Tuesday, January 05, 2016

MAKATIBU WAKUU WAPYA OFISI YA WAZIRI MKUU WAANZA KAZI RASMI LEO




PICHA NO. 1
Katibu Mkuu Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. FlorenS Turuka ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (wa pili kulia) akisitiza jambo wakati makatibu wakuu wapya wa Ofisi ya Waziri Mkuu walipokutana na Menejimenti ya Ofisi hiyo (hawapo pichani) leo, tarehe 4 Januari, 2016, kulia kwake ni Katibu Mkuu (Bunge) Mussa Uledi, (wa kwanza kushoto) ni Katibu Mkuu (Kazi na Ajira) Erick Shitindi na (wapili kushoto) ni Katibu Mkuu (Sera) Dkt. Hamis Mwinyimvua.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PICHA NO.2
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwasikiliza makatibu wakuu wapya (hawapo pichani) wakati makatibu wakuu hao (hawapo pichani) walipokutana na Menejimenti hiyo leo, tarehe 4, 2016 Januari katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dar es salaam.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PICHA NO.3
Katibu Mkuu (Kazi na Ajira), Erick Shitindi akisisitiza jambo wakati wa kikao na  Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu (hawapo pichani) alipowasili katika Ofisi hiyo na makatibu wakuu wapya wengine wa Ofisi hiyo , leo, tarehe 4 Januari 2016,  (kulia kwake ) ni, Katibu Mkuu (Sera) Dkt. Hamis Mwinyimvua.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PICHA NO.4
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwasikiliza makatibu wakuu wapya (hawapo pichani) wakati makatibu wakuu hao (hawapo pichani) walipokutana na Menejimenti hiyo leo, tarehe 4 Januari, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dar es salaam.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PICHA NO.5
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwa na Makatibu wakuu wapya Katibu Mkuu, (Bunge) Mussa Uledi, (wa pili kushoto) pamoja na aliye kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo ambaye sasa ni Katibu Mkuu Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. FlorenS Turuka (wa tatu kutoka kushoto), Katibu Mkuu (Kazi na Ajira), Erick Shitindi (katikati) na Katibu Mkuu (Sera) Dkt. Hamis Mwinyimvua (watatu kutoka kulia) mara baada ya makatibu wakuu hao kukutana  na Menejimenti hiyo leo, tarehe 4 Januari, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KIWANDA CHA TUMBAKU MKOANI RUVUMA NA KUWASIMAMISHA KAZI VIONGOZI WA CHAMA CHA USHIRIKA CHA SONAMCU



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kusindika  tumbaku  cha mkoani Ruvuma na kuwasimamisha kazi viongozi wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika cha SONAMCU.

Akizungumza  jana jioni(Jumanne, Januari 5, 2016), katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Ndogo ya Songea, wakati alipokutana na wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Namtumbo, Wananchama wa Vyama Vya Ushirika vya Mkoa wa Ruvuma, viongozi wa Mkoa pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.

Waziri Mkuu amesema, Serikali ina dhamira ya kufufua kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONAMCU, na lengo la kutembelea kiwanda hicho ni katika utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli la kufufua viwanda nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea maeneno mbalimbali ya kiwanda hicho na kukagua mitambo iliyokua ikitumika kusindika tumbaku, kabla kiwanda hicho kuzimwa miaka kadhaa iliyopita  baada ya kukosa malighafi za kuendelea na uzalishaji.

Pia, amemtaka Afisa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bibi. Stela Lugongo kuandaa na kuwasilisha kwake mkakati wa kufufua kiwanda hicho cha kusindika tumbaku, na baadae kuwasimamisha kazi viongozi wote wa Chama Kikuu cha Ushirika cha SONAMCU waliohusika na tuhuma hizo na kutaka wafikishwe Mahakamani.

“Serikali imeazimia kufufua viwanda, hasa vile ambavyo havina wawekezaji vimebaki vyenyewe, Tunahitaji kujua namna ya kuvifufua”. Alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa pia, amesikiliza  na kujibu kero mbalimbali za wakulima wa tumbaku wa Mkoa huo, ambao walilalamikia  mfumo wa Vyama vya Ushirika na namna ambavyo vyama hivi vimekua vikiwaibia fedha zao  hadi kushindwa kuendelea kulima zao la tumbaku na kukosa masoko ya mazao yao.

Aidha, Waziri Mkuu amewasihi wakulima kuwa watulivu na kusubiri maamuzi ya Mahakama baada ya kuwa viongozi wa Chama cha Ushirika SONAMCU ambao wamehusika na wizi wa fedha za wakulima kiashi cha Shilingi milioni 800 kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014 tayari wamefikishwa Mahakamani na uchunguzi unaendelea. Pia, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu kukutana na wakulima hao ili kupatia ufumbuzi matatizo yao.

Aidha, ametoa wito kwa wakulima kuendelea kulima zao la tumbaku kwa kuwa linaongeza pato la mtu mmoja mmoja, linasaidia kuchangia pato la Mkoa na kukua kwa uchumi wa nchi. Amewashauri wakulima kuunda  na kuviendesha Vyama Vya Ushirika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Waziri Mkuu amemaliza ziara yake mkoani Ruvuma, atafanya majumuisho ya ziara hiyo leo, kabla ya kuagana na viongozi wa Chama na Serikali na kurejea jijini Dar es Salaam.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU AKAGUA JENGO LA MAKAO MAKUU YA HALMASHAURI YA WILAYA YA SONGEA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wialaya ya Songea lilipo katika kijiji cha Lundusi, Wilaya ya Peramiho mkoani Ruvuma.

Alipowasili  jana katika eneo hilo alikutana na viongozi wa jadi ambapo  Mzee Daniel Gama  alimkabidhi  ngao na silaha ikiwa ni ishara ya kumkaribisha kijijini hapo, pia alipata fursa ya kutazama ngoma ya mila ya kabila la Wangoni.

Mara baada ya kukagua jengo hilo  la ghorofa,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lundusi Bwana Rajabu Mtiula amesema jengo hilo lenye  ofisi 50, vyoo 4, ukumbi mkubwa 1 na kumbi ndogo 2, ambapo mradi huo umetekelezwa kwa fedha za mfuko wa Mradi wa Maendeleo na Serikali. Hadi sasa Serikali imetoa kiasi cha zaidi ya  shilingi bilioni 200 na utekelezaji wake umekamika kwa 85%, hivyo wanatarajia kuanza kutumia jengo hilo mwezi Februari, 2016.

Akizungumza  jana  (Jumatatu, Januari 4, 2016)  na wananchi wa kijiji cha Lundusi, Waziri Mkuu, amewapongeza   wananchi  wa Lundusi kwa hatua hiyo ya maendeleo na kusema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono ujenzi wa jengo hilo.

Waziri Mkuu Majaliwa, ametaka kuwepo na mikakati ya uboreshaji wa eneo hilo kwa kusogeza huduma karibu ili kuvutia watu zaidi katika eneo hilo.

Naye, Waziri wa Nchi  Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Uratibu, Ajira na Walemavu  Jenista Mhagama  ametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli na Waziri Mkuu kwa kuchaguliwa na kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.

Pia, ameishukuru Serikali kwa kusaidia kujenga jengo hilo, na pia ameeleza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo ikiwemo wakulima kutofaidika kwa bei ya soko ya kuuza mahindi, kutokuwepo na umeme na maji.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza Waziri Jenista kufuatilia kero hizo kwa Wizara husika na baadae kuleta mrejesho kwa wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa anaendelea na ziara mkoani Ruvuma, leo siku ya jumanne (Januari 5, 2016)  atatembelea na kukagua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kuongea na Watumishi wa hospitali hiyo  na baadae ataongea na Watumishi wa Umma.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU AKAGUA MAGHALA YA WAKALA WA HIFADHI YA TAIFA YA CHAKULA (NFRA) KANDA YA SONGEA


Waziri Mkuu  Kassim  Majaliwa amekagua  maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea, wakati akiendelea na ziara yake mkoani Ruvuma.

Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala hiyo, wadau wa kilimo pamoja na wananchi jana, (Jumatatu, Januari 4, 2016) nje ya majengo ya Wakala mara baada ya kukagua mahindi yaliyohifadhiwa katika maghala  ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , mkoani Ruvuma amesema  kufuatia taarifa ya kuwepo na baadhi ya maeneo yenye njaa nchini, Serikali imetoa tamko kuwa hakuna mtanzania atayakekufa kwa njaa.

Ambapo, Serikali  kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa imeweka mikakati ya  kukabiliana na  tatizo la  njaa kwa kutoa msaada wa chakula katika maeneo yanayokabiliwa na njaa.

 “Ni wajibu wangu kuhakikisha nasimamia vizuri hili, nimeona hali ya uhifadhi  wa chakula, tunayo mahindi ya kutosha lakini hakuna sehemu ya kuhifadhi chakula” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa ameendelea kwa kusema uwezo wa maghala hayo yaliyopo chini ya Wakala Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea yana uwezo wa kuhifadhi tani 29 pekee   na Songea  inauwezo wa kuzalisha zaidi tani 70 hadi 80.

Pia , ameagiza  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , kuanzia mwaka huu kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa pamoja Wakuu wa Wilaya  kuanzisha  vituo vya kununulia mahindi  na kuhakikisha magunia yanawafikia wakulima katika vituo hivyo ambapo wataweza kuhifadhi mahindi  na  kuuza  kwa bei ya kwenye soko.

Waziri Mkuu  pia, ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea ,kutumia teknolojia ya kisasa ya uhifadhi wa chakula, kuandaa utaratibu maalum utakaozuia msongamano wa  malori  yanayosubiri kupata huduma ya kununua mahindi  nje ya majengo ya Wakala na kukamilisha miradi itakayosaidia Wakala kuwa na fedha za kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake, Meneja Hifadhi wa  Chakula kanda ya Songea, Bwana. Morgan Mwaipaya amesema kati ya maghala 33 ya kuhifadhi mahindi nchi nzima, Songea ina maghala 6 kati ya hayo. Hivyo, Wakala imeweka vipaumbele vyake ambavyo ni  pamoja na kutoa chakula cha msaada kwa maeneo yenye matatizo ya njaa, kuongeza upatikanaji wa mahindi ili kuzuia kupanda kwa bei ya chakula mwaka 2015 – 2016, Wakala kununua na kuhifadhi  mahindi katika maeneo yaliyozalisha zaidi na kuzingatia sehemu ya sehemu ya akiba ya chakula na kuuza kwa wakulima, mawakala pamoja na Wakala wa Chakula duniani (World food program).

Amesema Wakala imeandaa mikakati ya mbalimbali ikiwemo  kuongeza  uwezo  wa tani 24600 hadi tani  45000 kwa mwaka 2014- 2017, kuboresha mfumo wa utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya stahili ya TEHAMA na kutumia fursa za mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za kifedha ili kuendesha shughuli za uwezeshaji I kiwemo kuelimisha taratibu za ununuzi kwa mawakala.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Songea, Mheshimiwa Leonidas Gama amesema   wakulima wachache wamekua wakiuza mahindi yao kwa bei ya soko,  wengi wao wamekua wakiuza mahindi kwa mawakala kwa bei ya shilingi 150 hadi 200  kwa kilo na  wakala wakiuza kwa shilingi 500 kwa Serikali. Ambapo amemuomba  Waziri Mkuu  kutatua tatizo la soko la mahindi kwa wakulima. Hata hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima kuendelea kuzalisha mahindi akiahidi Serikali kununua mahindi hayo kwa bei ya soko  ambayo itamnufaisha mkulima.

Waziri Mkuu Majaliwa anaendelea na ziara mkoani Ruvuma, leo siku ya jumanne(Januari 5, 2016)  atatembelea na kukagua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kuongea na Watumishi wa hospitali hiyo  na baadae ataongea na Watumishi wa Umma.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,