WAZIRI
MKUU mstaafu Mizengo Pinda amekabidhi ofisi kwa Waziri Mkuu Kasim Majaliwa na
kumtaka aimarishe ufuatiliaji wa maelekezo anayoyatoa kwenda ngazi za chini.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano yaliyofanyika jana jioni (Jumatatu, Novemba 30, 2015), kwenye
ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, Bw.
Pinda alisema katika kipindi cha uongozi wake kulikuwa na ucheleweshaji wa
kupata majibu kutoka ngazi ya chini katika maelekezo aliyokuwa akitoa.
“Ofisi
ya Waziri Mkuu ni kubwa na ina mambo mengi ya kufuatilia. Kama kuna changamoto
nilikumbana nayo ni ucheleweshaji wa majibu kutokana na maagizo niliyokuwa
nikitoa. Itabidi uwe makini sana katika kufuatilia hili,” alisema Waziri Mkuu
mstaafu.
Alimtaka
ahakikishe kila idara inakuwa na mpango kazi na kunakuwa na ufuatiliaji wa kila
kilichopangwa. “Pia ninashauri uandaliwe kikao na watu wa Hazina ili wakueleze
jinsi bajeti ya Serikali inavyoandaliwa ili iwe rahisi kwako kufuatilia
vipengele kadhaa vya bajeti ya Serikali pindi maswali yanapoulizwa bungeni,”
alisema.
Pia
alimkabidhi taarifa yenye kurasa 104 ambayo inaelezea majukumu mbalimbali ya
taasisi na idara zilizo chini ya Ofisi wa Waziri Mkuu. Ofisi ya Waziri Mkuu ina
taasisi nane, idara nane na vitengo saba. Taasisi hizo ni Msajili wa Vyama vya
Siasa, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS),
Tume ya Uchaguzi (NEC) na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA). Nyingine ni
Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Baraza la Biashara la Taifa
(TNBC) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Idara
zilizopo kwenye ofisi hiyo ni Utawala na Rasimali watu, Sera na Mipango, Uratibu
wa Maadhimisho ya Kitaifa na Sekta binafsi na Uwezeshaji. Nyingine ni Bunge na
Siasa, uatibu wa shughuli za Serikali, Mpigachapa Mkuu wa Serikali na Ofisi
Binafsi ya Waziri Mkuu.
Alisema
pia ameridhishwa na kasi ya utendaji kazi ambayo Rais Dk. John Pombe Magufuli
na Waziri Mkuu wameanza nayo na kwamba ana imani kwa uchapakazi wao na uadilifu
wao, anaamini wataweza kuivusha Tanzania
na kuifikisha kwenye uchumi wa kati ambako Serikali imejielekeza kufika.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimshukuru Waziri Mkuu mstaafu na kumuahidi
kutekeleza yote yaliyomo kwenye taarifa aliyomkabidhi. Pia aliahidi kusimamia
kwa karibu suala la ufuatiliaji wa maelekezo anayotoa pamoja na yale yanayotoka
ngazi za juu.
Kikao
hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu, Dk. Florens Turuka, Naibu Katibu Mkuu
(OWM), Bibi Regina Kikuli, wakuu wa taasisi zote nane, wakuu wa idara na
vitengo vya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wasaidizi wa Waziri Mkuu walioko ofisi
yake binafsi.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,