WAZIRI wa ushirika, chakula na masoko Mhandisi Christopher
Chizza amewahimiza viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika nchini kushikamana ili waweze kuendeleza na kuviimarisha vyama vya vyao badala ya kujenga dhana ya kuvididimiza.
Mhandisi Chizza aliyasema hayo jana wakati wa kikao chake na
viongozi wa serikali ya mkoa wa Kagera, uongozi wa chama cha ushirika Kagera
(KCU) na waandishi wa habari kilichofanyika kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa wa
Kagera.
Katika kikao hicho alisema migongano zinazojitokeza kati ya baadhi ya wanachama wanaounda vyama ushirika na waliopewa
jukumu la kusimamia na kuongoza vyama vya ushirika kamwe haziwezi kuviimarisha
na kuviendeleza vyama vya ushirika.
Alisema kuwa duniani kote migongano ndio huwa chanzo cha
kudidimiza vyama vya ushirika, Chizza alisema ili vyama vya ushirika viweze
kuimarika na kuendelea ni lazima wana
ushirika wapendane, waaminiane na waheshimiane, “hizi ndio nguzo kuu zinazoimarisha ushirika”alisema
kwa msisitizo.
“Ndugu zangu viongozi wa KCU ninapokea barua rundo
zinazowatuhumu, nyingine zinazoelea masuala ya ubadhilifu na barua hizi zinaandikwa
na wanaushirika wenu, ila taarifa mliyonipa ya utendaji wa kazi naiona iko wazi
na inaelezea hali halisi ya utendaji kazi mzuri wa KCU, sasa sielewi hizi barua
zinaashiria kitu gani” alisema kwa msangao.
Aliuagiza uongozi wa KCU kuwawajibisha watendaji ndani ya
ushirika huo wanawaona wanajihusisha na masuala ya ubadhilifu wa mali ya
wakulima, alisema yoyote wanayemuona anajihusisha na masuala ya ubadilifu
wasiishie kumfukuza tu bali wamfikishe mahakamani ili sheria ichukue mkondo
wake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa KCU, John Binunshu katika
taarifa yake kwa waziri huyo aliiomba serikali isitoe vibali vya kununua kahawa moja kwa moja toka kwa
wakulima kwa makampuni makubwa ambayo
ununua kahawa inayakusanywa na vyama vya ushirika moja kwa moja mnadani.
Binunshu alisema kuwa hali ya serikali kutoa vibali kwa
makampuni hayo makubwa inadhoofisha vyama vya ushirika kwa kuwa yanachangia
mnada wa kahawa kuchelewa, alisema minada ya kahawa inapochelewa vyama vya
ushirika vinakosa fedha za kuwalipa wakulima hivyo vinalazimika kununua kahawa
kwa mkopo.
Akitoa ufafanuzi juu ya kwa nini baadhi ya wanunuzi wa
kahawa wananunua kahawa kwa bei kubwa alisema, wanaonunua kahawa kwa bei kubwa
ni wale wanaonunua kahawa bila kutumia minzani, aliendelea kuwa wanunuzi hao
wananunua kahawa kwa ujazo badala ya kilo jambo ambalo linawapunja wakulima.
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bi. Ziporah Pangani alikiri kuwepo
kwa magendo ya kahawa, alisema kamati yake ya ulinzi na usalama
inalishughulikia suala hilo, alimaliza kwa kusema kuwa kamati yake imeshakamata
magari yaliyokuwa yanavusha kahawa kwa njia ya magendo na kufilisi kahawa hiyo.
No comments:
Post a Comment