HALI YA MAANDALIZI YA MAADHIMISHO YA
MASHUJAA KITAIFA JULAI 25, 2013 NA ZIARA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MKOANI KAGERA
Ndugu Wananchi, kama
ambavyo nimewahi kuwajulisha mara nyingi kupitia vyombo vyetu vya habari juu ya
Mkoa wetu wa Kagera kupewa heshima kubwa ya kuandaa maadhimisho ya Siku ya
Kumbukumbu ya Mashujaa kitaifa mwaka 2013, leo napenda kuwajulisha juu ya
maandalizi ya maadhimisho hayo ambayo yataadhimishwa tarehe 25/07/2013 hapa
mkoani kwetu katika Wilaya ya Muleba katika Kambi ya Jeshi la Wananchi Kaboya.
Pia nawajulisha kuwa maadhimisho hayo yataambatana na ziara ya kikazi ya
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkoa wa Kagera.
MAADHIMISHO YA MASHUJAA MWAKA 2013
Ndugu Wananchi, Maandalizi
ya maadhimisho ya Siku ya Kumbumbu ya Mashujaa mkoani Kagera yanaendelea vizuri
kamati mbalimbali za maandalizi zinatekeleza majukumu yake ya mwisho ili
kufanikisha maadhimisho siku ya Alhamisi ya wiki hii tarehe 25 Julai, 2013. Kamati
zinazoandaa maadhimisho hayo ni Kamati ya Mapokezi, Usafiri na Malazi;
Kamati ya Ujenzi Uwanja na Mapambo; Kamati ya Chakula na Afya; Kamati ya Ulinzi
na Usalama; na Kamati ya Burudani, Habari na Uhamasishaji.
Ndugu wananchi, Kwa
kiwango kikubwa maandalizi yote yamekamilika na tunatarajia kuanzia leo kupokea
wageni kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya mkoa, pia nje ya nchi
watakaohudhuria maadhimisho hayo.
Mkoa
wetu umejipanga vizuri kuwapokea wageni wote watakofika mkoani hapa kwa ukarimu
na bashasha kubwa.
Wajibu wa Wananchi
Ndugu wananchi, Napenda
kutumia fursa hii kuwaomba kuwa wakarimu kwa wageni wetu wote tunaowatarajia kuanzia leo kwa kutekeleza majukumu yenu kama Wanakagera kama ifuatavyo;
Ø Kila
mwananchi kuhakikisha maeneo yake na mazingira yanayomzunguka yanaendelea kuwa
katika hali ya usafi kama utamaduni wetu. Pia kumwajibisha mtu yeyote
atakaeonekana anachafua mazingira yetu. Hili ni jukumu la kila mwananchi.
Ø Kila
mwananchi kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha Siku yenyewe ya Kumbukumbu ya
Mashujaa tarehe 25 Julai, 2013 huko
Kaboya Wilayani Muleba. Kwani hatuna
budi kuwakumbuka Mashujaa wetu kwa sababu ya historia ya mkoa wetu kushiriki
katika vita ya kumwondoa adui aliyekuwa amevamia nchi yetu kupitia ardhi ya
mkoa huu mwaka 1978 hadi 1979.
Ø Kila
mwananchi kuhakikisha anaitunza amani na utulivu kama destuli ya mkoa wetu kwa
wakati wote wageni wetu watakapokuwepo hapa mkoani na baada ya maadhimisho ya
Mashujaa. Aidha, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imejipanga vizuri kuhakikisha amani na utulivu vinatawala wakati wote. Kwa
mwananchi yeyote atakayeona viashiria vya uvunjifu wa amani atoe taarifa mara
moja ili taarifa hizo zifanyiwe kazi mara moja.
Wajibu wa Vyombo vya Habari
Ndugu Wananchi, Vyombo
vyetu vya habari vina wajibu wa kuhakikisha vinaendelea kutoa taarifa
mbalimbali kwa wananchi kuhusu Maadhimisho ya Mashujaa kama ambavyo vimekuwa
vikifanya kuanzia mwezi Mei, 2013.
Aidha,
nawaombeni Waandishi, Wahariri na Wamiliki wa vyombo vya habari kutumia fursa
hii kuutangaza mkoa wetu wa Kagera katika sekta mbalimbali za uwekezaji na
fursa mbalimbali zinazopatikana katika mkoa wetu.
Vilevile
nawaombeni Wamiliki wa vyombo vya habari hasa redio zetu za jamii kutoa muda wa kutosha katika vituo vyenu vya redio kurusha habari
na matukio ya Kumbukumbu za Mashujaa papo kwa papo (live coverage) siku ya maadhimisho ili
wananchi ambao hawatapata muda wa kufika Kaboya wazipate habari hizo kupitia
redio zetu za Jamii.
ZIARA YA MHE. RAIS MKOANI KAGERA
Ndugu Wananchi, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye atakayekuwa mgeni Rasmi Katika
Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mashujaa tarehe 25 Julai, 2013. Pia Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika mkoa wetu wa
Kagera.
Ndugu Wananchi, Katika
ziara hiyo Mheshimiwa Rais Kikwete anatarajia kuzindua miradi mbalimbali ya
maendeleo katika mkoa wetu kama ifuatavyo:
§ Kuweka
jiwe la msingi katika ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.
§ Kuweka
jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Kagoma - Rusahunga
§ Kuweka
jiwe la msingi barabara ya kiwango cha lami Kyaka hadi Bugene
§ Kufungua
Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.
§ Kufungua
jengo la kitega uchumi la Chama Kikuu cha Ushirika (KCU Ltd)
§ Kuzindua
mradi wa maji Muleba
§ Kuzindua
kivuko kipya Rusumo (Ngara)
§ Kuzindua
mradi wa usambazaji umeme vijijini Nyaishozi (Karagwe)
§ Kuzindua
Wilaya Mpya ya Kyerwa
Ndugu Wananchi,
Vilevile Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataongea na
wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara katika Wilaya zetu ndani ya
mkoa.
Ndugu Wananchi, nawaombeni
kujitokeza kuanzia tarehe 24/07/2013 uwanja wa ndege wa Bukoba ili kumpokea
Mheshimiwa Rais, pia atakapokuwa anafanya ziara katika Wilaya zetu tujitokeze
kwa wingi kumsikiliza.
Mwisho; Nawatakia
ushiriki mzuri katika kuadhimisha Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa na mapokezi
mazuri ya wageni wetu hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete.
Kagera:
Amani na Maendeleo.
Amani
na Maendeleo; Kagera.
Imetolewa na: Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe
Mkuu wa Mkoa
KAGERA
No comments:
Post a Comment