WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na hita za kuchemshia maji kwa
wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya moto na atakayekutwa atachukuliwa
hatua kali.
“Kuna tabia ya baadhi ya
wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa vya kienyeji vya
kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari kwani linaweza kusababisha
ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 17, 2016) katika
harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Lindi yaliyoungua
moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka
huu.
Katika ajali hiyo shule imeathirika
kwa asilimia 34 ambapo vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo
na jengo la maabara ya kemia na fizikia yameungua na kusababishia hasara ya sh.
milioni 682.78.
Waziri Mkuu amesema kwa
namna ambavyo majengo hayo yameungua ni vema yakavunjwa na kujengwa upya ambapo
aliwataka kutumia nafasi hiyo kwa kujenga jengo la ghorofa ili kutumia eneo
dogo kwa kujenga madarasa mengi.
Pia alimuagiza Mkuu wa mkoa
wa Lindi, Godfrey Zambi kuhakikisha fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo
zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Harambee ilihudhuriwa na mke
wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa, mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, mama Salma
Kikwete, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego pamoja na wadau wa maendeleo na
wanafunzi waliosoma shule hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhandisi Ramo Makani.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka taasisi mbalimbali
nchini kufunga vifaa vya kuzimia moto katika majengo yao kwa ajili ya kuvitumia
pindi ajali za moto zinapotokea.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
No comments:
Post a Comment