WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
haina kuweka mkakati utakaohakikisha kuwa nchi wanachama zinakuwa na mpango
mahsusi wa kuendeleza viwanda kama ambavyo imekubaliwa kwenye kikao chao
kilichomalizika leo.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 18, 2015), wakati akizungumza na
waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza mkutano wa 35 wa wakuu wa nchi za
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Gaborone,
Botswana.
“Jumuiya
ya SADC kupitia sekretarieti yake itabidi iweke mkakati maamlu wa kufuatilia
kama nchi wananchama imeandaa mapango wa kuendeleza viwanda kulingana na
makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha leo,” alisema Waziri Mkuu ambaye
ameshiriki kikao hicho kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.
Alisema
yeye binafsi amefurahishwa na kupitishwa kwa azimio la uendelezaji wa viwanda katika
nchi za SADC kwani unaendana na juhudi za Serikali ya Tanzania za kukuza uchumi
kupitia uendelezaji wa viwanda vya usindikaji.
“Nimefurahi
kwa sababu azimio hili linaendana na mpango wetu wa kuendeleza viwanda wa mwaka
2015/2016 hadi 2020/2021. Sisi tumelenga viwanda vya kusindika mazao ya
wakulima, wavuvi na wafugaji… kwa hiyo naamnini tutaenda vizuri na mpango mzima
wa Jumuiya hii,” alisema.
Kuhusu
madeni ya michango kutoka kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu
alisema Tanzania iko kwenye hatua nzuri ya ulipaji michango hiyo. “Jana
nilipofika niliulizia suala hilo, nikaambiwa kwamba Tanzania imekwishalipa kwa
kiwango cha kuridhisha. Nilitoa wito wakamilishe kulipa hiyo michango
iliyobakia kwenye maeneo husika,” aliongeza.
Mapema,
Waziri Mkuu Pinda alisoma salamu maalumu mbele ya wakuu wa nchi na washiriki wa
mkutano huo zaidi ya 500, zikiwa ni salamu maalum za kuwaaga zilizotolewa na
Rais Jakaya Kikwete. Rais Kikwete anamaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu na
hatapata nafasi nyingine ya kushiriki kikao cha wakuu wa nchi.
Kikao
kijacho kimepangwa kufanyika Agosti, 2016 nchini Lesotho ambapo Mfalme Letsie
Mswati wa III alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wakuu wa nchi wanachama kwenye
mkutano huo.
Katika
hatua nyingine, wakuu
wa nchi za Jumuiya ya SADC wamechangua
Rais Ian Khama Seretse Khama kuwa mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo.
Katika kikao hicho waliazimia
kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa ya Kifua Kikuu, Malaria na kuazimia
kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwenye nchi wanachama.
Mbali na kusisitiza utunzaji na
uhifadhi wa mazingira, waliazimia pia kila nchi itekeleze mpango wake wa kilimo
ili kuwa na akiba ya kutosha hasa ikizingatiwa hali ya ukame ambayo imezikumba nchi
za kusini mwa jangwa la Sahara na kuashiria uhaba mkubwa wa chakula.
Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea
nchini leo jioni.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment