Ndugu Mgeni rasmi,
Tunaomba kutambua uwepo wa Mkurugenzi mtendaji wa AGPAHI, Meneja wa
Miradi wa AGPAHI – Shinyanga & Simiyu, wafanyakazi wa AGPAHI, Waganga Wakuu
wa Mikoa ya Shinyanga na Simiyu, Madaktari kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto
Tanzania, wapendwa watoto na walezi, wageni waalikwa mabibi na mabwana.
Awali ya yote, tunachukua nafasi hii
kumshukuru mwenyenzi Mungu kwa kutuamsha salama siku hii ya leo.
Tunashukuru sana ndugu Mgeni rasmi kwa
kuacha shughuli zako na kukubali kuwa pamoja na sisi watoto.
Ndugu mgeni Rasmi,
Karibu katika Kambi yetu nzuri ya
Ariel hapa ELCT Bukoba Hotel. Kambi hii ya Ariel ni ya tano kufanyika chini ya
shirika la AGPAHI; kambi ya kwanza na ya pili zilifanyika hosteli ya Nyakahoja
mkoani Mwanza, na kambi ya tatu na ya nne zilifanyika Uhuru Hotel, Mkoani
Kilimanjaro. Kambi hii ya tano inafanyika hapa mkoani Kagera.
Tunapokua
kwenye kambi tunapata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali kama vile Taarifa
sahihi kuhusu VVU na UKIMWI; Ufuasi mzuri wa dawa na Kuweka wazi hali yetu;
Usafi binafsi; Stadi za maisha na Mabadiliko ya tabia kutokana na msukumo wa
kundi; Haki na wajibu watoto; Huduma na msaada wa kisaikolojia; Jinsia,
mahusiano ya kimapenzi na Uzazi wa Mpango.
Ndugu Mgeni Rasmi
Kambi ya Ariel mwaka 2015 imefanyika
hapa Bukoba, Mkoani Kagera kuanzia Jumatatu tarehe 15 Juni na tunategemea
kuhitimisha baadae leo tarehe 19 Juni.
Kambi hii ya tano ya shirika la
AGPAHI imetukutanisha watoto 57 kutoka Mikoa wa Shinyanga na Simiyu kwa muda wa
siku tano. Watoto tuliopo hapa tuna umri wa kati ya miaka 8 hadi 17. Katika
muda wa siku 5 tuliokaa hapa tumepata nafasi ya kucheza pamoja michezo
mbalimbali, tumechora picha mbalimbali, tumeimba, tumecheza mpira, tumeshiriki
kwenye shidano la mrembo na mtanashati wa Ariel Camp, tumepata marafiki, tumekula
chakula na pia tumeelewa kuwa AGPAHI inajali watoto wakue na kuishi kwenye
matumaini chanya.
Pia tumefanya matembezi na kuona mto Kagera, Kiwanda cha Sukari cha Kagera, kuona na kuelezewa
maeneo ya vita vya IDD AMIN na pia tumefika kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda
eneo la Mutukula.
Tumefurahi sana kwa sababu ni bahati
ya aina yake tuliyoipata kupitia shirika la AGPAHI.
Ndugu Mgeni rasmi
Tunapenda kutoa shukrani zetu za
pekee kwa shirika la AGPAHI kwa kubuni na kufadhili shughuli hizi za kambi ya
watoto na kututhamini na kutuenzi sisi watoto. AGPAHI imetusafirisha kutoka
Shinyanga na Simiyu na kutuleta hapa. Tunashukuru kwa kutujali kwa kutupa
zawadi mbalimbali. Pia tunashukuru wazazi na walezi wetu kwa kuturuhusu na
kutuandaa kwa safari hii yenye historia kubwa katika maisha yetu. Bila
kuwasahau wenyeji wetu wa hapa ELCT Bukoba Hotel kwa mapokezi na huduma nzuri
ya matunzo, chakula kizuri, malazi na mazingira tulivu.
Ombi
Ndugu Mgeni Rasmi
Tunaomba
Serikali yetu iwaunge mkono shirika la AGPAHI ili huduma za kisaikolojia kwa
watoto na kambi kama hizi ziendelezwe na zifikie watoto wengi zaidi kila mwaka
na pia zienee Tanzania nzima.
AGPAHI inajali watoto, wakue na kuishi
kwenye matumaini chanya
Risala
hii imeandaliwa na watoto wa kambi ya Ariel mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment