WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji
safi na salama hasa vijijini kwa sababu nchi zake bado hazijamudu kuunganisha
huduma hiyo katika maeneo hayo.
Kufuatia hali hiyo, Waziri
Mkuu amewataka wataalamu wa masuala ya maji watafute njia sahihi itakayowezesha
kutatua tatizo hilo kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya maji vilivyoko.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo
jana (Jumatatu, Julai 18, 2016) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Julius Nyerere jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa 10 wa
Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika (AMCOW) ambao unaokwenda sambamba na
maadhimisho ya Wiki ya Maji Afrika.
“Tunategemea baada ya
kumazika kwa mkutano huu wataalamu wetu wataondoka na maazimio mazuri ya
kumaliza tatizo la maji katika Bara letu kwa kutumia mito na maziwa ili
kufikisha maji kwa wananchi,” alisema.
Akizungumzia kwa upande wa Tanzania
alisema, suala la maji limepewa
kipaumbele hata katika bajeti ya mwaka huu na kwamba Serikali itahakikisha maji
yanapatikana katika maeneo yote ili kutimiza sera yake ya kila mwananchi kupata
maji umbali usiozidi mita 400.
Kwa upande wake Rais Mstaafu
wa Kenya Mwai Kibaki ambaye ni Mjumbe Maalumu wa UNESCO kwa ajili ya masuala ya
maji Barani Afrika alisema maji ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi, hivyo wataalamu
wanatakiwa kuhakikisha huduma hiyo inapatika katika maeneo yote.
Mkutano huo wa siku tano unahudhuriwa Mawaziri wa Maji
kutoka nchi 45 za Afrika na unaongozwa na Waziri wa Maji na Mazingira wa
Senegal Amadou Mansour Faye ambaye ni Rais wa AMCOW.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment