Monday, November 23, 2015

HOTUBA YA MHESHIMIWA MAJALIWA KASSIM MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA KWANZA WA BUNGE LA KUMI NA MOJA, DODOMA TAREHE 20 NOVEMBA, 2015



1.      Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu
kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu vizuri
ya Mkutano wa Kwanza wa Bunge la Kumi na Moja ulioanza tarehe 17
Novemba, 2015. Nimefarijika kuwa kazi zote zilizopangwa katika ratiba
yetu tumezikamilisha kwa muda mfupi na kwa umahiri mkubwa.

2.      Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii ya awali kukupongeza
wewe binafsi, Kwanza kwa kuchaguliwa na Wananchi wa Jimbo la Kongwa
kuwa Mbunge wao na Pili, kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi za kishindo
kuwa Spika wa Bunge la Kumi na Moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Nina imani utaliongoza Bunge hili Tukufu na kukidhi kiu ya
Watanzania ya kutaka Bunge hili litekeleze majukumu yake vizuri kwa
weledi na umakini mkubwa wa kuwawezesha kupata maendeleo endelevu.

3.      Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya ngu hii fupi napenda kutumia
nafasi hii kumshukuru tena Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani kubwa aliyoionesha
kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Namwombea Mungu akubariki na kukujalia afya njema na nguvu
ya kuwatumikia Watanzania. Nami nakuahidi kuoa ushirikiano na
kutekeleza yale yote uliyonielekeza. Aidha, naomba niwashukuru tena
Waheshimiwa Wabunge kwa kunithibitisha kuwa Waziri Mkuu wa Kumi na
Moja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kura nyingi hapa Bungeni
kwa zaidi ya asilimia 73. Hii inaonyesha imani kubwa mliyonayo juu
yangu nami ninawaahidi kwamba nina imani kubwa juu yenu.

4.      Vilevile, nawashukuru wananchi wote wa Jimbo la Ruangwa kwa kuwa na
imani nami na kunichagua kuwa mwakilishi wao. Napenda kukishukuru
Chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua kugombea Ubunge katika
Jimbo la Ruangwa na kushiriki katika Kampeni zilizoniwezesha kushinda
na kuwa Mbunge wa Jimbo. Bila Wananchi wa Ruangwa na Chama changu
nisingekuwa na sifa ya kuwa Waziri Mkuu leo.

5.      Ninawashukuru Wazazi wangu kwa malezi na miongozo mbalimbali
waliyonipa ambayo imeniwezesha kufikia hatua hii leo. Ninamshukuru
Mwenza wangu kwa ushirikiano, ushauri na uvumilivu wake kwa muda wote
ambao nilikuwa nafanya kazi za utumishi wa umma. Bila yeye, naamini
nisingekuwa hata na hamu ya kushiriki siasa.

6.      Mheshimiwa Spika, nimeendelea kupokea salam za pongezi  kutoka  kwa
 marafiki,  ndugu  na Watanzania wengine. Nawashukuru sana!! Ninajua
kazi iliyo mbele yangu ni  nzito na  yenye  majukumu  mazito,  lakini
kutokana na imani kubwa ushirikiano mliyonionesha na kwa msaada wa
Mungu naamini nitaiweza. Ninachowaomba wote ni ushirikiano wenu. Nami
ninaahidi nitafanya kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu kuwatumikia
Watanzania wote na sitowaangusha. Awamu ya Tano ya Uongozi wa Nchi
yetu ni ya Kazi tu. Mheshimiwa Rais ameshaonesha mwelekeo. Nami
nitaitekeleza Kaulimbiu hiyo kwa nguvu zangu zote. Nampongeza sana
Mheshimiwa Rais!

7.      Mheshimiwa Spika, hivi punde Mheshimiwa Rais ameeleza kwa kina
kuhusu wajibu wetu katika kujenga Nchi yetu. Nimpongeze sana
Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake nzuri ambayo ndiyo mwongozo wetu
katika kuanza kutekeleza majukumu yetu. Kama Kiongozi wa Shughuli za
Serikali Bungeni, naomba niseme machache kwa yale aliyoyasema
Mheshimiwa Rais na wajibu wetu kama Wabunge.

8.      Mheshimiwa Spika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina
jukumu moja kubwa la kutunga Sheria. Sisi kama Wabunge, hiyo itakuwa
ndiyo kazi yetu ya msingi. Lakini ni kazi inayotakiwa kufanywa kwa
weledi na umakini mkubwa. Nakumbuka Rais Mstaafu, Mzee Benjamin
William Mkapa wakati akifungua Bunge Jipya la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania siku kama ya leo tarehe 20 Novemba, 2000 alitupa Methali ya
Kilatini inayosema:

“Mabaya wayafanyayo watu huendelea baada ya wao kuondoka Duniani.
Wanaua baada ya wao wenyewe kufa kwa hisia ya hoja walizozijenga
wakiwa hai, na kwa sheria walizozitunga.” mwisho wa kunukuu.

9.      Tunapoanza kazi hii muhimu, naomba Waheshimiwa Wabunge tukumbuke
maneno ya methali hii katika kutekeleza majukumu yetu hasa hili la
kutunga Sheria. Nami nawaombea kila la kheri na fanaka tuwe na busara
na hekima katika kutekeleza jukumu hili muhimu la utungaji sheria.

10.     Mheshimiwa Spika, kazi nyingine kubwa ya Wabunge kwa maoni yangu
ni kuwa karibu na Wananchi waliowachagua. Kuna ukweli kwamba, kama
Mbunge anafanya kazi yake vizuri, ataweza kuwa karibu na wananchi
waliomchagua kwa kuwaunganisha na Serikali na kufikisha mawazo yao
Serikalini. Aidha, Mbunge mzuri ni yule anayeweza kuwaeleza Wananchi
kile ambacho Serikali imepanga kukifanya na jinsi ya kutumia
rasilimali, fursa, mipango na taratibu zilizopo za Serikali kuboresha
maisha yao. Ninakumbuka maneno ya Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akifungua rasmi Bunge la Kumi la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapa Dodoma tarehe 30 Desemba, 2005,
alisema na nanukuu:-

“Ninyi Waheshimiwa Wabunge, ndio macho na masikio ya Wananchi.
Mmeaminiwa na kuheshimiwa. Naomba kila siku mnapoingia au kutoka
katika Bunge hili, mnapozungumza humu ndani au mnaposikiliza wengine
wakizungumza, mnapokuwa macho au mnapofumba macho kutafakari kwa kina,
kila mara mkumbuke imani na heshima hiyo kubwa mliyopewa na Wananchi.”
mwisho wa kunukuu.

11.     Maneno haya ya hekima ukiyasoma kwa undani yamebeba hoja na ujumbe
mzito sana kwetu. Ni hoja ambayo tunatakiwa tujikumbushe kila mara
katika kipindi chote cha miaka mitano cha uhai wa Bunge letu.

12.     Mheshimiwa Spika, nafahamu kuwa Mheshimiwa Mbunge anakuwa na
majukumu mengi, lakini kubwa ninalolijua ni utumishi wako kwa
waliokupa kura. Wananchi wana mategemeo makubwa kuwa kila mmoja wetu
atajitahidi kuwa nao ili ashiriki kutatua changamoto mbalimbali za
maendeleo. Mheshimiwa Rais, kwenye hotuba yake ameliezea vizuri jambo
hili.

13.     Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wanalo pia jukumu la
kuisimamia na kuishauri Serikali ili kuhakikisha kuwa matatizo na kero
mbalimbali  za wananchi zinatatuliwa. Aidha, kazi ya Mbunge ni
kuisimamia Serikali kuhakikisha kuwa inatoa mchango wake kikamilifu
katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kutumia nguvu kazi na
rasilimali tulizonazo. Ni matarajio ya Serikali kuwa itapata taarifa
na ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge juu ya maeneo yanayohitaji
kupewa msukumo ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa letu. Kwa
upande wake, Serikali itafanyia kazi taarifa na ushauri huo. Lengo ni
kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi
na kuiingiza katika mkondo wa uchumi imara, endelevu, unaokua na wa
Taifa linalojitegemea. Jukumu hilo ni letu sote Watanzania. Kila mmoja
akifanya kazi kwa kujituma, nina imani Taifa letu litasonga mbele na
maisha ya watu wetu yatabadilika. Mwanazuoni mmoja, Bwana Ralph Bunche
aliandika:

To make our way, we must have firm resolve, persistence and tenacity.
We must gear ourselves to work hard all the way. We can never let up!

14.     Mheshimiwa Spika, anachosema Mwanazuoni huyu ni kwamba, tukitaka
kusonga mbele kwa mafanikio lazima tuweke dhamira ya kweli na tukomae
nayo kwa kufanya kazi zaidi na kwa bidii zote na kwa uadilifu wote.
Mheshimiwa Rais ameshatupatia nguvu mpya ya kwamba “Hapa ni Kazi tu”.
Tuweke dhamira na pasiwe na yeyote wa kuturudisha nyuma.

15.     Mheshimiwa Spika, narudia kuwaombeni kwamba sasa uchaguzi
umekwisha, wote tuseme kwa dhamira moja kuwa “yaliyopita si ndwele
tugange yajayo”. Twendeni sasa tukashirikiane na Wananchi kufanya
kazi. Turejeshe ushirikiano na mshikamano. Tuwasaidie na kuwaongoza
Wananchi kutatua matatizo yao. Tusibaki tunatafuta mchawi kumbe mchawi
tumemuanzisha sisi wenyewe kwa tabia zetu.

16.     Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuomba ushirikiano wa
Watumishi wote wa Serikali katika kutekeleza Ahadi za Mheshimiwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati na baada ya Kampeni za
Uchaguzi, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Dira ya Maendeleo. Tufanye
kazi kwa bidii na kuwatumikia Watanzania kwa kasi na umakini wa hali
ya juu. Kila mtendaji afanye kazi kwa sababu hatutakuwa na uvumilivu
kwa wazembe.

17.     Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wote waliotuwezesha
kukamilisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Kwanza wa
Bunge la Kumi na Moja kwa ufanisi mkubwa. Ni dhahiri tumeanza vizuri
na ninaamini tutaendelea vizuri!

18.     Mheshimiwa  Spika, baada ya kusema hayo, nawatakia safari njema na
naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liahirishwe sasa hadi
Jumanne, tarehe 26 Januari, 2016, saa Tatu Asubuhi litakapokutana tena
hapa mjini Dodoma.

19.     Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment