Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa
kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne
kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha
matokeo, uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi. Majimbo hayo ni
Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe. Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo
haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa
zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa
haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria. Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo
Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM
imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya. Tunataka
sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa. Bado tunaendelea
kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa
uliobadilisha matakwa ya wapiga kura. Hata hivyo, tunakiri kwamba kwenye maeneo
mengi tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko,
tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili
tubaini makosa na kuyarekebisha.
MAONI YA
WAANGALIZI WA UCHAGUZI
CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi.
Tumefarijika kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu
ulikuwa wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba
changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza
kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa. Tumepokea mapendekezo
waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi
kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za
waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo
yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu
viongozi wanaowataka.
MALALAMIKO
YA UKAWA
Tumesikia malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia
mkutano wao na waandishi wa habari jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba
hawakubali matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo, matokeo ya
Ubunge wanayakubali na, kule wanakoshinda, wanayasheherekea. Tunashangazwa
kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo iliyoandaa uchaguzi wa
Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na sheria na taratibu
zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo walizosaini wakala wao kwenye
vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika sehemu (columns) tatu: Urais, Ubunge
na Udiwani. Mawakala wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya kupiga kura. Wameanza kuwa na matatizo na matokeo haya
baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama mwelekeo ungekuwa tofauti, wangekuwa
na imani na Tume, wasimamizi na taratibu zote.
Tunaomba ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga
demokrasia yetu na kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa
anayeshindwa kunyanyua simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza. Nafasi ya
mwisho aliyonayo Mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea heshima katika jamii
yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku Dkt. Magufuli
atakapotangazwa mshindi.
Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na
kutengeneza sera bora na kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa
nchi, ndio njia zetu pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi
wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita ambao
tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali. Nguvu na utashi
wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu.
Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni,
tutawapata madiwani, wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape
nafasi watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za
kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za vurugu na
maandamano hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani kitendo cha wafuasi wa UKAWA
kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi. Amani ya nchi hii ina thamani kuliko hitaji la
madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana
haki ya kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza
mitaani wafanye vurugu na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli
za watu wengine. Tunawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida
huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu.
January Makamba
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
No comments:
Post a Comment