EWURA
Kuanzia
Mwezi Julai mwaka 2014 mpaka Desemba, bei ya mafuta ghafi imekuwa
ikishuka kutoka $110 kwa pipa mpaka $56 kwa pipa. Mporomoko huu wa bei
wa zaidi ya 40% haujaleta unafuu kwa mtumiaji wa kawaida wa mafuta
ikiwemo wenye daladala na kupelekea nauli za usafiri wa umma kupungua.
Leo bado bei ya mafuta kwenye vituo vya mafuta ni tshs 2029 kwa Petroli
na 1909 kwa dizeli, bei ambayo ni karibia ile ile kwa miezi michache
iliyopita.
EWURA,inasemekana,
wamesema kuwa bei za hapa nchini hushuka baada ya miezi 2 kwa sababu
waagizaji huagiza kwa ujumla mafuta mengi zaidi na hivyo kutofaidika na
punguzo la bei. Hata hivyo bei zimeanza kushuka toka mwezi Julai na
hatujashuhudia unafuu wowote kwa wananchi. Ingekuwa bei ya mafuta
imepanda tungeona bei zimepanda mara moja na sababu za kununua ' bulky'
huwa hazitolewi.
Ni kweli
kwamba Tanzania hununua mafuta yaliyosafishwa na hivyo bei inayoshuka
sio hiyo. Lakini hao wasafishaji hununua mafuta ghafi yenye bei ndogo
hivi sasa kwa hiyo ni dhahiri lazima bei za pampu zipungue. Vile vile ni
kweli kwamba thamani ya shilingi ya Tanzania imeporomoka hivyo wananchi
hawawezi kuona unafuu wa bei ya mafuta kwa sababu hununuliwa kwa fedha
za kigeni na kuuzwa kwa Sarafu yetu. Hata hivyo kasi ya kushuka kwa bei
ya mafuta ni 40% wakati shilingi imeshuka kwa chini ya 10%. Katika hali
ya kawaida na kwa kutumia mfumo wa kukokotoa bei wa EWURA, angalau bei
ya mafuta ingeshuka kwa kati ya 15% and 25%.
Ni
dhahiri mamlaka za nchi na hasa EWURA wanapaswa kueleza kwa umma ni
Kwanini bei za mafuta hazishuki kulingana na bei ya bidhaa hiyo katika
soko la Dunia. Wananchi wana haki ya kujua na kama hakuna Maelezo basi
bei hizo zishuke na wananchi wafaidike na punguzo hilo.
Zitto Kabwe, Mb
No comments:
Post a Comment