Tuesday, July 19, 2016

NSSF YACHANGIA MILIONI 50 HARAMBEE YA UJENZI MPYA WA LINDI SEKONDARI


Shirika la Hifadhi ya Taifa ya Jamii NSSF Makao Makuu ikishirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Lindi Imechanga Jumla ya Shilingi Milioni 50 Kwa Ajili ya Kuchangia Harambee ya Kusaidia Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Lindi Iliyoungua Moto Wiki Iliyopita
Kwa Kutambua Umuhimu wa Elimu kwa  Watoto Shirika Hilo Kupitia Mkurugenzi Mkuu Wake ,Aliewakilishwa na Meneja wa Mkoa Bi Nour Aziz Limetoa ahadi hiyo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Majaliwa Kasim Majaliwa Alieongoza Harambee Hiyo Ambayo Ilihudhuriwa na Wadau Mbali mbali Akiwemo Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,Mama Salma Kikwete
Katika Harambee Hiyo Jumla ya Shilingi Milioni 80 Taslimu zilichangwa Huku Ahadi na Vifaa vya Ujenzi zikifikia Shilingi Milioni 640 Ambapo Katika Ujenzi Mpya Waziri Mkuu Ameagiza Kujengwa Jengo la Ghorofa litakalokuwa na Ofisi na  Madarasa
Katika Tukio Hilo la Moto,Jumla Ya Madarasa 9 na viti na Meza zaidi ya 300,Ofisi 4 na Vyoo Matundu 24  Viliteketea na Moto Uliotokana na hitilafu ya Umeme

MAJALIWA: MARUFUKU WANAFUNZI KUTUMIA VIBERITI, MISHUMAA MABWENINI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na hita za kuchemshia maji kwa wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya moto na atakayekutwa atachukuliwa hatua kali.
“Kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa vya kienyeji vya kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari kwani linaweza kusababisha ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 17, 2016) katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Lindi yaliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.
Katika ajali hiyo shule imeathirika kwa asilimia 34 ambapo vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya kemia na fizikia yameungua na kusababishia hasara ya sh. milioni 682.78.
Waziri Mkuu amesema kwa namna ambavyo majengo hayo yameungua ni vema yakavunjwa na kujengwa upya ambapo aliwataka kutumia nafasi hiyo kwa kujenga jengo la ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa kujenga madarasa mengi.
Pia alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kuhakikisha fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Harambee ilihudhuriwa na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa, mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, mama Salma Kikwete, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego pamoja na wadau wa maendeleo na wanafunzi waliosoma shule hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka taasisi mbalimbali nchini kufunga vifaa vya kuzimia moto katika majengo yao kwa ajili ya kuvitumia pindi ajali za moto zinapotokea.
(mwisho)
 IMETOLEWA NA:

Tuesday, March 08, 2016

WAZIRI MKUU: RUSHWA YAPOTEZA DOLA BILIONI 150 AFRIKA



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema tatizo la rushwa barani Afrika limesababisha bara hilo lipoteze dola za Marekani bilioni 150 kila mwaka.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 8, 2016) wakati akihutubia wajumbe wa mkutano wa tano wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linaloendesha vikao vyake jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulioanza Machi 6, utamalizika Machi 18, mwaka huu.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema rushwa imechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya Jumuiya hiyo. "Rushwa yaweza kuwa kwa njia kuhonga fedha, kupata fedha kwa kula njama, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, ama kwa njia za vitisho," alisema.

"Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Afrika (AU), rushwa na urasimu vimeainishwa kuwa ni vikwazo vikubwa vinavyochangia kuchelewesha ufanyaji wa biashara kwenye mipaka ya nchi za Jumuiya yetu," alisema.

Amesema sekta binafsi inachukuliwa kama injini ya maendeleo na ukuaji wa uchumi na akatumia fursa hiyo kuipongeza jumuiya ya wafanyabiashara wa Afrika Mashariki kwa kuandaa kanuni za kiutendaji  ambazo zimelenga kuhamasisha uadilifu kwenye ufanyaji biashara unaozingatia haki za binadamu, sheria za kazi, utunzaji mazingira na vita dhidi ya rushwa.

Akizungumzia kuhusu uondoaji wa vikwazo visivyohusisha kodi (non-tariff barriers) kama njia mojawapo ya kuimarisha biashara kwenye jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema kwa upande wa Tanzania, vizuizi vya barabarani kwenye barabara kuu ya Kaskazini vimepunguzwa kutoka 50 hadi vitano.

Alivitaja vizuizi vitano vilivyobakia kuwa ni vile vilivyopo kwenye mizni ya Mikese (Morogoro), Nala (Dodoma), Njuki (Singida), Mwendakulima (Shinyanga) na Nyakahura (Kagera).

"Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya uondoaji wa vikwazo visivyohusisha kodi ilipitishwa Machi 2015 na sasa hivi inaendelea kusainiwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pamoja na mambo mengie, nia ya sheria hii ni kuondoa vikwazo vinavyosababisha uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, kurahisisha sheria za biashara ndani ya Jumuiya yetu," alisema.

Akizungumzia kuhusu miradi ya uwekezaji ya Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema miradi ya ujenzi wa barabara inahitaji kiasi cha dola za marekani bilioni 20; ukarabati na upanuzi wa njia za reli unahitaji dola za marekani bilioni 30; uendeshaji wa mashirika ya ndege na viwanja vya ndege unahitaji dola za marekani bilioni 15; uendelezaji bandari na usafiri wa majini unahitaji dola za marekani bilioni 10; utekelezaji wa miundombinu ya nishati inahitaji dola bilioni 5 ambavyo kwa pamoja vinahitaji dola marekani bilioni 80.

Alisema kuwepo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ndani ya jumuiya hiyo, kunaifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhesabika kuwa ni jumuiya yenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Afrika.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMANNE, MACHI 8, 2016.

Saturday, February 13, 2016

SERIKALI YAWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI WAKALA WA VIPIMO TANZANIA



SERIKALI imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.

Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.

Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo (Ijumaa, Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.

“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.

Waziri Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.

Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.

Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).

Pia Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.

Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.

“Jana niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.




IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,

WAZIRI MKUU AFANYA TENA ZIARA YA GHAFLA BANDARINI



*Aibukia kitengo cha mita za kupimia mafuta Kurasini
*Akuta mafundi wakizitengeneza, akuta zimejaa kutu
*Ataka barua ya maelezo ifikapo saa 11 leo jioni


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara ya ghafla kwenye kitengo cha upimaji mafuta bandarini (Oil Flow Metres) na kukuta zimejaa kutu baada ya kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano. Pia alitembelea mita za kupimia mafuta zinazoendelea kujengwa Kigamboni.

Aidha, Waziri Mkuu amempa saa nne tu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita na amletee barua hiyo ofisini kwake ifikapo saa 11 leo jioni.

“Nataka unieleze ni kwa nini ulitoa maelekezo ya kufunga mita hizo, na kwa nini jana uliamua kubadili uamuzi huo? Ni kwa nini umeamua kuchukua maamuzi haya baada ya kupokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms) wakati mita zimekaa bila kufanya kazi kwa miaka mitano? Ni kwa nini umeamua kufanyia kazi ujumbe wa sms wakati unajua Serikali inafanya kazi kwa maandishi rasmi?” alisema Waziri Mkuu.

“Umesema mlikuwa mnatumia utaratibu wa kupima kwa kijiti. Huu hauna uhakika na huwezi kutegemea taarifa ya mtu mwingine au kuingia kwenye meli ya mtu na kuanza kuchukua vipimo hadi ujiridhishe. Nataka kujua ni kwa nini mlikuwa na utaratibu wa ku-bypass mafuta ili yasipite kwenye mita za kupimia mafuta? Ni kwa nini umetoa amri zianze kutengenezwa jana na siyo mwaka 2012 au 2013?” alihoji Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema mita hizo za Kurasini zilinunuliwa na Serikali kwa gharama za dola za marekani milioni 1.2 (wakati huo) na haiwezekani kuacha kuzitumia wakati watu wanachezea mifumo na kuongeza mianya ya kupoteza mapato kwa Serikali. Ameagiza mita hizo zianze kufanya kazi mara moja.

Wazir Mkuu alisema matumizi ya mita hizo yaliafikiwa na Serikali baada ya kubaini upotevu mkubwa wa kodi kwenye mafuta yanayoingizwa nchini na baada ya kuona hakuna tija ya kuendelea na ukadiriaji au kupokea taarifa za waagizaji peke yao.


Waziri Mkuu ambaye aliwasili Kurasini leo saaa 4: 30 asubuhi (Alhamisi, Februari 11, 2016) kwenye kitengo hicho kilichopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty), alikagua mita hizo na kisha kwenda kukagua meli iliyokuwa ikishusha mafuta bila kutumia mita hiyo ya kupima mafuta yanayopokelewa kwa sababu mafundi walikuwa bado wanaendelea na ukarabati.

Akiwa Kurasini, Waziri Mkuu alielezwa na Bibi Chuwa kwamba mita hizo zilianza kufanyiwa ukarabati jana na leo asubuhi moja imekamilika ambayo ni ya kupokelea mafuta ya petroli. Ya dizeli ilikuwa inafunguliwa na mafundi na kukutwa imejaa kutu sababu ya kutotumika kwa muda mrefu.

“Hii ya dizeli imefunguliwa leo na ile ya mafuta ya kula, haijawahi kufanya kazi tangu ilipofungwa mwaka 2011,” alielezwa Waziri Mkuu na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei.

Alipoulizwa ni kwa nini aliamua kuzifungia mita hizo ziisifanye kazi, Bi. Chuwa alijibu kuwa alifikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kwamba zinawapunja wateja. Hata hivyo, hakufafanua ni wateja gani au wa aina gani.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea na kukagua mita mpya za kupimia mafuta ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).

Akiwa hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba ujenzi huo ambao ulianza miezi nane iliyopita, unatarajiwa kukamilika ifikapo katikati ya mwezi Machi, 2016. “Tunajitahidi kazi hii ikamilike ifikapo katikati ya mwezi ujao,” alisema Eng. John Bura, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BQ Contractors Ltd ambayo inasimamia ujenzi wa mita hizo.

Vilevile, Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia bainaya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.

Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.

“Natoa mwezi mmoja hili bomba liondolewe kwenye mfumo huu na kama yapo mabomba mengine pia yaondolewe,” alisema huku akionyesha karatasi iliyokuwa mfukoni kwake yenye mchoro unaobainisha kuwa kuna bomba jingine la inchi 10 limeungwa kinyemela kwenye bomba kuu.

“Kila mmoja anapaswa aje kuchukua pale kwenye manfold ili tujue nani kachukua nini. Msajili wa Hazina hili ni eneo lako na wewe unamiliki TIPER kwa asilimia 50, hebu simamia hili. Ninyi TPA leteni mapendekezo yenu Serikalini ili tuone tunaweza kudhibiti vipi vitendo kama hivi,” alisema Waziri Mkuu.

Pia alimtaka Msajili wa Hazina, Bw. Lawrence Mafuru awasiliane na Mwanasheria Mkuu ili waangalie upya mkataba na umiliki wa matenki hayo uwe chini ya Serikali kwa asilimia 100 ili mafuta yanayoagizwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency) yaweze kuhifadhiwa huko.

Mapema, Waziri Mkuu ambaye alifuatana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alikagua eneo la manfold ya Mamlaka ya Bandari iliyopo Kigamboni na kukuta ni kampuni nne tu zenye matenki Kigamboni ambazo zinachukua mafuta yao hapo.

Kampuni hizo ni HASS, WORLD OIL, LAKE OIL na MOIL. TIPER haikutaka kufuata mfumo huo licha ya kuwa nafasi ya kufanya hivyo ipo. Kampuni nyingine zenye matenki yake nchi kavu, zinachukulia mafuta kwenye manfold ya Kurasini.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,

Tuesday, January 05, 2016

MAKATIBU WAKUU WAPYA OFISI YA WAZIRI MKUU WAANZA KAZI RASMI LEO




PICHA NO. 1
Katibu Mkuu Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. FlorenS Turuka ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (wa pili kulia) akisitiza jambo wakati makatibu wakuu wapya wa Ofisi ya Waziri Mkuu walipokutana na Menejimenti ya Ofisi hiyo (hawapo pichani) leo, tarehe 4 Januari, 2016, kulia kwake ni Katibu Mkuu (Bunge) Mussa Uledi, (wa kwanza kushoto) ni Katibu Mkuu (Kazi na Ajira) Erick Shitindi na (wapili kushoto) ni Katibu Mkuu (Sera) Dkt. Hamis Mwinyimvua.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PICHA NO.2
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwasikiliza makatibu wakuu wapya (hawapo pichani) wakati makatibu wakuu hao (hawapo pichani) walipokutana na Menejimenti hiyo leo, tarehe 4, 2016 Januari katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dar es salaam.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PICHA NO.3
Katibu Mkuu (Kazi na Ajira), Erick Shitindi akisisitiza jambo wakati wa kikao na  Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu (hawapo pichani) alipowasili katika Ofisi hiyo na makatibu wakuu wapya wengine wa Ofisi hiyo , leo, tarehe 4 Januari 2016,  (kulia kwake ) ni, Katibu Mkuu (Sera) Dkt. Hamis Mwinyimvua.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PICHA NO.4
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwasikiliza makatibu wakuu wapya (hawapo pichani) wakati makatibu wakuu hao (hawapo pichani) walipokutana na Menejimenti hiyo leo, tarehe 4 Januari, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dar es salaam.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PICHA NO.5
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwa na Makatibu wakuu wapya Katibu Mkuu, (Bunge) Mussa Uledi, (wa pili kushoto) pamoja na aliye kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo ambaye sasa ni Katibu Mkuu Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. FlorenS Turuka (wa tatu kutoka kushoto), Katibu Mkuu (Kazi na Ajira), Erick Shitindi (katikati) na Katibu Mkuu (Sera) Dkt. Hamis Mwinyimvua (watatu kutoka kulia) mara baada ya makatibu wakuu hao kukutana  na Menejimenti hiyo leo, tarehe 4 Januari, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)