Saturday, August 22, 2015

WAZIRI MKUU: SERIKALI INATAFUTA SULUHISHO LA DIASPORA KUPIGA KURA



WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali bado inatafuta suluhisho la kudumu litakalowezesha Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) waweze kupiga kura wakiwa huko waliko.

Ametoa kauli hiyo juzi usiku (Jumatano, Agosti 19, 2015), wakati akijibu maswali ya Watanzania waishio Uganda katika kikao kilichofanyika hoteli ya Serena jijini Kampala.

“Serikali tulitamani sana mchakato huu umekamilika mwaka huu ili Watanzania waishio nje ya nchi waweze pia kushiriki uchaguzi mkuu lakini tulipoongea na wenzetu wa NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi), ilibainika kwamba isingekuwa rahisi kupeleka mashine za BVR nje ya nchi wakati huo huo zoezi la uandikishaji likiwa linaendelea hapa nchini…”, alisema.

“Walisema kuna suala la uandikishaji, likimalizika kuna suala la uhakiki wa majina ya walioandikishwa… yote haya yanataka muda na maandalizi ya kutosha,” aliongeza Waziri Mkuu.

Alisema Serikali bado haijakata tamaa na yeye binafsi anaamini jambo hilo linaweza kufanyika kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020 bila matatizo yoyote.

Akigusia kuhusu uandikishaji wapiga kura nchini, Waziri Mkuu alisema lengo la awali lilikuwa ni kuandikisha wapiga kura milioni 24 lakini kutokana na takwimu na uzoefu uliopatikana kwenye nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilishauri lengo la Serikali liwe ni kuandikisha watu milioni 22.

“Lakini kama wengi mlivyosikia, wakati hata hawajamaliza kuandikisha wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam, ambao ulikuwa wa mwisho, tayari tulishavuka lengo la awali la kuandikisha watu milioni 24,” alisema.

Alisema hilo ni jambo la kujivunia kwa sababu tangu mwanzoni, mchakato huo ulikuwa umegubikwa na kelele nyingi na watu walihofia kwamba kwamba zoezi hilo lisingekamilika. “Sote ni mashuhuda, watu wamejiandikisha na sasa wanakamilisha taratibu za uhakiki,” aliongeza.

Waziri Mkuu Pinda aliwasili nchini Uganda Jumatano usiku kwa ziara ya siku moja akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya Chama cha Maskauti cha Uganda (Uganda Scouts Association – USA). Amerejea nchini jana usiku.

Rais Yoweri Museveni ndiye mlezi wa chama hicho na alikuwa amemwalika Rais Kikwete kwenye maadhimisho hayo.

No comments:

Post a Comment