WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema wakati Tanzania inajiandaa kutekeleza awamu ya pili
ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano (2016 -2020) ambao unalenga kukuza
viwanda nchini, haina budi kuangalia ni aina gani ya uwekezaji unafaa
kuchukuliwa kwa manufaa ya nchi.
Ametoa
kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Septemba 2, 2015), wakati akizungumza na
mabalozi na wageni mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya miaka 70 ya Uhuru wa
Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam na miaka 50 ya kuanzishwa kwa mahusiano ya
kidiplomasia baina ya Tanzania na Vietnam, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Huu
ni wakati muafaka kwa nchi zetu kuangalia ni aina zipi za uwekezaji zinafaa
kuchukuliwa kwa manufaa ya nchi zetu na wananchi wake. Nitumie fursa hii
kuwakaribisha wawekezaji kutoka makampuni ya Ki-Vietnam waje kuwekeza kwenye usindikaji
wa korosho, utengenezaji wa saruji na viwanda vya nguo,” alisema.
Aliyataja
maeneo mengine ambayo wenye makampuni wanaweza kuwekeza kuwa ni nyanja ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na ujenzi wa nyumba za
kuishi (real estate development).
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuipongeza kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vietnam
(VIETTEL) kwa uamuzi wake wa kutenga dola za Marekani bilioni moja ambazo
zitatumika kuendesha shughuli zake hapa nchini.
“Huu
ni mtaji mkubwa sana, siyo tu hapa Afrika Mashariki na Kati bali hata barani
Asia. Uwekezaji huu utazalisha ajira za moja kwa moja 1,700 na ajira nyingine
20,000 ambazo si za moja kwa moja,” aliongeza.
Kwa upande wake, Balozi wa Vietnam nchini Tanzania,
Bw. Vo Thanh Nam alisema tangu ipate uhuru wake hadi, nchi hiyo
imekwishaanzisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi 185 na wakati huo huo
imekwishaweka mahusiano ya kibiashara na uwekezaji na nchi 220. “Vietnam ni
mwanachama hai katika mashirika ya kimataifa na kikanda zaidi ya 70 yakiwemo
UN, WTO, ASEAN NA APEC,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya Vietnam na Tanzania,
Balozi Thanh Nam alisema mbali ya kujenga mahusiano ya kijamii, kisiasa na
kiuchumi, nchi hizo mbili zimeunganishwa na uwekezaji uliofanywa na kampuni ya
VIETTEL GROUP kwenye sekta ya mawasiliano.
Hafla
hiyo ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Balozi Yahaya Simba na mabalozi wa nchi mbalimbali wakiongozwa na
Balozi Juma Alfani Mpango, ambaye ni Mkuu wa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao
hapa Tanzania.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment