*Aibukia kitengo
cha mita za kupimia mafuta Kurasini
*Akuta
mafundi wakizitengeneza, akuta zimejaa kutu
*Ataka
barua ya maelezo ifikapo saa 11 leo jioni
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara ya ghafla kwenye kitengo cha upimaji mafuta
bandarini (Oil Flow Metres) na kukuta zimejaa kutu baada ya kutelekezwa kwa
miaka zaidi ya mitano. Pia alitembelea mita za kupimia mafuta zinazoendelea kujengwa
Kigamboni.
Aidha,
Waziri Mkuu amempa saa nne tu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA),
Bi. Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita
hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita na amletee barua hiyo
ofisini kwake ifikapo saa 11 leo jioni.
“Nataka
unieleze ni kwa nini ulitoa maelekezo ya kufunga mita hizo, na kwa nini jana
uliamua kubadili uamuzi huo? Ni kwa nini umeamua kuchukua maamuzi haya baada ya
kupokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms) wakati mita zimekaa bila kufanya kazi kwa
miaka mitano? Ni kwa nini umeamua kufanyia kazi ujumbe wa sms wakati unajua Serikali
inafanya kazi kwa maandishi rasmi?” alisema Waziri Mkuu.
“Umesema
mlikuwa mnatumia utaratibu wa kupima kwa kijiti. Huu hauna uhakika na huwezi kutegemea
taarifa ya mtu mwingine au kuingia kwenye meli ya mtu na kuanza kuchukua vipimo
hadi ujiridhishe. Nataka kujua ni kwa nini mlikuwa na utaratibu wa ku-bypass
mafuta ili yasipite kwenye mita za kupimia mafuta? Ni kwa nini umetoa amri
zianze kutengenezwa jana na siyo mwaka 2012 au 2013?” alihoji Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu alisema mita hizo za Kurasini zilinunuliwa na Serikali kwa gharama za dola
za marekani milioni 1.2 (wakati huo) na haiwezekani kuacha kuzitumia wakati
watu wanachezea mifumo na kuongeza mianya ya kupoteza mapato kwa Serikali.
Ameagiza mita hizo zianze kufanya kazi mara moja.
Wazir
Mkuu alisema matumizi ya mita hizo yaliafikiwa na Serikali baada ya kubaini
upotevu mkubwa wa kodi kwenye mafuta yanayoingizwa nchini na baada ya kuona
hakuna tija ya kuendelea na ukadiriaji au kupokea taarifa za waagizaji peke yao.
Waziri
Mkuu ambaye aliwasili Kurasini leo saaa 4: 30 asubuhi (Alhamisi, Februari 11,
2016) kwenye kitengo hicho kilichopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty), alikagua
mita hizo na kisha kwenda kukagua meli iliyokuwa ikishusha mafuta bila kutumia mita
hiyo ya kupima mafuta yanayopokelewa kwa sababu mafundi walikuwa bado
wanaendelea na ukarabati.
Akiwa Kurasini, Waziri Mkuu alielezwa na Bibi Chuwa kwamba
mita hizo zilianza kufanyiwa ukarabati jana na leo asubuhi moja imekamilika
ambayo ni ya kupokelea mafuta ya petroli. Ya dizeli ilikuwa inafunguliwa na mafundi
na kukutwa imejaa kutu sababu ya kutotumika kwa muda mrefu.
“Hii
ya dizeli imefunguliwa leo na ile ya mafuta ya kula, haijawahi kufanya kazi tangu
ilipofungwa mwaka 2011,” alielezwa Waziri Mkuu na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari,
Eng. Aloyce Matei.
Alipoulizwa
ni kwa nini aliamua kuzifungia mita hizo ziisifanye kazi, Bi. Chuwa alijibu kuwa
alifikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kwamba zinawapunja wateja. Hata
hivyo, hakufafanua ni wateja gani au wa aina gani.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea na
kukagua mita mpya za kupimia mafuta ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo
zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).
Akiwa
hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba ujenzi huo ambao ulianza miezi nane
iliyopita, unatarajiwa kukamilika ifikapo katikati ya mwezi Machi, 2016. “Tunajitahidi
kazi hii ikamilike ifikapo katikati ya mwezi ujao,” alisema Eng. John Bura,
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BQ Contractors Ltd ambayo inasimamia ujenzi
wa mita hizo.
Vilevile, Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya
kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na
kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya
TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia bainaya Serikali na kampuni ya
Oryx Energies.
Katika
ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja
kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu
Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya
mwezi mmoja.
“Natoa
mwezi mmoja hili bomba liondolewe kwenye mfumo huu na kama yapo mabomba mengine
pia yaondolewe,” alisema huku akionyesha karatasi iliyokuwa mfukoni kwake yenye
mchoro unaobainisha kuwa kuna bomba jingine la inchi 10 limeungwa kinyemela
kwenye bomba kuu.
“Kila
mmoja anapaswa aje kuchukua pale kwenye manfold ili tujue nani kachukua
nini. Msajili wa Hazina hili ni eneo lako na wewe unamiliki TIPER kwa asilimia
50, hebu simamia hili. Ninyi TPA leteni mapendekezo yenu Serikalini ili tuone
tunaweza kudhibiti vipi vitendo kama hivi,” alisema Waziri Mkuu.
Pia
alimtaka Msajili wa Hazina, Bw. Lawrence Mafuru awasiliane na Mwanasheria Mkuu
ili waangalie upya mkataba na umiliki wa matenki hayo uwe chini ya Serikali kwa
asilimia 100 ili mafuta yanayoagizwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja
(Petroleum Bulk Procurement Agency) yaweze kuhifadhiwa huko.
Mapema, Waziri Mkuu ambaye alifuatana na
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alikagua eneo
la manfold
ya Mamlaka ya Bandari iliyopo Kigamboni na kukuta ni kampuni nne tu zenye
matenki Kigamboni ambazo zinachukua mafuta yao hapo.
Kampuni
hizo ni HASS, WORLD OIL, LAKE OIL na MOIL. TIPER haikutaka kufuata mfumo huo
licha ya kuwa nafasi ya kufanya hivyo ipo. Kampuni nyingine zenye matenki yake
nchi kavu, zinachukulia mafuta kwenye manfold ya Kurasini.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
No comments:
Post a Comment