WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua Mpango wa Kitaifa wa
Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) unaolenga kukuza viwango vya
uelewa kwa watoto wa darasa la kwanza na la pili kwa nchi nzima.
Mpango huo wa miaka mitatu ulioanza kutekelezwa 2014/2015
hadi 2016/2017 umelengwa kuwahusisha watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 13
walio kwenye mfumo rasmi wa elimu na usio rasmi (MEMKWA).
Akizungumza na wadau wa elimu, walimu na wanafunzi
walioshiriki uzinduzi huo jana jioni (Jumamosi, Februari 7, 2015) Waziri
Mkuu Pinda alisema mpango huo ni mkubwa na umeandaliwa mahsusi kujibu
changamoto zilizojitokeza miaka ya nyuma.
Aliwataka watekelezaji wakuu wa mpango ambao ni Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuhakikisha kuwa wanazishirikisha asasi
zisizo za Kiserikali ambazo zinajihusisha na masuala ya elimu.
“Kuna
mashirika mengi yasiyo za kiserikali ambayo ni chachu ya kuhimiza elimu
nchini... jaribuni kuwashirikisha sababu wao ni wadau wazuri sana wa suala hili.
Pangeni utaratibu wa kukaa na hawa wadau na kuwapa mrejesho wa mpango huu mzima,”
alisema Waziri Mkuu.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu aliwataka wahusika wakuu wa mpango waangalie mgawanyo wa
mikoa iliyoingizwa kwenye mpango huo kwa kuzingatia kanda ili kuleta matokeo ya
mtawanyiko badala ya hali ilivyo sasa. “Nimeangalia jinsi mlivyogawa mikoa yenu,
inanipa taabu kidogo... kuna mikoa inahitaji msukumo wa pekee, mikoa ya
wadugaji, mikoa iliyoko pwani ya bahari na maziwa, yote inahitaji msukumo wa
tofauti,” alisema.
Katika
taarifa yao, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilisema mpango huo wa KKK au
LANES (Literacy and Numeracy Support Programme) unafadhiliwa na Ushirika wa Kimataifa wa
Maendeleo ya Elimu (Global Partnership for Education – GPE) na wahisani
wengine.
Wahisani hao ni pamoja na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID)
kupitia mradi wa EQUIP-T unaotekelezwa katika mikoa saba ya Kigoma, Shinyanga,
Mara, Simiyu, Lindi, Dodoma na Tabora; Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo
ya Elimu kwa Mtoto (UNICEF) wanaofadhili utelekezaji wa Mpango wa LANES katika mikoa
ya Iringa, Mbeya na Njombe; na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kupitia
Mradi wa TZ-21 unaotekelezwa katika mkoa wa Mtwara.
Mapema, akisoma taarifa ya mpango huo mbele ya Waziri Mkuu, Kamishna
wa Elimu nchini, Prof. Eustella Bhalalusesa alisema mpango huo umelenga
kuongeza ufanisi katika stadi za KKK, kurahisisha kazi ya walimu wanaofundisha
watoto wa darasa la kwanza na la pili pamoja na kuongeza ushiriki wa jamii
katika kuboresha elimu na hasa ujifunzaji wa stadi za KKK.
Alisema
mpango huo utachangiwa sh. bilioni 150 ambazo zitaingizwa moja kwa moja kwenye
mfuko wa elimu kupitia Wizara ya Fedha.
Alisema maandalizi yote ya utekelezaji wa mpango huu yamekamilika ikiwa ni
pamoja na mtaala wa darasa la kwanza na darasa la pili, muhtasari wa KKK kwa
darasa la I & II, pamoja na Mwongozo wa Mwalimu wa kufundisha kusoma
kuandika na kuhesabu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, FEBRUARI 8, 2015.
No comments:
Post a Comment