WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema tatizo
la rushwa barani Afrika limesababisha bara hilo lipoteze dola za Marekani
bilioni 150 kila mwaka.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne,
Machi 8, 2016) wakati akihutubia wajumbe wa mkutano wa tano wa Bunge la Afrika
Mashariki (EALA) linaloendesha vikao vyake jijini Dar es Salaam. Mkutano huo
ulioanza Machi 6, utamalizika Machi 18, mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk.
John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema rushwa imechangia kwa kiasi kikubwa
kurudisha nyuma maendeleo ya Jumuiya hiyo. "Rushwa yaweza kuwa kwa njia
kuhonga fedha, kupata fedha kwa kula njama, kujipatia fedha kwa njia za
udanganyifu, ama kwa njia za vitisho," alisema.
"Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja
wa Afrika (AU), rushwa na urasimu vimeainishwa kuwa ni vikwazo vikubwa vinavyochangia
kuchelewesha ufanyaji wa biashara kwenye mipaka ya nchi za Jumuiya yetu,"
alisema.
Amesema sekta binafsi inachukuliwa
kama injini ya maendeleo na ukuaji wa uchumi na akatumia fursa hiyo kuipongeza
jumuiya ya wafanyabiashara wa Afrika Mashariki kwa kuandaa kanuni za kiutendaji
ambazo zimelenga kuhamasisha uadilifu
kwenye ufanyaji biashara unaozingatia haki za binadamu, sheria za kazi,
utunzaji mazingira na vita dhidi ya rushwa.
Akizungumzia kuhusu uondoaji wa
vikwazo visivyohusisha kodi (non-tariff barriers) kama njia mojawapo ya
kuimarisha biashara kwenye jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema kwa upande wa
Tanzania, vizuizi vya barabarani kwenye barabara kuu ya Kaskazini vimepunguzwa kutoka
50 hadi vitano.
Alivitaja vizuizi vitano vilivyobakia
kuwa ni vile vilivyopo kwenye mizni ya Mikese (Morogoro), Nala (Dodoma), Njuki
(Singida), Mwendakulima (Shinyanga) na Nyakahura (Kagera).
"Sheria ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya uondoaji wa vikwazo visivyohusisha kodi ilipitishwa Machi 2015 na
sasa hivi inaendelea kusainiwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pamoja na mambo mengie, nia ya sheria hii ni kuondoa vikwazo vinavyosababisha
uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, kurahisisha
sheria za biashara ndani ya Jumuiya yetu," alisema.
Akizungumzia kuhusu miradi ya
uwekezaji ya Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema miradi ya ujenzi wa barabara
inahitaji kiasi cha dola za marekani bilioni 20; ukarabati na upanuzi wa njia
za reli unahitaji dola za marekani bilioni 30; uendeshaji wa mashirika ya ndege
na viwanja vya ndege unahitaji dola za marekani bilioni 15; uendelezaji bandari
na usafiri wa majini unahitaji dola za marekani bilioni 10; utekelezaji wa
miundombinu ya nishati inahitaji dola bilioni 5 ambavyo kwa pamoja vinahitaji
dola marekani bilioni 80.
Alisema kuwepo kwa shughuli
mbalimbali za kiuchumi ndani ya jumuiya hiyo, kunaifanya Jumuiya ya Afrika
Mashariki kuhesabika kuwa ni jumuiya yenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani
Afrika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMANNE, MACHI 8, 2016.