Wednesday, September 16, 2015

MWENENDO WA KAMPENI ZA CCM

Hadi jana, tarehe 16 September 2015, Mgombea Urais wa CCM, Dr. John Pombe Magufuli, alikuwa amekwishafanya kampeni katika mikoa 12 na Majimbo 94. Amekwishafanya mikutano mikubwa ya hadhara 76 na mikutano ya barabarani 381. Amekwishatembea, kwa gari, jumla ya kilomita 13,720. Kwa ujumla amekwishakutana, moja kwa moja, na asilimia zaidi ya 30 ya wapiga kura. Kwa kuwa baadhi ya mikutano yetu inatangazwa moja kwa moja na redio za kijamii na luninga, wapiga kura waliopata nafasi ya kumsikia wanakadiriwa kufikia asilimia 70.

Tunafarijika na idadi kubwa ya watu wanaokuja kwenye mikutano ya kampeni zetu. Tunafarijika pia kwamba karibu Watanzania wote wanaopata fursa ya kumuona na kumsikia wamemuelewa na wamepata matumaini ya Tanzania Mpya kupitia kwake. Utafiti wetu wa ndani, tulioufanya kwa kipindi cha siku kumi zilizopita katika majimbo 246 kati ya majimbo 269, unaonyesha kwamba Dr. Magufuli atapata ushindi wa asilimia 69.3 Tunaamini kwamba asilimia hizi zitaongezek kadri Watanzania wengi zaidi wanavyopata fursa ya kumsikiliza Dr. Magufuli na kusikiliza Ilani na sera za CCM.



Kwa upande wa kampeni zetu za Ubunge,  zaidi ya robo tatu ya wagombea Ubunge wa CCM wamekwishazindua kampeni zao na wanaendelea vizuri. Sekretarieti ya Kampeni ya CCM inaanda program maalum ya kampeni
katika majimbo yenye changamoto mahsusi.

Napenda kuchukua fursa hii kuwajulisha wana-CCM kwamba viongozi na makada wengine wa CCM, waliopo madarakani na wastaafu watapita tena, jimbo kwa jimbo, nchi nzima katika siku 30 za mwisho katika jitihada za kuongeza ushindi wa CCM na Dr. Magufuli.

MIDAHALO YA WAGOMBEA

Wiki tatu zilizopita, CCM, na kwa hakika vyama vingine pia, ilipokea mwaliko wa Mgombea Urais wa CCM, Dr. John Pombe Magufuli, kushiriki kwenye mdahalo wa wagombea Urais uliondaliwa na Baraza la Habari Tanzania (Media Council of Tanzania) kwa kushirikiana na taasisi nyingine kadhaa, ikiwemo Twaweza. Dr. Magufuli amekubali kushiriki katika mdahalo huo. Kwa msingi huo, kauli ya UKAWA iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ndugu James Mbatia, kwamba UKAWA inaomba mdahalo ni njia ya kuwahadaa Watanzania tu kwa kuwa mwaliko wa mdahalo ulikwishatolewa mapema kwa vyama vyote na wanaotakiwa kushiriki ni wagombea Urais wa vyama.

CCM inafurahishwa na utamaduni wa midahalo ambao unaanza kujitokeza
katika chaguzi zetu. Na inaamini kwamba midahalo ya Wagombea Urais ni
sehemu muhimu ya kuwashirikisha wapiga kura katika mchakato wa uchaguzi na kuwasaidia waamue nani wamchague kwa misingi ya hoja na sera na sio kwa ushabiki, kwa mihemko, na kwa propaganda. Mdahalo unatoa fursa ya wagombea kuulizwa maswali ya moja kwa moja na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu sera na ahadi zao, fursa ambayo hawaipati kwenye mikutano ya hadhara kampeni.

Hatukubaliani na kauli ya UKAWA kwamba mdahalo usiwe baina ya wagombea
bali uwe baina ya Wenyeviti wa Vyama. Tunaamini hoja hii ni kichekesho. Haijawahi kutokea popote duniani kwenye utamaduni wa midahalo, kwamba wagombea wasishiriki bali watu wengine ndio wafanye midahalo kwa niaba yao.  Tunaamini mdahalo huu unapaswa kuwa baina ya wagombea. Wao ndio wanaoomba dhamana. Wao ndio wanaopaswa kujibu maswali na kufafanua kuhusu ahadi zao.

CCM inaamini kwamba ili mdahalo huu uwe na tija, wagombea Urais wote,
hasa wa vyama vikuu, wawepo na washiriki. Mdahalo hautakuwa na maana
kama mgombea mmojawapo wa vyama vikuu atatengeneza kisingizio ili asishiriki.

UCHAGUZI WA AMANI

CCM inasikitishwa na kauli zinatolewa na baadhi ya viongozi wa UKAWA zenye kuashiria fujo na vurugu. Kauli kwamba kura zitaibiwa hazina msingi wowote. Kauli hizi zinaashiria maandalizi ya kushindwa na maandalizi ya kufanya vurugu baada ya matokeo ya kushindwa.

Utaratibu wa uchaguzi wetu unajulikana na umekubalika na vyama vyote. Kura zinapigwa kituoni na kuhesabiwa kituoni mbele ya mawakala wa vyama vyote, wasimamizi wa uchaguzi na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi. Baada ya kura kuhesabiwa, matokeo yanajazwa katika fomu ambayo kila wakala anasaini na kupewa nakala. Nakala ya matokeo hayo pia inabandikwa nje ya kituo cha kupiga kura. Kila Chama, na kila Mtanzania, kina fursa ya kujumlisha matokeo yake kwenye kila kituo na kupata jumla kuu. Matokeo ya nchi nzima yanajumlishwa mahala pamoja huku kukiwa na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi, pamoja na wawakilishi wa vyama vyote na wao wakiwa na fomu zao za kila kituo nchi nzima.

Tunapenda kuwasihi Watanzania wasikubali vishawishi vya kufanya vurugu. Mara nyingi, viongozi wanaohamasisha vurugu wanakuwa na ulinzi au walinzi au uwezo wa kukimbilia pahala penye utulivu zaidi huku wakiwaacha wafuasi wao katika wakihangaika.

UCHAGUZI NA UMOJA WA KITAIFA

CCM pia inapenda kusisitiza imani yake kwamba uchaguzi haupaswi kutugawa kama taifa. Uchaguzi ni tukio la kupita. Kuna maisha baada ya uchaguzi. Kuna taifa baada ya uchaguzi. Lazima taifa liendelee kubaki moja, tuendelee kubaki wamoja. Tusitoe kauli za kupitiliza zenye mrengo wa kujenga chuki katika jamii na kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu.

Kama Chama kilichoasisi umoja wa taifa letu, tunaendelea kuasa kwamba
wanasiasa wasijinadi kwa misingi ya udini, ukabila wala ukanda. CCM haina mpango kuendeleza mjadala wa kauli ya Mgombea wa UKAWA Ndugu Edward Lowassa aliyoitoa kanisani Tabora tarehe 6 September 2015kwamba nchi ilishapata viongozi Wakatoliki na kwamba sasa ni zamu ya Walutheri kuchukua nafasi hiyo. Tunaamini mjadala huo hauna tija. Tunaamini kwamba Watanzania wengi, wa dini na madhehebu yote, hawaamini katika siasa za namna hii. Tuliamini kwamba UKAWA ingetumia fursa ya mkutano wao na waandishi wa habari jana kuomba radhi kwa Watanzania. Kwakuwa hawakufanya hivyo, tunapendekeza mjadala wa jambo hili ufungwe. Itoshe tu kwamba Ndugu Lowassa amesema hivyo, Tume ya Uchaguzi imemuonya, na yeye hajajitokeza kuomba radhi wala kufafanua. Watanzania wamemjua ni kiongozi wa aina gani na watatoa hukumu yao tarehe 25 Oktoba 2015.
Imetolewa na:-


January Y. Makamba,
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM
MJUMBE WA KAMATI YA KAMPENI YA CCM

No comments:

Post a Comment