SERIKALI
imewasimamisha kazi watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao
jana iliamriwa kwamba watahamishiwa mikoani. Watumishi hao ni Bw. Anangisye
Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw. Robert Nyoni.
Uamuzi
huo umetolewa leo (Jumamosi, Novemba 28, 2015), na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim
Majaliwa ili kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma zinazowakabili. Kama ilivyo kwa
wenzao sita waliosimamishwa kazi jana (akiwemo aliyekuwa Kamishna Mkuu), nao
pia hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya nchi hadi uchunguzi utakapokamilika.
“Kazi ya kuwachunguza ilianza jana ileile na
sasa, tumeona hawa watu wanapaswa kuwa nje ya utumishi ili kupisha uchunguzi
ufanyike kwa uhuru zaidi,” alisema Waziri Mkuu.
Pia
Waziri Mkuu amemuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Philip Mpango atekeleze
maagizo hayo kwa kuwaandikia barua watumishi hao.
Jana
mchana, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kushtukiza kwenye bandari ya Dar es
Salaam akiwa na nia ya kukagua namna
shughuli zinavyoendelea kwenye bandari hiyo hasa kwenye maeneo ya kupokelea
mizigo kutoka nje ya nchi.
Katika
kikao kilichofanyika bandarini hapo na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa
Serikali, Waziri Mkuu aliamua kuwasimamisha kazi maafisa watano na TRA kutokana
na ‘upotevu’ wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.
Waziri
Mkuu alisema upotevu huo unasababishwa na mchezo unaofanyika baina ya wafanyabiashara
na watumishi wa TRA ambao wanaruhusu makontena kupita bila kulipiwa ushuru na
hivyo kuikosesha Serikali mapato.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA
WA MAGOGONI,
No comments:
Post a Comment