Monday, July 13, 2015

MWALIMU GEORGE RUBEIYUKA APANIA KUMUONDOA MBUNGE WA JIMBO LA BUKOBA MJINI BALOZI KHAMIS KAGASHEKI



Na Audax Mutiganzi,Bukoba +255 784 939 586

Sasa kumekucha, asiye na mwana aeleke jiwe, nimeanza makala yangu hii  kwa kutanguliza usemi huu hii ni kwa kuwa tunatarajia kuona mengi  kufuatia mchauano mkali unaoanza  wa  kuwapata wale wataopeperusha bendera za Chama Cha Mapinduzi (CCM)  wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini kote mwezi Octoba, mwaka huu katika ngazi za udiwani na ubunge.

Mchuano uliopo sasa  ni baina  ya wale  wanaotaka kuendeleza juhudi za kutetea viti vyao vya ubunge na udiwani wanavyovishikilia kwa sasa  kwa nguvu zote na wale wanaovikodolea macho viti hivyo baada ya  kuonyesha nia ya kutaka kuviwania.

Hali hii inawachanganya sana wale ambao wanafanya kila njia ya kutetea viti vyao kwa mara nyingine tena, ninachikielewa kiongozi ambaye alitekeleza ahadi yake vizuri baada ya kupewa ridhaa ya uongozi na wananchi hapaswi kuwa na wasiwasi hata wakijitokeza watu zaidi ya 1000 wanaotaka kuchuana naye.
Ninachokielewa mimi na kukifikiri pia ni kwamba kiongozi anayepaswa kuwa na wasiwasi pale anapojitokeza mtu anayetangaza nia ya kuchuana naye ni yule aliyeshindwa kuwatumukia wananchi vizuri hasa kwa kukwamisha maendeleo yao kwa maslahi yake binafsi bila kutanguliza maslahi ya wananchi.

Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu tumeanza kuona mengi na tutaendelea kuona mengi, hii ni kwa sababu kuna baadhi ya viongozi  wanaotaka kulinda viti vyao kwa kutumia mbinu ya kuwajenga hofu wale wamaowahisi wanataka kutangaza nia ya kuchuana nao.

Baadhi ya viongozi wamekuwa na kawaida ya kutumia maneno makali wanapokuwa kwenye majukwaa, wengine wanathubutu kusema kuwa watahakikisha wanawapasua  vifua au kuwavunja meno wale wote watakaojitokeza kuchuana nao, kauli hizi mara kwa mara zimekuwa zikitafsiriwa vibaya na wananchi.

Mara nyingi binadamu huwa hawapendi kukubali matokeo na lazima  tuelewe kuwa  kila siku sio siku ya jumapili, ninachotaka kukielezea inapotokea ukapingwa tena wa mtu wako  karibu au yule ambaye mnazaliwa tumbo moja  ni lazima ujie kwamba kuna tatizo kwa maana hiyo ni lazima ujitathimini  ili uweze kupata majibu ya haraka, kama unadhamilia kufanya jambo ama urudi nyuma au usonge mbele.


Ninachokielewa nafasi za uongozi hasa zile zinazopatikana kwa ridhaa ya wananchi hazipatikani kwa njia iliyorahisi, hapa naongelea nafasi ya ubunge ambayo inaliliwa na watu wengi, nafasi hii sio ya kung’ang’ania, kwa kuwa sio ajira rasmi na wala sio nafasi za urithi kwa kuwa inatokana na matakwa ya wananchi.

Jambo linalowashangaza wananchi walio wengi ni pale wanapomuona mbunge anamjengea chuki mtu yoyote anayejitokeza kumnyanganya tonge mdomoni, inashangaza pale unapomuona mbunge na kwa kushirikiana na wapambe wake wanapofikia hatua ya ya kuwatolea vitisho baadhi ya watu wanaotangaza nia ya kuwania viti vya ubunge.

Ninachoshangaa ni kauli za baadhi ya wabunge ambao kawaida yao uchaguliwa na wananchi kwa   kutumia nguvu kubwa pale wanapotamba na kuwaeleza wananchi kuwa hakuna mtu yoyote ambaye anaweza kupambana nao huku akielewa wazi kwamba nafasi zao ya ubunge ziko rehani.

Katika karne ya sasa wananchi hawadanganyiki tena, hii kwa sababu wanajua kuchambua mchele na pumba, ninachotaka kukisema ni kwamba wananchi walio wengi sasa hawadanganywi, wanatambua haki yao hasa kwa kuwapigia kura wabunge  wanaofaa tofauti  na zamani ambapo walikuwa wakichagua wabunge  kwa kuongwa pombe, sukari na vijipesa vidogo.

Kwa maana hiyo mbunge  anapochaguliwa anapaswa kuwajibika zaidi hasa kwa kutetea maslahi ya waliomchagua, pale anaposhindwa kuwajibika vizuri na akagundua mvuto wake kwa wananchi unafifia hapaswi kulazimisha hivyo hana budi kuachia ngazi na kuwaachia wengine uwanja ili wapate nafasi ya kujimwaga, habari ndoo hiyo, kugang’ania hakuna maana.

Katika mkoa wa Kagera ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baadhi ya makada wa chama hicho wameanza kuonyesha nia yao ya kushiriki kwenye kura za maoni kuwania nafasi ya ubunge kupitia katika chama hicho.

Baadhi ya makada wa CCM ambao wameonyesha nia ya kuwania nafasi ya ubunge kupitia katika chama hicho ni pamoja na Julius Rugemalila, Dr. Mazima, Dr Diodorus Kamala na Kyombo wanaotaka kushiriki kwenye kura za maoni kwa lengo la kumg’oa mbunge wa jimbo la Misenyi Asumpta Mshama.

Tukienda katika jimbo la Karagwe tunamkuta Karim Amri AmirI anayetaka kuchuaa na mbunge wa sasa wa jimbo hiloGozibert Brandes, na katika jimbo la  Ngara tunamkuta Willison Gashaza anayetaka kuwania nafasi ya ubunge kupitia CCM kwa lengo la kumg’oa Ntukamazina na tukienda katika jimbo la Bukoba vijijini tunamkuta Nazir Kalamagi anayetaka kuwania kiti cha ubunge kinachoshikililiwa na Jasson Rweikiza.

Katika jimbo la Bukoba mjini  Mwalimu George Joseph Lubaiyuka ni miongoni mwa makada wa CCM ambao wameishaonyesha nia ya kutaka kuwania kiti cha ubunge kinachoshikiliwa na mbunge wa sasa katika jimbo hilo Balozi Khamis Kagasheki kupitia chama hicho.

Mtangaza nia huyo ni katibu wa uchumi na fedha katika wilaya ya Bukoba mjini, pia ni kada wa CCM wa muda mrefu na ambaye amewahi kushika nyazifa mbalimbali ndani ya  chama hicho,  baadhi ya nyazifa hizo ni pamoja na mjumbe wa halmashauri kuu CCM wilaya ya Bukoba mjini na mkoa wa Kagera.

Nyazifa nyingine ndani ya Chama hicho mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Bukoba mjini na mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa, nyazifa ambazo aliwahi kuzishika ni pamoja na kuwa mjumbe wa kamati ya utekelezaji wa jumuia ya wazazi wa wilaya ya Nyamagana iliyoko mkoani Mwanza, mjumbe wa kamati tendaji wa jumuia ya wazazi na katibu elimu na uchumi na malezi wa kata ya Pamba jijini Mwanza.

Mwalimu Lubeiyuka ni mtumishi wa serikali, ni afisa elimu vifaa na takwimu katika halamashauri ya willaya ya Misenyi, mwalimu huyo ni msomi mwenye shahada ya uzamili ya elimu katika masaula ya utawala, mipango na sera ‘masters’.

Kwa sasa anaendelea kusoma shahada ya kwanza ya sheria kupitia chuo kikuu huria nchini, mwalimu ambaye amewahi kushika nyazifa nyingi za uongozi ambazo ni pamoja na urais wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu huria kituo cha Kagera, mjumbe wa kamati ya ushauri ya chuo kikuu huria na waziri wa elimu wa chuo kikuu taifa.

Akitangaza vipaumbele vyake baada ya kuonyesha nia yake Lubeiyuka anasema akibahatika kuwa mbunge wa jimbo la Bukoba mjini atahakikisha anavunja makundi yanayochangia migogoro inayokwamisha maendeleo katika jimbo hilo.

Amesema migogoro katika jimbo hilo katika manispaa hiyo inayokwamisha maendeleo kuwa inachangiwa na baadhi ya wanaotaka kugang’ania nafasi za uongozi kwa hisia kwamba wanaobuni mipango ya maendeleo watanyang’anya tonge mdomoni.

Lubeiyuka anasema kuwa hakuna kiongozi yoyote anayeweza kuleta maendeleo kwa juhudi zake binafsi, anasema maendeleo yanaletwa na juhudi ya pamoja, “ukiona mtu anataka kuwaletea maendeleo wananchi maendeleo kwa kutumia juhudi zake binafsi ujue huyo anataka kuwaweka mfukoni mwake” anasema.

Akizungumzia suala la elimu amnasema kuwa katika jimbo la Bukoba mjini akiwa mbunge atahakikisha anachagua shule 2 za sekondari za kata, anasema katika shule hizxo kwa kushirikiana na wadau atahakikisha anajenga vyumba vya madarasa ya kidato cha tano na sita.

Anasema atafanya hivyo ili kuwaongezea nafasi wanafunzi katika jimbo hilo wanaofaulu vizuri masomo yao ya kidato cha nne na kukosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano kutokana na uchache wa shule za sekondari za serikali zilizoko hapa nchini.

Lubeiyuka anasema iwapo atakuwa mbunge wa jimbo la Bukoba mjini pia anatarajia kuanzisha mfuko wa jimbo. Anasema mfuko huo utawahudumia zaidi watoto wanaofaulu wanaofaulu vizuri masomo yao ya elimu ya msingi ambao wazazi wao wana uwezo mdogo kiuchumi.

Katika hatua nyingine amesema mfuko huo utasadia kuboresha mazingira mazuri ya walimu ambapo utakuwa ukitumika kutoa zawadi kwa walimu ambao wanafunzi wao wanafnya vizuri na utatumika kufanya kazi ya kuwazadia wanafunzi wanaofaulu vizuri.

Mtangaza nia huyo huyo ameahidi kufanya mkakati wa kutengeneza ajira zisizo rasmi kwa vijana zitakazowawezesha kujiajiri wenyewe badala ya kuwa tegemezi ndani ya jamii, amesema vijana wanatengenezewa ajira wanakuwa wanajiepusha na vitendo vinavyojiingiza ambavyo ni pamoja na uzuruuaji.

Anasema katiia jimbo la Bukoba mjini vijana wamesahalika kabisa na ndio maana wakati mwingine unakuta wanashabikia vyama vya upinzani ambavyo haviwezi kuwapa manufaa, anaendelea kusema kuwa katika kutengeneza ajira ya vijana kuwa atashirikiana na wadau mbalimbali.

Lubeiyuka anasema ni vigumu kabisa mtu kutengeneza ajira ya vijana kwa kutumia fedha ya mtu binafsi anayoitoa toka  mfukoni, anasema kutengeneza ajira ya vijana kunahitaji nguvu ya pamoja, anaendelea kusema mtu anayetengeneza ajira kwa vijana kwa kutumia fedha yake ya mfukoni anakuwa anatengeneza chuki kwa kuwa ajira ya fedha ya mfukoni haiwezi kumfikia kila kijana kwa maana hiyo ni lazima itolewe kwa ubaguzi.

Ameahidi kuimarisha mshikamano ndani ya CCM, na pia ameahidi kushirikiana na viongozi wa chama hicho katika suala zima la kutoa maamuzi yanayohusiana na masuala ya maendeleo yanayogusa maslahi ya wananchi, anasema yeye atakuwa na tofauti na wabunge wengine.

Mtangaza nia huyo anasema atahakikisha anatafuta ufumbuzi wa migogoro ambayo imeikumba manispaa ya Bukoba ambayo imekwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa inagusa maslahi ya wananchi ambayo ni pamoja na ujenzi wa soko kuu la Bukoba, ujenzi wa standi kuu ya mabasi ya Kyakailabwa na upimaji wa viwanja wa viwanja 5,000.

Anasema endapo akichaguliwa hataendekeza majungu, atakuwa na chuki na hatatukana watu ,badala yake atafanya kazi ya kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na kwa uadilifu mkubwa hadi pale atakapowavusha,. “uwezo wa kuongoza ninao, nia ya kuongoza ninayo na karama ya kuongoza ninayo na sina doa lolote” anasema.

Lubeiyuka anasema kamwe hatatoa ahadi ambayo atashindwa kuitekeleza sambamba na wabunge ambao wamepita katika jimbo la Bukoba mjini ambao walishindwa kutimiza ahadi zao,anasema  hakuna mtu anayeweza kutamba kuwa jimbo hili amelitoa mbali, “ jimbo hili lilikuwepo na wabunge wengi wamepita na wamefanya mengi, anayetamba kuwa jimbo amelitoa mbali anawadanganya wananchi kwa lengo la kujitafutia umaarufu”anasema.

Anasema  siasa za kuwalaghai wananchi kwa kitu wanachokiona kwa macho zimepitwa na wakati, mtu  mwenye nia ya kuwatumia wananchi ni lazima atangulize ukweli ili wananchi waupime na wautolee maamuzi, “nafasi ya ubunge haitaki majaribio” anamaliza.

Baadhi ya wananchi walioongea juu ya mtangaza nia huyo wanasema, anafaa kuwania kito cha ubunge katika jimbo la Bukoba mjini kwa kuwa ni msomi mzuri, mtu mwenye uelewa na mchapakazi, Idrisa Bingileki ni mkazi wa kata ya Kashai ambaye anasema mtangaza nia huyo ndiye chaguo la wengi kulingana na hali ya upinzani toka kwenye vyama vingine vya siasa.

Bingileki anasema jimbo la Bukoba mjini linahitaji mgombea mwenye mvuto kama Lubeiyuka, anasema Mwalimu huyo anapendwa na lika zote,” tumechoka na siasa za matusi zinazotolewa na baadhi ya viongozi tunaowachagua, nafasi za ubunge sio za urithi sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko” anasema.

“Hatudanganywi tena huu ni wakati wa kuchambua pumba na mchele, nawashauri CCM wasifanye kosa, wakiamuangusha Mwalimu Lubeiyuka watakuwa wanafanya kosa kubwa ambalo watalijutia, vijana wana usongo mkubwa na wana siri kubwa wamepania kufanya maajabu katika uchaguzi wao, chonde… chonde msituletee mgombea ambaye hauziki” anamaliza.




No comments:

Post a Comment