WAZIRI
MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi wa vitengo na wakuu wa
taasisi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) wapate nakala ya hansard ya hotuba ya Rais Dkt. John
Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la 11, waisome na kufanyia kazi maeneo yote
aliyoyaainisha.
“Katibu
Mkuu hakikisha umepata hansard ya
hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge na uhakikishe kila mkurugenzi
ana nakala na kila mmoja wenu lazima ahakikishe anafanyia maeneo ambayo Mheshimiwa
Rais ameyaainisha. Ni lazima tuelewane ni nini tunapaswa tufanye,” alisema.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Novemba 24, 2015) wakati akizungumza na wakuu
wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwenye
mkutano uliofanyika ofisi ndogo ya TAMISEMI, barabara ya Kivukoni, jijini Dar
es Salaam.
“Ninatamani
kuona mabadiliko ya utendaji kazi Serikalini katika kipindi kifupi. Natamani
kila mmoja asiridhike na uzembe unaofanywa huku chini. Ni nyote ni wataalamu,
kwa hiyo mnapaswa kudhirisha elimu yenu na ujuzi mlionao,” aliwasisitizia
Wakurugenzi hao.
Alisema
kila mkurugenzi na mkuu wa taasisi anapaswa kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa
kazi kwenye sekta yake kwani hilo litasaidia kukidhi matarajio ya Watanzania ya
kuona mabadiliko ya utendaji kazi kwenye Serikali ya Awamu ya Tano. “Ninyi
wakurugenzi siyo desk officers bali
ni field officers. Nataka muweke
utaratibu wa kwenda vijijini mkasimamie watu wenu, pia mhimize uadilifu,
uaminifu na weledi wa kazi,” alisisitiza.
“Mambo
ninayotaka mhimize watendaji waliopo chini yenu ni pamoja na haya yafuatayo:
muda wa kuripoti kazini uzingatiwe, muda wa kukaa kazini uzingatiwe, utokaji
kazini kwenda kwenye chai na chakula cha mchana udhibitiwe, na mipango na
malengo ya kazi kwa siku ni lazima yafikiwe,” alisema.
“Tunataka
kujua mtumishi amefanya nini tangu alipoingia ofisini. Suala siyo kukaa tu
ofisini, kwani kuna mtu anakaa ofisini, hajaenda hata kunywa chai lakini
ukiuliza amefanya nini hupati jibu la kueleweka. Sisi kama vongozi wao ni
lazima tujue wanafanya kazi gani wanapokuwa maofisini,” alisisitiza.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameitisha kikao ofisini kwake kesho saa 4
asubuhi akitaka kupatiwa taarifa ni kwa nini mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART)
haujaanza kazi hadi sasa. “Kesho saa 4 asubuhi Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu DART
na watendaji wako mje ofisini. Nataka kupata maelezo ni kwa nini mabasi
hayajaanza kazi hadi leo, je ni lini yataanza kazi, je ni nani anakwamisha. Na hata
kama ni sheria, ni kwa nini tusiziharmonise ili kuondoa hivyo vikwazo,?” alihoji
Waziri Mkuu.
“Ninataka
kupata haya maelezo kwa sababu Watanzania na hasa wana-Dar es salaam,
wamesubiri kwa muda kuona mradi ukianza kazi ili uondoe kero ya usafiri. Wao
wanajua anayehusika ni TAMISEMI,” aliongeza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na watumishi na viongozi wa TAMISEMI, Katibu Mkuu wa OWM-TAMISEMI,
Bw. Jumanne Sagini alimweleza baadhi ya mafanikio na changamoto ambazo wizara
hiyo imekabiliana nazo katika utendaji wake wa kazi.
Kuhusu
ujenzi wa vyumba vya maabara kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya
sayansi, Bw. Sagini alisema vyumba hivyo vimeongezeka kutoka 247 mwaka 2005/2006
na kufikia 6,161 mwaka 2014/2015. Pia alisema vyumba
4,228 viko kwenye hatua za kukamilika ujenzi wake.
Kuhusu
utengaji wa madirisha ya kuhudumia makundi yenye msamaha kama wazee na watu wenye
ulemavu hospitalini na kwenye vituo vya afya, Katibu Mkuu alisema nayo
yameongezeka kutoka madirisha 5,074 mwaka 2010 na kufikia 7,903 mwaka 2014/2015
sawa na ongezeko la asilimia 55.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
No comments:
Post a Comment