weledi wenu la sivyo katika
miaka 37 ijayo kama wanavyosema watafiti, itakuwa balaa tupu,” alisema.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wataalamu
hao kutoka mikoa yote hapa nchini, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka alisema maafisa
mipango miji wanakabiliwa na changamoto ya kufikiri na kubuni aina ya miji
ambayo itakidhi mahitaji ya jamii ya baadaye.
Alisema hata hivyo maafisa hao wamekuwa wakikabiliwa na
changamoto ya kushindwa kutoa maamuzi ama ushauri wa kitaalamu kwa kuhofia
kuadhibiwa na madiwani.
Mkutano huo wa siku mbili
unafanyika katika hoteli ya Blue Pearl, Ubungo na unatarajiwa kufungwa kesho na
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, NOVEMBA 27, 2013
No comments:
Post a Comment