SERIKALI
imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini
(WMA) kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana
na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.
Waliosimamishwa
kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na
Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye
anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.
Akitangaza
uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo (Ijumaa, Februari
12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm
Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.
“Katibu
Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi.
Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika.
Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.
Waziri
Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi ili
wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika hatua rasmi
zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.
Waziri
Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache
kutumiwa mara moja.
Jana
(Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini
(Kurasini Oil Jetty) na kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu
dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).
Pia
Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold)
iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya
mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya
Serikali na kampuni ya Oryx Energies.
Katika
ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja
kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu
Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya
mwezi mmoja.
“Jana
niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo
huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold
kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
No comments:
Post a Comment