ZAIDI ya watu 23 wamekufa wilayani Muleba
kufuatia kuzuka kwa mlipuko wa ugonjwa malaria ambao ni pamoja watoto 16 chini
ya umri wa miaka 5 na watu wazima 7 kati ya mei 20 hadi mei 31, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili
lilizipata na ambazo zilithibitishwa na mkuu wa wilaya ya Muleba, Lembres
Kipuyo jana ni kwamba vifo hivyo vilitokea katika hospitali teule ya wilaya
hiyo ya Rubya.
Alisema katika wilaya hiyo maeneo ambayo
yamekubwa na mlipuko wa ugonjwa wa Malaria kuwa ni yale ya vijiji vinavyozuka
mto Ngono ambao maji yake hutiririka hadi Wilayani Missenyi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema vifo vingi
vilichangiwa na uhaba wa madawa, alisema baada ya mlipuko wa ugonjwa huo
kutokea hospitali teuli ya Rubya ilikuwa na kiasi kidogo cha madawa ya kutibu
ugonjwa wa Malaria.
uongozi wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na
uongozi wa mkoa umeunda mikakati madhubuti ya kudhibiti ugonjwa huo ambayo ni
pamoja namna ya kupata madawa kwa ajili ya kudhibiti mlipuko huo ambao ni
tishio kwa maisha ya watu.
Amesema hatu nyingine ambayo uongozi wa wilaya
ya Muleba umeichukua ya kudhibiti ugonjwa huo ni pamoja na kuwahamasisha
wananchi wanaoishi kwenye maeneo mlipuko wa malaria ulipojitokeza kuyafanyia
usafi maeneo yao ili waue mazalia ya mbu wanaoeneza malaria.
Hata hivyo pamoja na jitihada za uongozi wa
wilaya ya Muleba kufanya za kuthibiti mlipuko huo, baadhi ya wananchi ambao
hawakutaka majina yao yatajwe waliliambia gazeti hili kuwa vifo vya watu
vilivyotokana na mlipuko wa ugonjwa wa malaria kuwa vilichangiwa na uongozi wa
wilaya hiyo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti
hili kuwa baada mlipuko kujitokeza viongozi walikuwa na taarifa lakini
hawakuchukua hatua za haraka za kuthibiti hali hiyo hadi wananchi walipoanza
kueleza kilio chao ndipo viongozi walishtuka, walisema ndio maana wagonjwa
waliopelekwa Rubya kwa matibabu walikosa msaada wa haraka ambao ni pamoja na
madawa.
Walisema wananchi walipokuwa wakifikishwa
hospitalini walikuwa wakilazwa katika hospitali ya Rubya bila msaada wowote, waliendelea
kusema kuwa hali hiyo ndio ilichangia vifo vya watu wengi, walisema wagonjwa
walikuwa wakipewa maji tu.
Walidai kuwa kama uongozi wa wilaya ya Muleba
kama ungechukua hatua za haraka za kuthibiti mlipuko wa ugonjwa huo kwa
kusambaza madawa ya malaria kwa wakati vifo vingepungua sana.
"Ndugu waandishi msidanganywe hata
waliolazwa afya mawodini mkiwaona afya zao sio nzuri uko uwezekano wa kutokea
vifo vingine vingi zaidi, hali ni mbaya sana, muandike taarifa sahihi
msipotoshwe na baadhi wa viongozi wanaotaka kufagilia unga wao" alisema
mmoja wa wananchi.
"Hapa viongozi hasa wa halmashauri ya
wilaya ya Muleba wanapaswa kuwajibika kwa suala hili, mimi binafsi naiomba
serikali ichukue suala hili kwa umakini zaidi kwa kuwa wameonyesha uwajibikaji
mdogo" alisema mwananchi mwingine bila kutaja jina lake.
Kufuatia kuzuka kwa mlipuko wa ugonjwa huo
katika Hospitali ya Rubya imefurika wagonjwa kiasi cha uongozi wa hospitali kulazimika
kuwalaza mgonjwa zaidi ya watatu kwenye
kitanda kimoja.
Katika hatua kuwafariji wanaougua ugonjwa wa
Malaria waziri ardhi nyumba na maendeleo ya makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametoa
msaada wa vyakula vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5.
Msaada ulitolewa na Profesa Tibaijuka ambaye pia
ni mbunge wa jimbo la Muleba kusini ulikabidhiwa na katibu wake wa jimbo hilo la
Muleba Kusini, Denis Mutajwaha alipofika katika hospitali ya Rubya kuwafariji
wagonjwa.
Hii ni mara ya pili mlipuko wa ugonjwa wa
Malaria kuzuka wilayani Muleba, tabribani zaidi ya miaka 5 iliyopita mlipuko wa
ugonjwa huo ulijitokeza na kusababisha vifo vya watu wengi.
No comments:
Post a Comment