Friday, June 28, 2013

IDARA YA MAHAKAMA NCHINI KUSHIRIKIANA NA WANANCHI KATIKA KUBORESHA MAJENGO YA MAHAKAMA ZA MWANZO

 
“Tumekuwa tukiendesha kesi  na kazi za mahakama katika majengo ya ajabu na ambayo hayastaili binadamu kufanyia kazi, mfano kuna mkoa mmoja Idara ya Mahakama imekuwa ikiendesha shughuli zake katika jengo lililokuwa zizi la ng’ombe na mkoa  mwingine chini ya mti.”
Maneno hayo yalisemwa na Kaimu Jaji Mfawidhi Kanda ya Bukoba Mhe. Pellagia Barnaba Khaday alipokuwa akikabidhiwa jengo la Mahakama ya mwanzo katika Kata ya Ijumbi Tarafa Nshamba Wilayani Muleba Juni 15, 2013.
Jengo hilo lilijengwa kwa nguvu za wananchi na kukabidhiwa katika Halmashauri ya Wilaya Muleba na Halmashauri hiyo iliamua kukabidhi jengo hilo katika idara ya Mahakama kutokana uhitaji wa huduma za kisheria katika kata hiyo na kata zingine za jirani.
Akikabidhi jengo hilo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Masswe aliwasistiza wananchi kufuata sheria za nchi ili mahakama hiyo isigeuke kuwa adui kwao pale watakapokuwa wamevunja sheria za nchi na kuhukumiwa.
Kaimu Jaji  Mfawidhi Kanda ya Bukoba Mhe. Pellagia alisema sasa umefika wakati wananchi kuanza kuchangia katika ujenzi wa wa majengo ya mahaka kwani yalisaulika sana na kupelekea majengo mengi hasa ya mahakama za mwanzo kuwa katika hali mbaya sana nchini.
Mhe. Pellagia alisistiza kuwa sasa Idara ya Mahakama imeanza rasmi kushirikiana na wananchi kupitia Halmashauri za Wilaya kuboresha majengo ya mahakama na huduma za mahakama. Aidha alitoa tahadhari kwa wananchi kuacha kuwarubuni Mahakimu na rushwa ili watende kazi zao kwa haki
“Tunatarajia kuanzia sasa kuwaleta Mahakimu wenye shahada ya kwanza kwa hiyo ni mategemeo yetu kuwa kesi nyingi zitamalizikia ngazi ya mhakama za mwanzo. Wananchi wenye uwezo mtaanza sasa kuwaweka mawakili kusimamia kesi zenu katika mahakama za mwanzo.     “Alimazia Mhe. Pellagia.
Ardhi lilipojengwa jengo la mahakama hiyo lilitolewa na mpenda maendeleo Bw. Prosper Rweyendera ambaye pia ametoa bure nyumba za walimu kuishi na kufanya kazi zao, aidha alijenga kituo cha Polisi na kuwapatia nyumba za kuishi.
Aidha nyumba ya Karani na Hakimu tayari zimenjwa katika eneo hilo kinachosubiliwa ni huduma za kisheria tu.
 Mkuu wa Mkoa Akipokea Hati ya Ardhi na Jengo Kutoka Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Muleba Bi Oliver Vavunge Na Baadae Mkuu wa Mkoa alikabidhi nyaraka Hizo kwa Kaimu Jaji Mfawidhi Kanda ya Bukoba. Hayupo Pichani
Kaimu Jaji  Mfawidhi Kanda ya Bukoba Mhe. Pellagia Akitoa Shukrani Baada ya Kukabidhiwa Nyaraka za Jengo na Ardhi Ijumbi.

No comments:

Post a Comment