WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema uongezaji virutubisho kwenye vyakula umeibua mguso
mpya na kuleta mlipuko baina ya sekta binafsi na sekta za umma (PPP) ambazo zinasimamia
masuala ya afya kwa kiwango kikubwa.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema kazi kubwa zaidi inabidi ifanyike ili elimu ya
kutosha iweze kufikishwa kwa mabilioni ya watu ambao milo yao ya kila siku
haina virutubisho vya kutosha.
Ametoa
kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Septemba 9, 2015) wakati akizungumza na washiriki
zaidi ya 400 kutoka nchi 30 wanaohudhuria mkutano wa kwanza wa kimataifa wa urutubishaji
vyakula ulioanza jana jijini Arusha. Mkutano huo utamalizika kesho, Septemba
11, 2015.
“Bila
kuwa na sera zinazoeleweka na jamii, bila kuwekeza zaidi na bila kuwa na timu
ya wataalamu waliobobea kwenye masuala la chakula, tuko hatarini kupoteza kasi
tuliyoanza nayo na tunaweza tusifanikiwe kutimiza malengo tuliyotarajia,”
alionya Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu ambaye alifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, alisema
urutubishaji wa vyakula unaohimizwa ni uongezaji wa madini na vitamini kwenye
vyakula vinavyosindikwa viwe vya mafuta au nafaka ili kupambana na udumavu na
utapiamlo. Alisema hivi sasa virutubisho vinavyoongezwa kwenye vyakula ni
pamoja na madini ya chuma, zinc, vitamini
A na vitamini B12.
“Uongezaji
wa virutubisho unaendana na kampeni ya siku 1,000 za mwanzo wa maisha ya mtoto
(1,000 days of a child’s life) ambayo inaendeshwa na Serikali yetu kwa
kuzingatia kuwa faida zake zinagusa ukuaji na afya ya mtoto, ukuaji wa ubongo
wa mtoto, ujenzi wa kinga imara za mwili, uelewa mkubwa unaomwezesha mtoto
kufanya vizuri masomoni na uhakika wa maisha marefu ambao unachangia ukuaji wa
uchumi na pato la Taifa,” alisema.
Kuhusu
juhudi za Serikali, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali za
Mitaa imelenga kupanua huduma za urutubishaji wa vyakula vijijini ambako
asilimia 70 ya Watanzania wanaishi. “Mifumo imewekwa ili kusaidia wenye viwanda
vya kusindika nafaka na mafuta waweze kuongeza virutubishi hivyo,” alisema.
Alisema
Tanzania ilianza kampeni za kuongeza virutubisho kama vile madini joto (iodine)
kwenye chumvi tangu miaka ya 90 na matokeo yake hivi sasa hakuna wagonjwa wa goitre kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Hivi
sasa kila kaya inatumia chumvi yenye madinijoto na asilimia zaidi ya 80 ya kaya
zinatumia chumvi ya aina hii. Matokeo yake ni kupungua kwa ugonjwa wa goitre na kufikia chini ya asilimia tano kwa
watoto wenye umri kati ya miaka 6-12 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwenye
miaka ya 1980,” alifafanua.
Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) wa
Masuala ya Kupambana na Njaa, Mfalme Letsie III wa Lesotho alisema suala la
kurutubisha vyakula lisiachwe kuwa la Serikali peke yake bali linahitaji nguvu
ya pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali na hata ikibidi Serikali zote za Bara la
Afrika.
“Vyanzo
vya upungufu wa virutubisho na utapiamlo na vingi na vina njia mbalimbali za
kukabiliana nazo. Lakini hapa nataka nisisitize kwamba, tunahitaji utashi wa
kisiasa kutoka kwa wakuu wa nchi zote duniani na siyo kwa bara la Afrika peke
yake ili suala hili liweze kufanikiwa,” alisema.
“Nikiwa
Balozi wa AU wa kupambana na njaa, ninazitaka nchi zote na Serikali zilizoko
madarakani ziweke sheria mahsusi au sera za kitaifa ambazo zitaweka bayana
suala la urutubishaji wa vyakula kama njia ya kupambana na njaa na pia kumaliza
kabisa tatizo la upungufu wa virutubisho vya kutosha kwenye milo ya kila siku
ya watu wetu,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Naibu Waziri wa
Afya, Dk. Kebwe S. Kebwe
alisema Serikali imelenga kuajiri maafisa lishe kwenye Halmashauri za Wilaya 157
ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa viinilishe kwenye vyakula.
Alisema
kati ya mwaka 2010 na 2013 Serikali imeongeza kiasi cha fedha kutoka sh.
bilioni 19/- hadi sh. bilioni 33/- ili zisaidie kusimamia masuala ya lishe na
urutubishaji wa vyakula.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu Mkutano huo
wa Kwanza wa Kimataifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Alliance for Improved
Nutrition (GAIN), Dk. Marc Van Ameringen alisema mkutano huo unawajumuisha
watendaji kutoka serikalini, taasisi binafsi, vyuo vikuu na taasisi za utafiti
ili kwa pamoja waje na suluhisho la kudumu juu ya urutubishaji vya vyakula kama
njia ya kupambana na njaa na udumavu.
Alisema
wana maeneo matano ambayo wameyalenga yakiwemo uboreshaji wa sheria; utoaji wa
elimu zaidi na ushawishi kwa jamii; haja ya kupata uwekezaji zaidi kwenye eneo
hilo; haja ya kupata msukumo kutoka Serikali za nchi mbalimbali na kuhakikisha
kuwa urutubishaji wa vyakula unaingizwa kwenye mikakati ya kitaifa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment