Wizara imesikitishwa na taarifa za uongo zilitolewa
katika vyombo vya habari kuwa Mhe. Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika uongozi wake wa miaka 10 ametumia Shilingi trilioni 4 kwa
ajili ya safari za kikazi nje ya nchi, ambazo ni wastani wa bajeti nzima ya
wizara kwa miaka mitano (5).
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
inapenda kutoa ufafanuzi kuwa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, kiasi kikubwa kabisa
cha bajeti kuwahi kutengwa kwa ajili ya safari za Viongozi Wakuu yaani Rais,
Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ni shilingi bilioni 50 ambazo zilitengwa kwa
Mwaka wa Fedha 2014/2015 kwa ajili ya Idara ya Itifaki. Kwa miaka mingine yote
wastani umekuwa ni kati ya shilingi bilioni tano hadi 25 kulingana na mahitaji
ya idara hiyo.
Ifahamike kuwa kiasi hicho cha shilingi bilioni 50 ni
bajeti nzima ya Idara ya Itifaki, ambapo kuna fungu maalum kwa ajili ya ziara
za viongozi. Fungu hilo linagharamia makundi makuu matano kama ifuatavyo:
1.
Kundi la Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri
au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
2.
Kundi la Makamu wa Rais wakiwemo Wasaidizi,
Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
3.
Kundi la Waziri Mkuu wakiwemo Wasaidizi,
Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
4.
Kundi la Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka
nje ya nchi wanapotembelea Tanzania; na
5.
Kundi la Wajumbe Maalum wanaokuja nchini
kuleta taarifa muhimu kwa Rais.
Makundi yote haya hugaramiwa na Serikali kupitia Wizara
ya Mambo ya Nje ndani ya bajeti ya Idara ya Itifaki kifungu cha Ziara za
Viongozi.
Aidha uandaaji wa bajeti ya Wizara chini ya Idara ya
Sera na Mipango unahusisha wadau wengine nje ya Wizara kama vile Kamati ya
Bunge ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hupitishwa kila mwaka na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunapenda kuwaatahadharisha wananchi juu ya watu
wanaotoa taarifa za uongo kwa madhumuni ya
kujenga chuki dhidi ya Serikali.
Ikumbukwe kuwa ziara za viongozi zinazoratibiwa na Wizara ya Mambo ya
Nje zina mafanikio makubwa kwa nchi na Watanzania kwa ujumla.
Wizara inaandaa taarifa ya ndefu ya utekelezaji wa
majukumu ya Wizara, changamoto na mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha
miaka kumi ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambayo itatolewa kwa umma
kwa lengo la kutoa elimu zaidi.
MWISHO.
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa
Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa,
No comments:
Post a Comment