CCM inapenda kutoa taarifa kuhusu
masuala kadhaa kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wake na kwa umma wa
Watanzania.
Kufunga Kampeni
CCM
itafunga kampeni zake kwa utaratibu mpya na kwa kishindo. Kampeni za CCM
zitafungwa Kitaifa kwa mikutano mikubwa ya kampeni katika mikoa mitano.
Mikutano hiyo itaongozwa na viongozi wa CCM Kitaifa waliopo madarakani na
wastaafu. Mikoa hiyo na viongozi watakaoongoza mikutano hiyo ni kama ifuatavyo:
1. Mwanza
– Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli,
Mgombea Urais, na Ndugu Samia Hassan Suluhu, Mgombea Makamu wa Rais
2. Tanga –
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM
3. Mbeya –
Ndugu Benjamin William Mkapa, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
4. Mtwara –
Ndugu Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
5. Kigoma – Ndugu
Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
6. Kilimanjaro –
Ndugu Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu
7. Mara – Ndugu Joseph Warioba, Mjumbe wa
Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu
Kati
ya leo na kesho, maeneo mengine yanaweza kuongezeka. Mikutano hii itaanza saa
sita mchana na itarushwa, yote kwa pamoja, kwa matangazo ya moja kwa moja ya
vituo vya televisheni vitano na vituo vya redio 67. Vilevile, watakaohudhuria
katika mikutano hii wataunganishwa moja kwa moja na mkutano wa Mwanza, alipo
Mwenyekiti, Mgombea na Mgombea Mwenza, na wataweza kusikiliza hotuba ya Dkt.
Magufuli moja kwa moja kupitia screens zitakazokuwa katika viwanja vyote hivi
saba.
Namna
hii ya ufungaji wa kampeni itakuwa ni ya kihistoria, na inadhihirisha nguvu ya
CCM inayoiwezesha kufanya mikutano mikubwa ya kampeni kwa siku moja katika
maeneo mbalimbali nchini. Lakini pia tutaweka historia katika tasnia ya
utangazaji wa televisheni hapa nchini kwa kutangaza na kuunganisha kwa pamoja
matukio saba kwa wakati mmoja.
Kwa
upande wa Dar es Salaam, tutafanya mkutano mkubwa wa ufungaji wa kampeni za
Mkoa wa Dar es Salaam, katika Uwanja wa Jangwani, kesho, Ijumaa, tarehe 23
Oktoba 2015. Siku ya Jumamosi, tarehe 24 Oktoba 2015, Wagombea Ubunge katika
majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam watafunga kampeni katika maeneo ya majimbo yao
kwa namna mahsusi.
Tathmini ya Kampeni
Kama
Chama, tumeridhika na ubora na ukubwa wa kampeni tulizofanya licha ya
changamoto za hapa na pale. Dkt. Magufuli na Ndugu Suluhu wamefanya kazi kubwa,
na kwa bidii kubwa, na maarifa makubwa. Wamekuwa barabarani kwa siku 57
wakifanya mikutano kati ya 8 hadi 12 kwa siku. Imani yetu ya ushindi
inatokana na kazi kubwa waliyofanya. Pia, CCM inawashukuru viongozi, wapenzi wa
washabiki wake – wa makundi mbalimbali ya kijamii - kote nchini kwa kazi kubwa
ya kampeni waliyoifanya.
Kutokana na kazi kubwa na nzuri
iliyofanyika, na kutokana na mwenendo wa tafiti huru na tafiti zetu za ndani,
CCM inategemea ushindi wa asilimia zisizopungua 69.
Uchaguzi wa Amani
CCM
haitachoka kuendelea kusisitiza uchaguzi wa amani na utulivu. Sisi kama chama
kikubwa cha siasa nchini, chenye wafuasi wengi zaidi, na chenye dhamana ya
uongozi wa dola, tutatimiza wajibu wetu wa kuhimiza utulivu kwa wapenzi,
washabiki na wanachama wetu. Tunawataka na wenzetu wafanye hivyo.
Kauli
za wenzetu kwamba kura zitaibiwa ni kauli za kutojiamini na kujiandaa kufanya
vurugu. Kauli za kwamba washabiki wa UKAWA wakishapiga kura wabaki vituoni
kulinda kura si kauli za wanaotaka uchaguzi wa amani.
Kwa
utaratibu wetu wa uchaguzi, utaratibu wa pekee kwa Chama kulinda kura zake ni
kwa kupitia wakala wa vyama waliopo kwenye kila kituo cha kupiga kura na wenye
nguvu na mamlaka ya kisheria ya kushuhudia zoezi zima, kuanzia kupiga kura,
kuhesabu kura hadi kutangaza matokeo. Kura zinapigwa na kuhesabiwa vituoni
mbele ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Mawakala wa vyama na Waangalizi wa Uchaguzi wa
ndani na nje ya nchi. Mawakala wa vyama na Wasimamizi wa Uchaguzi wanaweka
sahihi kwenye fomu za matokeo, na matokeo hayo yanatangazwa na kubandikwa
kwenye kituo. Kwenye kituo kikuu cha Tume cha kujumlisha matokeo, mawakala wa
vyama pia huwepo na Tume hujumlisha matokeo kutoka kwenye fomu za matokeo za
vituo vya nchi nzima zilizosainiwa na mawakala wa vyama kwenye kila
kituo. Kwa viongozi wa UKAWA kuwaambia watu waingie barabarani au
kuvizunguka vituo vya kupigia kura eti ili kulinda kura hakuna maana yoyote
zaidi ya kutafuta namna ya kuhalalisha fujo, vurugu na uporaji na kuwazuia watu
wengine, hasa wanawake, kupiga kura. Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama
vizuie hili jambo kwa sababu halina nia njema.
Mkakati
wa UKAWA ni kufanya vurugu baada ya kushindwa na kutengeneza mazingira ya
mgogoro wa kisiasa ili Jumuiya ya Kimataifa iingilie kati na kupendekeza
kugawana madaraka. Mkakati huo hautafanikiwa. Tunaviomba vyombo vya ulinzi na
usalama vihakikishe ulinzi na usalama wa watu wote na mali zao siku ya uchaguzi
na baada ya uchaguzi.
CCM
haitakubali hata kidogo ushindi wake kuhojiwa au kutiliwa shaka kwa sababu tu
ya vurugu zilizoanzishwa na watu wengine.
Siku
ya Jumamosi, CCM itatangaza namba maalum za simu kwa Watanzania wote ili siku
kabla ya Uchaguzi, siku ya Uchaguzi na mara baada ya uchaguzi, waweze kupiga
simu au kutuma ujumbe pale watakapokuwa wanabaini au kushuhudia vitendo vya
kuvuruga amani na kuvuruga utaratibu mzima wa Uchaguzi.
Kupokea Matokeo
CCM
imeweka utaratibu wa kupokea matokeo kwa kutumia Mawakala wake moja kwa moja
vituoni na kupitia mtandao wa Chama. CCM inategemea kuwa na matokeo ya Uchaguzi
nchi nzima ifikapo saa nne usiku, siku ya Uchaguzi, tarehe 25 Oktoba
2015.
Imetolewa na:
January
Makamba
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
MJUMBE WA KAMATI YA KAMPENI
22 OKTOBA 2015